Maelfu ya raia wa Nigeria
waliokimbia mashambulizi ya kundi la kigaidi na kitakfiri la Boko Haram,
wamefukuzwa nchini Niger. Taarifa iliyotolewa leo na kiongozi mmoja wa
Niger, imesema kuwa, zaidi ya watu elfu tatu miongoni mwa wavuvi na
wakimbizi raia wa Nigeria ambao walikimbia nchi yao kutokana na
mashambulio ya kundi hilo, tayari wameondoshwa nchini humo. Kwa upande
wao raia hao wa Nigeria, wamenukuliwa wakisema kuwa, wamelazimika
kurejea nchini mwao na kwamba mamia ya wakimbizi wengine wa nchi hiyo
nao wanajiandaa kurudi makwao. Wameongeza kuwa, watu watatu kati yao
walipoteza maisha kutokana na kutembea kwa muda mrefu usiopungua siku
tatu katika safari hiyo ya kurejea kwao. Kufuatia taarifa hiyo, serikali
ya Nigeria, imeahidi kupeleka malori kwa ajili ya kuwabebea wakimbizi
hazo. Charles Otegbabe, mmoja wa maafisa wa serikali ya Nigeria
amethibitisha habari hiyo na kusema kuwa, serikali imewapokea wakazi wa
mji wa Gaidam, uliopo katika jimbo la Borno ambao awali walikimbilia
nchini Niger ili kuokoa maisha yao kipindi kundi la Boko Haram
liliposhadidisha jinai zake nchini humo. Kwa mujibu wa serikali ya
Niger, Jumatatu iliyopita, jeshi la nchi hiyo lilitekeleza operesheni
katika eneo la ziwa Chad nchini humo na kuchukua hatua ya kuwahamisha
raia kutoka sehemu moja kwenda nyengine . Hii ni katika hali ambayo
Niger, imewapa hifadhi raia wapatao laki moja wa Nigeria waliokimbilia
nchini humo kuokoa maisha yao kutokana na mashambulizi ya kundi la Boko
Haram.
No comments:
Post a Comment