Unordered List


Blogger Tips and TricksLatest Tips And TricksBlogger Tricks

Sunday, 24 May 2015

UN yalaani mauaji wa kiongozi wa upinzani Burundi

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-moon amelaani mauaji ya kiongozi wa upinzani nchini Burundi. Zedi Feruzi, kiongozi wa chama cha Umoja kwa ajili ya Amani na Maendeleo ya Burundi (UPD-Zigamibanga) aliuliwa kwa kupigwa risasi na watu wasiojulikana jana usiku wakati alipokuwa akielekea nyumbani kwake katika wilaya ya Ngagara iliyoko katika mji mkuu wa nchi hiyo Bujumbura. Taarifa iliyotolewa na Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa kupitia msemaji wake imeeleza kuwa jinai hiyo na ya shambulio la guruneti la siku ya Ijumaa katika soko kuu la jiji la Bujumbura lililoua watu wawili na kujeruhi wengine wengi yanatishia kuleta hali ya kutoaminiana na kuchochea machafuko nchini humo. Ban Ki-moon amewahimiza wadau mbalimbali nchini Burundi kufuatilia mazungumzo ya kisiasa yaliyoandaliwa na Umoja wa Mataifa na kuhusisha wawakilishi wa serikali, vyama vya upinzani na jumuiya za kidini.
Wakati huohuo wanaharakati wa upinzani nchini Burundi wamesimamisha mazungumzo na serikali kufuatia mauaji ya kiongozi wa chama cha upinzani cha UPD-Zigamibanga. Katika taarifa yao waliyoitoa mapema leo, wanaharakati hao wamelaani mauaji hayo waliyoeleza kuwa ni "kitendo kibaya sana" na kusema, wanasimamisha mpango wa kufanya mazungumzo na serikali. Aidha wamesema mauaji ya Zedi Feruzi yanaweza yakawa sehemu ya mpango wa kuwaondoa viongozi wanaoendesha kampeni dhidi ya Rais Pierre Nkurunziza wa nchi hiyo. Watu wapato 30 wameshauawa hadi sasa nchini Burundi katika matukio mbalimbali yakiwemo ya mashambulio na mapigano kati ya polisi na waandamanaji wanaopinga uamuzi wa Nkurunziza wa kugombea urais kwa muhula wa tatu

No comments:

Post a Comment