Jameel Syed, Muislamu wa jimbo la Michigan nchini Marekani
amekamilisha safari yake ya siku 35 ya kuzunguka na kusoma adhana katika
majimbo yote 50 ya nchi hiyo. Syed ambaye kitaalmu ni afisa masoko na
mwadhini katika msikiti ulioko kwenye kiunga cha Rochester katika jimbo
la Michigan, alikamilisha ziara yake hiyo ya kidini siku ya Ijumaa kwa
kuadhini katika msikiti huo. Jameel Syed, mwenye umri wa miaka 40
anasemekana kuwa ni mtu wa kwanza kusoma adhana katika majimbo yote 50
ya Marekani. Akizungumzia safari yake hiyo Syed amesema, ilikuwa ni
safari kubwa na ya kustaajabisha ambayo ilimkutanisha na Waislamu wa
rangi na asili tofauti, pamoja na wasiokuwa Waislamu katika vituo vya
taksi, viwanja vya ndege na misikiti. Miongoni mwa maeneo alikosoma
adhana Muislamu huyo ni katika ufukwe wa Hawai ambako alikutana na
kuzungumza pia na wasiokuwa Waislamu. Jameel Syed alifanya ziara pia
katika msikiti wa Chapel Hill huko Carolina Kaskazini walikokuwa
wakisali wanachuo watatu Waislamu waliouliwa kwa kupigwa risasi na
Mzungu mmoja mapema mwaka huu. Itakumbukwa kuwa mnamo tarehe 10
Februari, Craig Hicks aliwaua kwa kuwapiga risasi Deah Shaddy Barakat
aliyekuwa na umri wa miaka 23, mke wake Yusor Mohammad Abu-Salha, miaka
21 pamoja na dada yake Razan Mohammad Abu-Salha aliyekuwa na umri wa
miaka 19 karibu na Chuo Kikuu cha Carolina Kaskazini. Japokuwa polisi
ilitangaza kuwa mauaji ya wanachuo hao Waislamu yalitokana na mzozo juu
ya eneo la kuegesha magari, lakini wazazi wa marehemu hao wamesema
watoto hao waliuliwa kwa sababu ya chuki za kidini. Jameel Syed
alikutana na familia za vijana hao wa Kiislamu na kuwapa mkono wa pole
kwa msiba huo uliowafika
No comments:
Post a Comment