Nyaraka za siri zilizokuwa
zimefichwa kwenye masjala ya Wakala wa Usalama wa Taifa wa Marekani NSA
zinaonyesha kuwa, Marekani ilikuwa na mpango wa kushambulia kwa
makombora vinu na mitambo ya nyuklia ya China. Taarifa zinasema kuwa,
Marekani ilichukua uamuzi wa kuvishambulia kwa makombora vinu na mitambo
ya nyuklia ya China wakati wa tawala za marais John F Kennedy na Lyndon
B. Johnson katika muongo wa sitini. Nyaraka hizo za siri zinaonyesha
kuwa, aliyekuwa Mkuu wa Kamisheni ya Nyuklia ya Marekani kuanzia mwaka
1961 hadi 1971 alithibitisha juu ya kutaka kufanyika shambulio hilo
dhidi ya mitambo ya nyuklia ya China. Mkuu huyo alieleza kwenye nyaraka
hizo kwamba uamuzi huo wa Marekani ulichukuliwa baada ya China kukataa
kujiunga kwenye makubaliano ya upigaji marufuku majaribio ya silaha za
nyuklia. Taarifa hizo zinaeleza kuwa, Umoja wa Kisovieti wa Urusi ya
zamani pia ulikubali kushirikiana na Marekani kwa ajili ya kuvishambulia
vinu vya nyuklia vya China. Hata hivyo, Marekani ilishindwa kutekeleza
azma yake hiyo kwa hofu kwamba China ingelitoa radiamali kali dhidi ya
Taiwan, inayohesabiwa kuwa mshirika mkubwa wa Marekani katika eneo la
Mashariki ya Mbali.
No comments:
Post a Comment