Watu 18 wameteketea kwa moto katika ajali ya barabarani nchini
Tanzania baada ya basi la Kampuni ya Nganga Express na lori aina ya Fuso
kugongana uso kwa uso na kuwaka moto katika eneo la Iyovi, Milima ya
Uduzungwa, mkoani Morogoro. Katika ajali hiyo iliyotokea abiria 15
waliokuwa kwenye basi na wengine watatu wa lori waliteketea kwa moto
huku wengine 10 wakijeruhiwa vibaya. Kamanda wa Polisi Mkoa wa
Morogoro, Leonard Paul amesema kuwa, ajali hiyo ilitokea baada basi
hilo lililokuwa linatoka Kilombero kwenda Mbeya likiwa kwenye mistari ya
barabarani ya katazo na kwenye mwendo kasi kugongana na lori lililokuwa
limebeba matikiti na kuwaka moto. Alisema majeruhi wanne wamelazwa
katika Hospitali ya St. Kizito, Mikumi na sita wako katika Hospitali ya
Mtandika, Iringa. Kamanda wa Polisi Mkoa wa Morogoro ameongeza kuwa,
kwenye basi hilo kulikuwa na pikipiki ambayo pia iliungua inawezekana
ndiyo iliyosababisha moto huo. Ajali hiyo ni mfululizo wa ajali
zinazotokea katika maeneo mbalimbali nchini Tanzania juma hili, ikiwa ni
siku moja baada ya watu watano kufariki dunia na wengine kadhaa
kujeruhiwa katika mikoa ya Dodoma na Iringa. Tanzania imekuwa
ikishuhudia ajali za mara kwa mara za barabarani ambapo makumi ya watu
wamekuwa wakipoteza maisha yao. Uzembe wa madereva na mwendo wa kasi
zinatajwa kuwa sababu kuu zinazosababisha mlolongo wa ajali nchini
Tanzania.
No comments:
Post a Comment