Gavana wa jimbo la Darfur ya Kusini
nchini Sudan amewatuhumu askari wa vikosi vya kulinda amani vya Umoja wa
Afrika na Umoja wa Mataifa katika eneo la Darfur UNAMID kuwa wameua
raia saba wasio na hatia katika jimbo hilo. Adam Jarunnabiy, amesema
askari wa UNAMID wamewaua kwa kuwapiga risasi raia saba wasio na ulinzi
katika eneo la Kaas jimboni humo. Ameongeza kuwa tayari tume ya
kuchunguza mauaji ya raia hao saba wa Sudan imeshaundwa. Kwa mujibu wa
gavana huyo wa Darfur ya Kusini, kundi la waasi lilipora gari moja la
vikosi vya kulinda amani vya UNAMID na kwamba wakati askari wa vikosi
hivyo waliopokuwa wakiwafukuza waasi hao waliwafyatulia risasi na kuwaua
raia ambao walikuwa hawahusiki kwa namna yoyote ile na tukio la wizi wa
gari hilo. Kumekuwepo na malalamiko mengi ya raia wa Sudan kuhusiana na
uwezo wa vikosi vya UNAMID katika kulinda amani na kudhamini usalama wa
raia hao kiasi cha kuifanya serikali ya Khartoum iutake Umoja wa Afrika
na Umoja wa Mataifa ziviondoe vikosi hivyo nchini humo. Darfur ya
Kusini ni moja ya majimbo matano yanayounda eneo la Darfur lililoko
magharibi mwa Sudan. Darfur ni eneo lenye utajiri mkubwa wa mafuta na
maliasili nyenginezo yakiwemo madini ya urani na dhahabu, suala ambalo
limesababisha kuzuka uasi wa utumiaji silaha ulioanza tangu mwaka 2003
na kuendelea hadi sasa…
No comments:
Post a Comment