Watu 13 wamepoteza maisha yao nchini Yemen kufuatia mashambulio
ya anga ya vikosi vamizi vya Saudi Arabia. Mashambulio hayo ambayo
yamepelekea pia watu wasiopungua 70 kujeruhiwa yalilenga maeneo ya soko
na makazi ya raia katika mji wa Haraz, kaskazini magharibi mwa jimbo la
Hajjah. Msemaji wa Harakati ya wananchi ya Ansarullah amesema kuwa,
mashambulio ya utawala wa kifamilia wa Aal Saud dhidi ya wananchi wa
Yemen ni jinai dhidi ya binadamu. Muhammad Abdus Salaam amebainisha
kwamba, hatua ya Saudia ya kuwauwa kwa umati wananchi wa Yemen na
kutokomeza miundo mbinu muhimu ya nchi hiyo umeufanya utende jinai mbaya
kabisa dhidi ya binadamu. Wakati huo huo vyama vinavyounda Muungano wa
Kitaifa wa Demokrasia nchini Yemen vimetangaza kuwa, Saudi Arabia
imepuuza matakwa yote ya kimataifa ya kusitisha mauaji dhidi ya raia wa
Yemen na kuacha kuharibu miundo mbinu ya nchi hiyo. Vyama hivyo aidha
vimelaani mashambulio hayo ya Saudia ambayo yamekuwa yakiwauwa raia
wasio na hatia yoyote na kusisitiza kwamba, Baraza la Usalama la Umoja
wa Mataifa linapaswa kuichukulia hatua Saudia kutokana na kutenda jinai
dhidi ya binadamu
No comments:
Post a Comment