Makundi hasimu nchini Libya yameanza kutekeleza makubaliano ya
kusimamisha vita kwa muda wa siku kumi katika mji wa bandari wa Sirte wa
kaskazini mwa nchi hiyo. Gazeti la Bawwabatul Wasat la Libya limeripoti
kuwa, lengo la usimamishaji vita huo wa muda ulioanza jana Jumatatu ni
kutoa fursa ya kufanya mazungumzo na kundi la kitakfiri la Daesh. Kwa
mujibu wa gazeti hilo, makundi yote yanayohusika na mgogoro wa Libya
yamekubaliana na usitishaji vita huo. Huku hayo yakiripotiwa, taarifa
nyingine zinasema kuwa, kumetokea mripuko wa bomu kwenye ubalozi wa
Uhispania huko Tripoli, mji mkuu wa Libya. Hata hivyo hakuna taarifa
zozote zilizotolewa kuhusiana na hasara kamili zilizosababishwa na
mripuko huo uliotokea usiku wa kuamkia leo. Taarifa za awali zinasema
kuwa mripuko huo umesababisha uharibifu katika eneo la ubalozi huo na
kwenye majengo jirani. Kundi la kigaidi la Daesh ndilo linalonyooshewa
kidole cha lawama kutokana na kufanya mashambulizi kama hayo ya
kuwalenga wageni nchini Libya kwa muda mrefu sasa.
No comments:
Post a Comment