Jeshi la Sudan Kusini limetangaza kuwa, linajiandaa na vita vya
miaka kumi dhidi ya waasi katika nchi hiyo changa zaidi barani Afrika.
Makamanda wa jeshi la Sudan Kusini wakishirikiana na wenzao wa jeshi la
UgandaUPDF wamo katika maandalizi ya vita vya miaka kumi dhidi ya
makundi ya waasi. Makamanda wa jeshi la Sudan Kusini wanatabiri kwamba,
waasi wanaoongozwa na Riek Machar aliyekuwa makamu wa Rais wa Sudan
Kusini hawatasalimu amri kwa haraka hivyo jeshi la nchi hiyo linapaswa
kuweka malengo ya vita ya miaka kumi. Jeshi la Sudan Kusini limekuwa
likisaidiwa na jeshi la Uganda UPDF katika juhudi za kuwatokomeza waasi
wa nchi hiyo wanaoongozwa na Riek Machar. Hayo yanajiri katika hali
ambayo, Umoja wa Afrika unaendelea na upatanishi wake wa mgogoro wa
Sudan Kusini ambapo siku ya Jumamosi uliitisha mkutano wa pande mbili
hasimu za nchi hiyo. Umoja wa Afrika ulipendekeza katika mkutano huo
kwamba, pande mbili hasimu huko Sudan Kusini kila mmoja upatiwe asilimia
40 ya madaraka, asilimia kumi ipewe miungano na vyama vya kisiasa na
asilimia kumi iliyobakia apewe Pagan Amum, Katibu Mkuu wa zamani wa
chama tawala.
No comments:
Post a Comment