Waziri wa Mambo ya Nchi za Nje wa Marekani amewataka wajumbe wa
kongresi ya nchi hiyo wasiingilie mazungumzo yanayoendelea ya nyuklia
kati ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na kundi la 5+1, kabla ya kumalizika
muhula uliopangwa wa kumalizika mazungumzo hayo tarehe 30 Juni mwaka
huu. Kwenye mahojiano aliyofanyiwa na Kanali ya Televisheni ya CBS ya
Marekani, John Kerry amesema kuwa, kuanzia leo na kesho atatoa ufafanuzi
kamili kwa wajumbe wa kongresi juu ya makubaliano yaliyofikiwa hivi
karibuni huko Lausanne, Uswisi. Wakati huohuo, Rais Barack Obama wa
Marekani amesema kuwa, mizozo na mivutano ya kichama na kimirengo
kuhusiana na kadhia ya nyuklia ya Iran yenye malengo ya amani na masuala
mengine yanayohusiana na sera za kigeni za Washington inapaswa
kusimamishwa. Rais Obama ameyasema hayo kwenye kikao cha kila mwaka cha
wakuu wa nchi za bara la Amerika, kinachofanyika nchini Panama. Wiki
iliyopita, Seneta John Sidney Mc Cain alisema kuwa, maelezo yaliyotolewa
na viongozi wa Iran kuhusiana na makubaliano ya Lausanne ni sahihi
zaidi na ya kimantiki zaidi, kuliko yale yaliyotolewa na John Kerry
Waziri wa Mambo ya Nchi za Nje wa Marekani. Hii ni katika hali ambayo,
Maseneta wa mrengo wa Republican wanataka kukwamisha kufikiwa
makubaliano ya mwisho, bila ya kuzingatia tahadhari iliyotolewa na
serikali ya Obama ya kuwataka wajiepushe na uingiliaji wa mazungumzo
hayo ya nyuklia. Maseneta hao wanashinikiza makubaliano ya mwisho ya
nyuklia lazima yachunguzwe na kuangaliwa pia na wajumbe wa kongresi.
No comments:
Post a Comment