Umoja wa Afrika (AU) umeonya leo
kuwa hali ya Burundi si mwafaka kwa ajili ya kufanyika uchaguzi na
kusema kuwa haitoweza kutuma waangalizi wake nchini humo baada ya
malalamiko ya machafuko yaliyosababisha vifo, yaliyochochewa na hatua ya
Rais wa nchi hiyo Pierre Nkurunziza kuamua kugombea urais kwa kipindi
kingine cha tatu. Mkuu wa Kamisheni ya AU Bi Nkosazana Dlamini Zuma
amesema mazingira yaliyopo si mwafaka kwa ajili ya uchaguzi na kuongeza
kama ninavyomnukuu:”Huwezi kwenda kwenye nchi ambayo unakutana na
wakimbizi wanaoondoka, kisha useme, ‘tunakwenda kufanya uangalizi wa
uchaguzi’”. Mkuu wa Kamisheni ya Umoja wa Afrika amebainisha kuwa
kutokana na mambo yalivyo haoni hata kama uchaguzi utaweza kufanyika
katika mazingira hayo. Kuhusiana na uamuzi wa Mahakama ya Katiba ya
Burundi wa kumuidhinisha Rais Nkurunziza kugombea urais kwa muhula wa
tatu, Bi Nkosazana Dlamini Zuma amesema, ukiondoa mahakama hiyo, tafsiri
nyengine zote wanazopatiwa kuhusiana na katiba ya nchi hiyo zinaonyesha
kuwa Rais Nkurunziza hafai kugombea kwa kipindi cha tatu. Wakati huohuo
watu wasiopungua wanne wameuawa katika wimbi jipya la machafuko
yaliyosababishwa na upinzani dhidi ya hatua ya Rais Pierre Nkurunziza ya
kugombea urais kwa kipindi kingine cha tatu. Kwa mujibu wa Shirika la
Msalaba Mwekundu maiti tatu zimeonekana leo kwenye barabara za mji mkuu
Bujumbura. Mtu mwengine ameuawa kwa guruneti katika mapigano kati ya
polisi, waandamanaji na wanamgambo wanaoiunga mkono serikali wajulikanao
kama Imbonerakure. Katika tukio jengine lililotokea kwenye wilaya ya
Nyakabiga jijini Bujumbura leo, waandamanaji wanaopinga Rais Nkurunziza
kugombea tena urais wamemuua kwa kumvisha matairi ya moto shingoni mtu
mmoja, wakisema ni mwanachama wa tawi la vijana la chama tawala ambaye
aliwahi kuwashambulia wakati walipokuwa wakiandamana…/
No comments:
Post a Comment