Serikali ya Kenya, imetangaza kuwa
mwanachama mmoja wa kundi la kigaidi la ash-Shabab nchini Somalia
amejisalimisha kwa jeshi la polisi huko mkoani Garissa, kaskazini
mashariki mwa nchi hiyo. Kwa mujibu wa duru za usalama nchini humo,
mwanachama huyo wa kundi hilo ambalo limekuwa likitekeleza jinai katika
siku za hivi karibuni, amejisalimisha kwa polisi ya Kenya baada ya
kujiengua kutoka kundi hilo. Kwa mujibu wa taarifa hiyo, gaidi huyo wa
ash-Shabab ambaye bado hajatajwa jina lake, amechukua uamzi huo
kulalamikia jinai ambazo zimekuwa zikitekelezwa na wanachama wa kundi
hilo dhidi ya watu wasio na hatia katika maeneo tofauti ya ndani na nje
ya Somalia. Inaelezwa kuwa kijana huyo mwenye umri wa miaka 22, ambaye
hajatajwa kwa sababu za kiusalama, alijiunga na kundi hilo hapo mwaka
2011. Amesema kuwa, amejisalimisha kwa jeshi la serikali kupitia fremu
ya msamaha uliotangazwa na serikali ya Nairobi kwa wanachama wa kundi
hilo. Kwengineko viongozi wa serikali ya Nairobi wametangaza kuwa,
makumi ya vijana waliokuwa wamejiunga na kundi hilo la kigaidi,
wamerejea makwao kufuatia operesheni za askari wa kusimamia amani wa
Umoja wa Afrika nchini Somalia AMISOM. Mwanzoni mwa mwaka huu, serikali
ya Kenya ilitangaza msamaha kwa wote kwa ajili ya vijana waliojiunga na
kundi la kigaidi la ash-Shabab.
No comments:
Post a Comment