Wapinzani nchini Burundi wamepuuza onyo la serikali la kupiga
marufuku maandamano na badala yake wameendelea kuandamana wakipinga
hatua ya Rais Pierre Nkurunziza ya kuogombea kwa muhula mwingine
wakisisitiza kuwa, hatua hiyo inakinzana na Katiba na mkataba wa Arusha.
Jana mamia ya wanawake waliandamana katika mji mkuu Bujumbura na
kukusanyika katika Wizara ya Mambo ya Ndani ya nchi hiyo. Taarifa zaidi
kutoka Burundi zinasema kuwa, mgogoro wa kisiasa unaoikabili nchi hiyo
umezorotesha shughuli za kiuchumi. Jumuiya mbalimbali ukiwemo Umoja wa
Afrika na Jumuiya ya Afrika Mashariki zimeendelea kutoa wito wa
kudumishwa amani na utulivu nchini humo.
Takribani watu 15 wamepoteza maisha katika ghasia na maandamano
nchini Burundi. Wapinzani wanasema Nkurunziza anakiuka mapatano ya
Arusha yaliyomaliza vita vya ndani nchini humo, lakini wafuasi wa rais
huyo wanasema katika muhula wake wa kwanza Nkurunziza alichaguliwa na
Bunge na hivyo muhula huo hauwezi kuhesabiwa.
No comments:
Post a Comment