Makamu wa Rais wa Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania, Dk. Mohammed Gharib Bilal amesema kuwa, uharibifu
wa mazingira katika nchi zinazoendelea ni kati ya sababu zinazofanya
nchi hizo ziendelee kuwa maskini. Dakta Gharib Bilal amesema kuwa, upo
uhusiano mkubwa kati ya mazingira na umaskini kwa maana kwamba,
uharibifu wa mazingira unachangia kuongezeka kwa umaskini na kwamba
kadri hali ya umaskini inavyoongezeka inasababisha uharibifu wa
mazingira. Makamu wa Rais wa Tanzania ameongeza kuwa, kwa msingi huo
umuhimu wa kulinda na kuhifadhi mazingira nchini unachochewa zaidi na
ukweli kwamba mazingira ni mhimili wa sekta za uzalishaji kama vile
kilimo, utalii, uvuvi na madini. Aidha amebainisha kuwa, changamoto
iliyopo ni kuhakikisha mazingira na maliasili za Tanzania zinatumika
katika njia endelevu kwa kuzingatia uwiano mzuri kati ya matumizi ya
maliasili, hifadhi zake na uwezo wake kuendelea kutoa huduma. Makamu
huyo wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania amebainisha kuwa, ili
kusimamia masuala ya hifadhi ya mazingira kwa ufanisi ni lazima
kudhibiti shughuli za binadamu zinazoathiri mazingira, masuala ya
kijamii na kiuchumi kama vile ongezeko la watu, na shughuli za kiuchumi
zinazoendana na matumizi yasiyo endelevu ya mazingira zinazoweka
shinikizo kubwa katika mazingira na kusababisha uharibifu.
No comments:
Post a Comment