Chama tawala nchini Burundi cha
CNDD-FDD leo kimemtangaza rasmi Rais Pierre Nkurunziza wa nchi hiyo kuwa
ndiye atakayepeperusha bendera ya chama hicho katika uchaguzi ujao wa
Rais mwezi Juni mwaka huu. Akitangaza uamuzi huo katika mkutano wa
CNDD-FDD uliofanyika leo mjini Bujumbura, mwenyekiti wa chama hicho
Pascal Nyabenda amesema kama ninavyomnukuu: “Tuna furaha kuwatangazia
wananchi wa Burundi na ulimwengu kwa ujumla kwamba, chama cha CNDD-FDD
kimemteua Rais Nkurunziza kuwa mgombea wake katika uchaguzi ujao wa
Rais”. Mwisho wa kunukuu. Mwenyekiti huyo wa chama tawala nchini Burundi
amesema kuwa, wanawataka wapinzani wao kuwa watulivu na kwamba,
wakachuane na Rais Nkurunziza katika masanduku ya kupigia kura. Aidha
amesema, chama hicho kinavitaka vikosi vya usalama na polisi
kuwachukulia hatua wale wote watakaojitokeza barabarani kupinga uamuzi
huo. Wakati huo huo, vyama vya upinzani nchini Burundi vimeapa kwamba,
vitasimama kupinga uamuzi huo ambao vimesema unakinzana wazi na katiba
hasa kwa kutilia maanani kwamba, kiongozi huyo ameshaingoza nchi hiyo
kwa duru mbili. Taarifa zaidi zinasema kuwa, uamuzi huo unaweza kuzusha
machafuko katika nchi hiyo ambayo imeshuhudia amani na utulivu tangu
mwaka 2005 baada ya kumalizika vita vya wenyewe kwa wenyewe
No comments:
Post a Comment