Rais Pierre Nkurunziza wa Burundi amesema kuwa, hatasalimu amri
kwa wale wanaofanya njama kutaka asigombee urais katika uchaguzi mkuu
ujao nchini humo.
Hayo yamesemwa na Willy Nyamitwe, mshauri wa Rais Nkurunziza
akimnukuu rais huyo ambapo pia amekosoa maandamano ya wapinzani
wanaopinga azma yake ya kushiriki katika uchaguzi ujao na kuitaja hatua
hiyo kuwa ni kinyume na demokrasia. Nyamitwe amesisitiza kuwa, Rais
Nkurunziza hatasalimu amri katika azma yake hiyo. Amewataja wale
wanaoandamana kupinga hatua hiyo kuwa, wanatishia usalama wa wananchi
katika uchaguzi ujao.
Mshauri huyo wa raia wa Burundi anasema chama tawala CNDD-FDD, kama
vilivyo vyama vingine vya siasa na katika fremu ya mwenendo wa
kidemokrasia, kina haki ya kumteua mgombea yeyote kimtakaye.
Kwa muda wa siku tatu sasa, maeneo kadhaa ya Burundi yamekuwa
yamekumbwa na machafuko makali ambayo yamesababishwa na hatua ya chama
tawala CNDD-FDD kumuidhinisha Rais Nkurunziza kupeperusha bendera ya
chama hicho katika uchaguzi ujao
Umoja wa Mataifa umeeleza wasiwasi wake juu ya kusahaulika
mgogoro wa Jamhuri ya Afrika ya Kati. Ripoti iliyotolewa na Shirika la
Kuhudumia Wakimbizi la Umoja wa Mataifa (UNHCR) imesema kuwa, idadi ya
wakimbizi laki tisa wa nchi hiyo ambalo ni tatizo mkubwa la kibinaadamu,
ni suala ambalo halitakiwi kusahaulika wala kupuuzwa na jamii ya
kimataifa. Ripoti hiyo imeeleza kuwa, zaidi ya raia laki nne na 60 elfu
wa Jamhuri ya Afrika ya Kati wamekimbilia nje ya nchi, huku wengine
wapatao laki nne na elfu 36 wakiwa wakimbizi wa ndani. UNHCR imesisitiza
kuwa, karibu watu milioni mbili na laki saba wanahitajia msaada wa
haraka kutokana na hali yao mbaya. Imeongeza kuwa, licha ya kiwango
hicho cha kutia wasiwasi lakini bado asasi husika zimeshindwa kudhamini
bajeti kwa ajili ya misaada ya waathirika hao wa mgogoro wa Jamhuri ya
Afrika ya kati.
Mgogoro wa Jamhuri ya Afrika ya Kati ulishadidi zaidi mnamo mwaka
2013, baada ya kuondolewa madarakani aliyekawa rais wa nchi hiyo,
Francois Bozize na waasi wa muungano wa Seleka. Mgogoro ulifuatiwa na
mauaji makubwa, ambayo wahanga wake wengi walikuwa Waislamu.