Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesema kuwa, jeshi la
polisi ni dhihirisho la nguvu za utawala na usalama za Jamhuri ya
Kiislamu ya Iran.
Ayatullahil Udhma Sayyid Ali Khamenei amesema hayo
leo Jumapili wakati alipoonana na washiriki wa kongamano la makamanda,
wakuu na wakurugenzi wa Jeshi la Polisi la Iran na kusisitiza kuwa,
miongoni mwa majukumu makuu ya polisi ni kudhamini usalama wa watu
binafsi, wa kijamii, wa kimaadili, wa kiroho na wa kisaikolojia katika
jamii.
Ameongeza kuwa, jeshi la polisi linapaswa kuwa chombo chenye
nguvu ili liweze kulinda usalama lakini nguvu hizo zinapaswa kuchunga
uadilifu, murua na huruma.
Aidha amesema, vituko vinavyofanywa
barabarani na baadhi ya vijana waliolewa ghururi za utajiri kwa kutumia
magari ya kifakhari ni aina moja ya kuhatarisha usalama wa kisaikolojia
katika jamii na kusisitiza kuwa: Jeshi la Polisi linapaswa kupambana na
vitendo vya aina zote vya kuhatarisha amani.
Ayatullahil Udhma
Khamenei amesisitiza pia kuwa Iran haitaki kuwa na nguvu za jeshi la
ki-Hollywood na za jamii za Magharibi na Marekani na kubainisha kwamba:
Nguvu za aina hiyo si tu kwamba haziwezi kudhamini usalama, bali zenyewe
ni aina moja ya mambo yanayohatarisha usalama.
Kiongozi Muadhamu wa
Mapinduzi ya Kiislamu amegusia pia namna polisi wa Marekani
wanavyowakandamiza watu weusi nchini humo na kusema kuwa, huo ni moja ya
mifano ya nguvu za kidhulma za polisi.
Ameongeza kuwa: Polisi wa
Marekani wanawafanyia dhulma kubwa na kuwanyanyasa vibaya watu weusi
licha ya kwamba rais wa hivi sasa wa nchi hiyo ni mtu mweusi, na vitendo
hivyo bila ya shaka yoyote ndivyo vinavyopelekea kuzuka machafuko
nchini humo
No comments:
Post a Comment