Zaidi ya watu 1,400 wamepoteza
maisha yao kufuatia mtetemeko mkubwa wa ardhi wenye ukubwa wa 7.9 kwa
kipimo cha rishta uliotokea magharibi mwa Nepal karibu na mji mkuu
Kathmandu. Mtetemeko huo uliotokea majira ya mchana kwa wakati wa Nepal
umeutikisa vibaya mji mkuu Kathmandu ambapo mbali na kupelekea mamia ya
watu kupoteza maisha na maelfu ya wengine kujeruhiwa, umesababisha
uharibifu mkubwa wa nyumba. Waziri wa Habari wa Nepal Minendra Rijal
amewaambia waandishi wa habari kwamba, mji mkuu Kathmandu ndio
ulioathiriwa zaidi na baa hilo la kimaumbile. Idadi ya waliopteza maisha
katika mtetemeko huo wa ardhi inakadiriwa kuwa, itaongezeka hasa
kutokana na kuwa, watu wengi wamefukiwa na vifusi. Habari zaidi zinasema
kuwa, majengo na majumba mengi yakiwemo ya kihistoria yamebomolewa na
kuharibiwa kabisa na tetemeko hilo la ardhi. Waziri wa Habari wa Nepal
amesema kuwa, timu maalumu ya uokozi tayari imetumwa katika maeneo
yaliyokumbwa na mtetemeko huo wa ardhi na kwamba, kazi ya uokozi
inaendelea. Mtetemeko huo wa ardhi umeitikisa pia nchi jirani ya
Bangladesh na taarifa kutoka nchini humo zinasema, watu wawili
wamepoteza maisha na wengine mia moja wamejeruhiwa kufuatia janga hilo
la kimaumbile. Aidha mji mkuu wa India New Delhi na baadhi ya miji ya
mashariki mwa nchi hiyo nayo imekumbwa na mtetemeko huo wa ardhi.
No comments:
Post a Comment