Shirika la Afya Duniani (WHO)
limetangaza kuwa, zaidi ya watu 26,000 wameambukizwa virusi vya homa
hatari ya Ebola tangu ugonjwa huo ulipoibuka mwishoni mwa mwaka 2013.
Taasisi hiyo ya Umoja wa Mataifa imebainisha katika ripoti yake ya hapo
jana kwamba, watu 26,079 wameambukizwa virusi vya Ebola, wengi wao
wakiwa ni raia wa nchi tatu za Kiafrika za Liberia, Guinea na Sierra
Leone tangu virusi hivyo vilipoibuka Disemba mwaka 2013. Aidha ripoti
hiyo ya WHO imeeleza kuwa, 10,823 kati ya walioambukizwa wameshafariki
dunia. Taarifa zaidi zinasema kuwa, kiwango cha maambukizi ya virusi
hivyo kimepungua kutokana na watu 33 tu kuripotiwa kuambukizwa virusi
hivyo kwa wiki. Aidha Liberia ambayo ni miongoni mwa nchi zilizoathiriwa
zaidi na virusi vya Ebola, haijaripoti kesi mpya ya kupoteza mtu maisha
kwa homa hiyo tangu mgonjwa wa mwisho aage dunia mwezi uliopita wa
Machi. Mwezi ujao wa Mei Liberia inataraji kutangaza kutokomezwa maradhi
hayo nchini humo endapo hakutaripotiwa kesi mpya ya maambukizi. Dalili
za Ebola ni homa kali, kuharisha, kutapika na kutokwa damu katika sehemu
mbalimbali mwilini. Mtu anaweza kuambukizwa ugonjwa huo kwa kugusa
kinyesi na majimaji ya aina zote yanayotoka kwa mgonjwa kama vile damu,
mate na hata jasho.
No comments:
Post a Comment