Sunday, 24 May 2015
Daesh waua raia 400 katika mji wa Palmyra, Syria
Kundi la kigaidi na kitakfiri la Daesh limewaua kwa halaiki raia
400 wa Syria, wengi wao wakiwa ni wanawake na watoto katika shambulio
dhidi ya mji wa kale na wa kihistoria wa nchi hiyo wa Palmyra.
Televisheni ya Syria imeripoti jinai hiyo iliyofanywa na magaidi hao
wanaoungwa mkono na madola ya kigeni ikiwanukuu wakaazi wa mji huo wa
kihistoria wenye magofu ya kale yaliyohifadhiwa vizuri ya tokea enzi za
utawala wa Rumi yakiwemo mahekalu. Mauaji hayo ya halaiki yamefanywa na
magaidi wa kundi la Daesh baada ya kuwatuhumu wakaazi wa mji wa Palmyra
kuwa wanashirikiana na serikali na kukataa kutii amri za magaidi hao.
Wakati huohuo wanaharakati wa upinzani wameeleza kupitia mitandao ya
kijamii kuwa mamia ya miili ilikuwa imetapakaa barabarani katika mji huo
baada ya kushikiliwa na kundi la kitakfiri la Daesh siku ya Jumatano
iliyopita. Katika upande mwengine Mkurugenzi wa Mambo ya Kale wa
serikali ya Syria Mamoun Abdulkarim amesema athari nyingi za kihistoria
zilizokuwemo kwenye makumbusho ya mji wa Palmyra zimeondolewa, lakini
imeshindikana kuzihamisha baadhi ya nyengine zenye uzito wa tani tatu
hadi nne. Itakumbukwa kuwa kundi la kigaidi na kitakfiri la Daesh ni
maarufu kwa ubomoaji wa maeneo ya turathi za kihistoria kwa madai kwamba
athari hizo ni nembo na alama za shirk
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment