Duru za habari nchini Kenya
zimeripoti taarifa ya kutekwa nyara kiongozi mmoja wa serikali ya nchi
hiyo na kundi la kigaidi na kitakfiri la ash-Shabab la nchini Somalia.
Mukhtar Maalim Adan, ambaye ni afisa utawala katika mji wa Mandera
nchini Kenya, ametekwa nyara na kundi hilo ambalo limekuwa likitekeleza
mashambulizi ya mara kwa mara nchini humo. Maafisa wa polisi wamesema
kuwa, Mukhtar ametekwa nyara alipokuwa safarini kutoka mjini Mandera
kuelekea moja ya miji ya nchi hiyo ya Afrika Mashariki ambapo alivamiwa
na wanachama wa kundi hilo na kisha kuchukuliwa kwa gari lake na
kupelekwa kusikojulikana. Hadi sasa polisi bado haijafanikiwa kunasa
gari ya Mukhtar Adan na ingali inaendelea na uchunguzi kuwabaini
wahusika wa tukio hilo. Hata hivyo polisi ya Kenya ina wasi wasi kwamba
huwenda kiongozi huyo wa serikali akawa amepelekwa Somalia na kundi hilo
la kigaidi. Mji wa Mandera uko katika mpaka wa pamoja wa Kenya na
Somalia ambapo unatajwa kuwa njia mojawapo muhimu inayotumiwa na
wanachama wa ash-Shabab kuingilia nchini Kenya na kutekeleza uhalifu
wao. Licha ya kwamba hadi sasa hakuna kundi lolote lililotangaza
kuhusika na tukio hilo la utekaji nyara, lakini kidole cha lawama
kimeelekezwa kwa kundi hilo ambalo wiki kadhaa zilizopita, lilitekeleza
hujuma kali dhidi ya Chuo Kikuu cha mji wa Garissa kaskazini mashariki
mwa Kenya na kuua watu 150 wengi wao wakiwa ni wanafunzi.
No comments:
Post a Comment