Mahakama moja nchini Misri imewahukumu adhabu ya kifo watu 11
baada ya kuwapata na hatia ya kushiriki katika machafuko ya kwenye
uwanja wa mpira katika mji wa Port Said, miaka mitatu iliyopita. Hukumu
hiyo imetolewa leo kuhusiana na machafuko hayo ya mwaka 2012 ambayo
yalipelekea watu 74 kuuawa. Hukumu iliyotolewa mwezi Februari 2014 na
mahakama moja ya chini dhidi ya watuhumiwa 73 ilikatiwa rufaa baada ya
kuwahukumu kifo watu 21 kwa kosa la kushiriki kwenye machafuko hayo.
Hukumu ya adhabu ya kifo dhidi ya mashabiki 11 wa mpira imepelekwa kwa
Mufti Mkuu wa Misri na mahakama itaamua hatima yao pamoja na hatima ya
watuhumiwa wengine, Mei 30 mwaka huu. Mashabiki wenye misimamo mikali
mara nyingi huwa wanapambana na polisi wakati wa mechi nchini Misri.
Machafuko ya mwezi Februari 2012 yalitokea wakati mashabiki wa timu
mwenyeji ya al Masry walipopambana na mashabiki wa timu ya al Ahly ya
Cairo wakati wa mechi ya timu hizo mbili. Hata mwanzoni mwa mwezi
Februari mwaka huu pia, watu kadhaa waliuawa baada ya kutokea machafuko
kati ya mashabiki na polisi wakati wa mechi kati ya timu ya Zamalek na
ile ya Enppi, mjini Cairo
No comments:
Post a Comment