Wanamgambo wa kundi la kigaidi na
kitakfiri la Boko Haram wamewalazimisha mamia ya askari wa Nigeria
kuukimbia mji wa mpakani wa Marte ulioko kwenye fukwe za Ziwa Chad. Kwa
mujibu wa Imamu Habeeb, ambaye ni kiongozi wa eneo hilo pamoja na
mashuhuda wa tukio hilo magaidi wa Boko wapatao 2,000 walichomoza
kutokea pande tofauti na kupambana na askari wa jeshi la Nigeria. Kwa
mujibu wa bwana Habeeb mapigano hayo yalizuka siku ya Alkhamisi usiku na
kuendelea hadi jana. Shehu Dan Baiwa, ambaye ni mmoja wa wanamgambo wa
kujitolea katika jimbo la Borno amesema idadi ya wapiganaji hao wa Boko
Haram ilikuwa zaidi ya elfu mbili wakiwa wamejizatiti kwa mabomu na
vifaru. Amesema wanamgambo hao walikuwa wakifyatua risasi ovyo na kuua
watu kadhaa. Hii ni mara ya tatu kwa kundi la kigaidi la Boko Haram
kuushikilia tena mji wa Marte katika jimbo la Borno ambalo ni kitovu cha
uasi wa kundi hilo unaoendelea kwa mwaka wa sita sasa na kusababisha
vifo vya watu 13,000 na wengine milioni moja na nusu kubaki bila
makaazi. Marte ulikuwa mmoja wa miji kadhaa iliyokombolewa na jeshi la
Nigeria katika wiki za hivi karibuni lililoanzisha operesheni maalumu
dhidi ya Boko Haram kwa msaada wa majeshi ya Chad, Cameroon na Niger.
Mwanasiasa mmoja wa mji wa Marte ambaye hakutaka jina lake litajwe
amethibitisha kushikiliwa tena mji huo na magaidi wa kundi la kitakfiri
la Boko Haram. “Tumepoteza watu wengi, kwa sababu baadhi ya watu wetu
waliokuwa wamekimbilia Chad walirudi baada ya askari wa Nigeria
kuukomboa mji hivi karibuni” ameeleza mwanasiasa huyo. Hata hivyo afisa
mmoja wa jeshi la Nigeria aliyethibitisha kutokea shambulio hilo la Boko
Haram katika mji wa Marte amekataa kusema kuwa mji huo umeshikiliwa
tena na kundi hilo na kueleza kwamba kuondoka kwa jeshi kumefanyika
katika sura ya mbinu na mkakati wa kivita…/
No comments:
Post a Comment