Sambamba na kukaribia siku ya
kusikilizwa kesi ya Sheikh Ali Salman, Katibu Mkuu wa harakati ya
Kiislamu ya Al Wifaq, wananchi wa Bahrain wamefanya maandamano makubwa
katika mji mkuu wa nchi hiyo Manama wakitaka kiongozi huyo pamoja na
wafungwa wengine wote wa kisiasa waachiwe huru na kukomeshwa vitendo vya
ukatili na ukandamizaji vya utawala wa Aal Khalifa dhidi ya raia.
Sheikh Ali Salman, ambaye ni mmoja wa maulamaa mashuhuri wa Bahrain na
Katibu Mkuu wa harakati muhimu zaidi ya kisiasa ya nchi hiyo alitiwa
nguvuni na vikosi vya utawala wa Aal Khalifa mwishoni mwa mwaka jana.
Kwa upande mwengine wananchi wa Bahrain
siku ya Jumamosi, ambayo imo kwenye masiku ya mnasaba wa kukumbuka
tukio la kubomolewa makumi ya misikiti na vikosi vya utawala wa Aal
Khalifa, walisali Sala za Adhuhuri na Alasiri kwenye magofu ya msikiti
wa Ainun Rastan kwenye eneo la Aali, katika mji mkuu Manama. Waumini
walioshiriki kwenye Sala hizo za jamaa waliutaka utawala wa Aal Khalifa
uache kuhujumu na kukandamiza uhuru wa kuabudu. Wananchi wa Bahrain
walisali Sala za jamaa za Magharibi na Isha pia katika magofu ya msikiti
wa Al Alawiyyat uliokuwa kwenye eneo la Az Zanj, ambao pamoja na
misikiti mingine 37 ulibomolewa na kusawazishwa na ardhi katika ubomoaji
misikiti uliofanywa na utawala wa Aal Khalifa mnamo mwaka 2011. Inafaa
kuashiria hapa kuwa hakuna aina yoyote ya jinai na ukatili ambao
haujafanywa na utawala wa kifalme wa ukoo wa Aal Khalifa katika
kuwakandamiza wananchi wa Bahrain. Kuanzia mauaji na kuwatia korokoroni
wanaharakati wa kisiasa, mpaka kuharibu na kubomoa majengo ya kidini na
ya ibada ni jumla ya jinai na ukandamizaji unaofanywa na utawala wa
kiimla wa Aal Khalifa. Ilikuwa ni kutokana na siasa hizo za kidikteta na
ukandamizaji ndipo mnamo mwezi Februari mwaka 2011, wananchi wa Bahrain
walianzisha harakati dhidi ya utawala wa Mfalme Hamad bin Issa Aal
Khalifa ya kudai mageuzi ya kisiasa, kiuchumi na kijamii. Lakini jibu la
utawala huo ambao umekuwa ukisaidiwa na askari wa vikosi vya kigeni
hususan wa Saudi Arabia ni kushadidisha ukandamizaji pamoja na kuwatia
nguvuni na kuwatesa wapinzani. Matokeo ya sera hizo za ukandamizaji za
utawala wa Aal Khalifa katika kipindi cha miaka minne hadi sasa ni
kushuhudiwa maelfu ya wafungwa wa kisiasa kwenye jela za nchi hiyo. Kwa
mujibu wa duru za habari, kuna wafungwa wa kisiasa wapatao elfu kumi
nchini Bahrain ambao kutokana na idadi ya raia wote wa nchi hiyo,
wameufanya utawala wa Aal Khalifa kuwa moja ya tawala zenye wafungwa
wengi zaidi wa kisiasa waliofurika kwenye magereza yake. Vitendo vya
utawala wa Aal Khalifa vinadhihirisha jinsi utawala huo usivyoheshimu si
uhuru wa kisiasa tu wa wananchi wa Bahrain, bali unavyowanyima pia
wananchi hao haki zao nyengine za msingi ikiwemo ya kuabudu na kufanya
shughuli zao za kidini kwa uhuru. Msingi wa siasa za utawala wa Aal
Khalifa ni kushadidisha vitendo vya kuvunjia heshima matukufu ya kidini
ya wananchi hususan Waislamu wa Kishia ambao ndio wanaounda idadi kubwa
zaidi ya raia wa Bahrain. Kutokana na dhana potofu uliyonayo, utawala wa
Manama unadhani kwamba kwa kubomoa misikiti na kuvunjia heshima
matukufu ya kidini ya wananchi utaweza kuwafanya wananchi hao waghairi
kuendeleza mapambano yao dhidi ya mfumo wa kifalme unaoitawala Bahrain.
Matukio yanayojiri Bahrain yanadhihirisha wazi kwamba hatua za utawala
wa Aal Khalifa za kupiga vita dini na kuwanyima raia haki zao sio tu
hazijaweza kuiyumbisha hata chembe harakati ya wananchi hao, bali badala
yake zimezidi kufichua na kuweka wazi zaidi mbele ya fikra za
waliowengi sura halisi ya kidikteta ya watawala wa Bahrain na kukoleza
zaidi moto wa upinzani wa wananchi dhidi ya utawala huo…/
No comments:
Post a Comment