Mashambulio ya anga ya Saudi Arabia yanayoendelea kushuhudiwa
nchini Yemen licha ya malalamiko ya jamii ya kimataifa yamelenga mitambo
na vituo kadhaa vya mawasiliamo magharibi na kaskazini magharibi mwa
nchi hiyo. Waziri wa Usafiri wa Yemen amesema kuwa, ndege za kijeshi za
Saudia zimeshambulia na kulenga mitambo ya kurushia matangazo ya
televisheni katika mji mkuu Sana’a na katika miji ya Sa’ada na Amran.
Taarifa zaidi zinasema kuwa, mashambulio hayo yaliyofanywa kwa makusudi
yalikusudia kukata nyenzo za mawasiliano zinazotumiwa na wanamapinduzi
wa Harakati ya al-Houthi. Baadhi ya duru zinaripoti kwamba, mawasiliano
ya simu yamevurugika huku huduma ya Intaneti ikikatika katika miji hiyo
mitatu kufuatia mashambulio hayo yaliyolenga vituo na mitambo ya
mawasiliano. Wakati huo huo mashirika mbalimbali ya utoaji misaada
yametahadharisha kwa mara nyingine tena kwamba, mgogoro wa Yemen
unaelekea pabaya kutokana na kuwa mbaya hali ya kibinadamu katika nchi
hiyo. Familia nyingi katika baadhi ya miji hazipati huduma muhimu kama
maji, chakula na dawa, huku watoto wakiwa ndio wahanga wakuu wa
mashambulio ya sasa ya anga ya Saudia huko Yemen, imebainisha taarifa ya
mashirika hayo.
No comments:
Post a Comment