Unordered List


Blogger Tips and TricksLatest Tips And TricksBlogger Tricks

Monday, 25 May 2015

TUMECHAGULIWA UTUMWA KUWA HATMA YETU

1 Nazungumzia Zanzibar. Tulitawaliwa na Wareno, wazee wetu hawakukubali walipambana na kuomba msaada kumtowa adui yule katika miaka ya nyuma, mreno aliondoka lakini utumwa ulibaki, tulifanya Mapinduzi ya 1964 kuondowa ubaguzi na leo miaka hamsini tunazungumzia utumwa na ukoloni mpya katika zama na mfumo mpya.Unaweza ukajiuliza hasa Zanzibar ina tatizo gani kiasi hiki?. Wakati mwengine hufikiri labda tuna majaaliwa mabaya mwisho hujisuta kwani ni wote au ni baadhi ya watawala wetu au ni sisi wananchi wa kawaida? wakati mwengine hujipa matumaini zama za kizazi cha kale kiliathiriwa na historia na hiki kipya kitaacha maradhi hayo. Kumbe sivyo,imekuwa ni maambukizo , inawezekana kuna GENETICS za miradhi zinatutesa na haziwezi kumea na kuishi katika KUJIAMULIA na kuwa huru. Zimeshaathiriwa na kuathirika kuishi katika utumwa. Yaelekea Watawala Zanzibar bila utumwa hawafurahi, hawatabasamu, hawajiamini. Maisha yao yamekulia katika utumwa, kuamuliwa na kuchaguliwa mambo yao.Utumwa wa Zanzibar hasa huu unaoendelea zama hizi una siri moja kubwa.Siyo ile ya kuwagawa watu tu, kunufaisha wachache tu, kurudisha nyuma mshikamano wa watu wa visiwa hivi tu, kuleta umasikini na kuvifanya visiwa kujisalimisha kwa mkoloni au kutegemea majaliwa ya mkoloni lakini ni ile siri ya KUPEWA PIPI ISIYOISHA SUKARI. Tunaaminishwa pipi hii itadumu wakati tunajuwa fika huyo mtengeneza pipi naye hawezi kudumu seuze pipi yenyewe. Ni dhahiri mkoloni wetu wa leo kadekezwa kwa miongo kama mitano tokea KUINGIA RASMI HAPA KWETU na WATAWALA WALAFI WASIOSIKILIZA MATAKWA YA WANANCHI.
WAMEAMINISHWA KUWA ADUI YAO NI KILA MTETEA ZANZIBAR.Kwao wao huyu ni hatari zaidi kuliko mkoloni, wameshatengenezwa kukubali utumwa. Mpaka lini haya? Aje nani tena atwambie umuhimu wa kuwa na nchi yetu huru na maamuzi ili watawala watanabahi? nani aje? kama ni viongozi wazalendo wote walikwenda na maji, kama ni wanavindaki ndaki wameshikishwa adabu, kama ni wapinzani wameshakubuhu hakuna jipya. Kimebaki nini tena? si tulibadilisha Katiba na kutamka sasa Zanzibar ni nchi imekuwaje? wachumia tumbo walijivisha gunia la usaliti na kujifunga vibwebwe viunoni na kukata viuno kule DODOMA. Walisherehekea UTUMWA wa milele kwa pipi ya Sukari zamani ikiitwa FAGI.Ili Zanzibar ibaki kuwa koloni. Sherehe ile ilikuwa na maana moja kubwa. KUKUBALI KUWA WATUMWA WA MILELE. Haingii akilini Kwamba ni juzi tu Mwanakindaki ndaki kipenzi chetu kutumia wadhifa wake na kujitowa muhanga kuirejesha Zanzibar katika nafasi yake eti leo amekuwa ADUI wa Wachumia tumbo. Hawa walikuwa nae bega kwa bega na walijivisha kilemba cha ukoka kuwa wako pamoja nae ili Zanzibar irudi kwenye heshima. Wapi leo. Genetics zimewazidi nguvu wamerudi katika uhalisia wao.
Bahati mbaya sana MILAFI imetuzuwiya kutumia fursa ya kihistoria pale ambapo mkoloni wetu mara hii alifurahi na kucheka na kusema hebu semeni mnataka nini badala ya kusema tunataka uhuru basi mitawala yetu ilisema tunataka KUTAWALIWA na KUWA WATUMWA WA MILELE.Ilitumia hilba yao kama kawaida kuziba sauti za Wazanzibari na kujifanya wasemaji wetu. Mbona kama ni wema hawatuulizi kupitia maoni huru tunataka nini. Wapi? fursa haiji mara mbili. Nasikitika na wale wanaoishabikia MITAWALA HII. Hawa kama ingekuwa ni katika uhalifu na wao wangekuwa wasaidia uhalifu.Wanapaswa kuadhibiwa kama walivyo wahalifu wengine lakini tuseme bado wakati wao ingawa hauko mbali.
Wamesahau awamu zote zikipiga kelele na safari iliishia njiani, awamu ya sita ilitenda na kuthubutu kuweka mazingira yote ya kurejea kwa Zanzibar. Hatimae nafasi ya mtende ikaja. Damu ya wasaliti ikachemka wakasahau kilio chao cha kama miezi mitano walipotowa machozi YA MAMBA YA KUITETEA Zanzibar katika Tume ya KATIBA. Hawachoki na wala hawashibi. Usaliti una lana kama ulivyo ulevi. Toka lini mtu kuvimbiwa pipi kama si uroho tu. Zanzibar imepotezwa kwa mikono ya wasaliti hawa na sasa miaka hamsini wanataka TUWAAMINI tena kwa lipi jipya? au mafuta ya mgando kungarisha kiatu?
Hatutawasamehe daima mpaka mtubu.Mnatuchagulia utumwa badala ya uhuru halafu mnataka tuwaunge mkono. Kamwe hatutafanya hivyo. Nyinyi endeleeni na shari zenu na hilba kama kawaida. Ni bora mshinde kwa HADAA MKIWA PEKEYENU MTAUSEMA UKWELI MCHUNGU JAPO VYOONI KWAMBA Wazanzibari WAMETUKATAA TENA. ENDELEENI TU.
Baya zaidi sasa mnazidi na mnakaribia laana ya wazi. Hili la kuwaadhibu na kuwafungulia kesi za kizushi mashehe si jema kwa mustkabali wa nchi. Mmeshavuka mipaka sasa subirini gharika itakayosababishwa na mikono yenu. Msije mkatafuta wachawi. Mnajuwa mipango ilisukwa na nani na kila mmoja atawajibika kivyake wakati ukifika.Wote safari yetu ni moja.Lakini hili la kuwaadhibu masheikh nawasihi mnakwenda KOMBO ZAIDI.Yaani mnajikubalisha utumwa mpaka kuwauza raia wenu ili nyinyi muishi na kuwapendezesha wakoloni kiasi cha kukosa utu. Hebu fikirini wale watoto wa masheikh wamekosa mangapi kwa maamuzi yenu yasiyo na uzalendo? Mmeekubali utumwa mpaka kwa mambo yasiyostahiki.
Hizi sio zama za kawaida. Nawasihi Wazanzibari kwa umoja wetu tujali UZALENDO. Kumeletwa misingi ya kidemokrasia katika kuonesha hisia na kuleta mabadiliko ya kiutawala KATIKA NCHI. MARA HII NI ZADI YA SIASA ZA VYAMA. Tusipoziba ufa tutajenga ukuta. Hata niandike vitabu mia sitomaliza kuonesha UCHOVU wa watawala wetu ingawa wenyewe wanakataa kuwa hivyo.
Mpaka lini tutaendelea kulalamika, kupumbazwa, kughilibiwa na kutumiwa kufanikisha mipango miovu dhidi ya MUSTAKABALI WA ZANZIBAR? Mpaka lini tutasemewa tusiyoyataka? aje nani afashamishe hili kuwa Zanzibar imepotezwa na Watawala wetu kwa miaka zaidi ya hamsini sasa? Inasikitisha kuona watawala wakati mwengine wanalia na kulalamika eti tusimame kwa MIGUU YETU sasa? hawa si ndio waliopiga kelele za furaha na kukata mauno kule Dodoma? mna mlilia nani?
MATUMAINI YA MABADILIKO KWA KUTUMIA MAARIFA YOTE YANAPASWA KUELEKEZWA KUWAZIBA SAUTI WASALITI KATIKA MAAMUZI YA KURA.
TUKATAE KUCHAGULIWA UTUMWA, TUWAKATAE WOTE WANAOTUTIA UTUMWANI.
MUNGU IBARIKI ZANZIBAR

Uwamsho waibua Mapya

farid Dar es Salaam. Sheikh Farid Hadi Ahmed (43) anayekabiliwa na kesi ya ugaidi na wenzake 23, wa Jumuiya ya Uamsho, wamesema wanahitaji Jaji Mkuu, Mwanasheria Mkuu wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, Mwanasheria Mkuu wa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Waziri wa Katiba wa Zanzibar, waende gerezani kuonana nao.
“Tunaomba iwe ndani ya siku saba, zikiisha uamuzi tutakaoutoa tusije kulaumiana, hatuwezi kudhulumiwa haki yetu tukakaa kimya,” alidai Sheikh Farid jana muda mfupi baada ya Wakili wa Serikali, Janeth Kitali kudai mbele ya Hakimu Mkazi, Renatus Rutta kuwa kesi yao ilikuja kwa ajili ya kutajwa.
Kitali alidai kuwa upelelezi bado haujakamilika na pia bado wanasubiri kumbukumbu za Mahakama Kuu ili waweze kupeleka rufaa yao katika Mahakama ya Rufani.
Baada ya kutolewa kwa maelezo hayo, Sheikh Farid alidai kuwa kesi ya ugaidi inayowakabili ni ya bandia na madai yao yalikuwa ni kuhakikisha Zanzibar inapata mamlaka yake sahihi na Muungano hawautaki na kwamba, madai hayo ndiyo yaliyosababisha wao kupata misukosuko na kujikuta wakibambikiwa kesi ya ugaidi.
IMG_0030
Alidai kuwa katika kesi hiyo, wapo washtakiwa ambao wamegoma kula na wanne kati yao wana hali mbaya kiasi cha kuwekwa katika eneo maalumu. Aliiomba mahakama ikawaangalie au isubiri kupokea maiti ili iingie kwenye Historia ya Zanzibar.
Hakimu Rutta alipokea taarifa hiyo, alimhoji askari magereza kama kweli mahabusu hao wamegoma kula, naye alikiri na kudai kuwa wamegoma hata kufika mahakamani.
Lakini mshtakiwa Salum Ally alikanusha kauli hiyo ya askari magereza na kudai kuwa hawakugoma kufika mahakamani bali walishindwa kwa sababu ya kukosa nguvu.
Baada ya kutolewa kwa maelezo hayo, Hakimu Rutta alisema ni haki ya watu waliopo gerezani kutembelewa na wanapaswa kutendewa kwa kadiri inavyopaswa.
Alimweleza Sheikh Farida na wenzake wakawaeleze wenzao kuwa wanapaswa kufika mahakamani na madai yao yatafanyiwa kazi.
Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP) aliwasilisha kusudio la kukata rufaa dhidi ya uamuzi wa Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam, uliotolewa na Jaji Fauz Twaib ulioamuru Mahakama ya Kisutu kusikiliza na kutolea uamuzi hoja zilizowasilishwa.
mahakamani hapo na upande wa utetezi.

Upande wa utetezi katika hoja zao, walikuwa wakiiomba mahakama ya Kisutu ifute mashtaka ya ugaidi dhidi yao, pia walihoji uhalali wa kushtakiwa Tanzania Bara wakati Zanzibar ni nchi ambayo ina Mahakama Kuu na kuomba wakashtakiwe katika sehemu walizokamatwa.
Katika kesi hiyo, Sheikh Farid Hadi Ahmed ambaye pia ni kiongozi wa jumuiya hizo na wenzake wanakabiliwa na makosa manne ya ugaidi.
Mwananchi

fivetanzanite

Sunday, 24 May 2015

Vikosi vya Iraq vyasonga mbele kuelekea al Ramadi

Vikosi vya jeshi la Iraq vikishirikiana na vikosi vya kujitolea vya wananchi vinasonga mbele kuelekea mji wa Al Ramadi, wiki moja baada ya mji huo kushikiliwa na wanamgambo wa kundi la kigaidi na kitakfiri la Daesh. Afisa mmoja wa Polisi na mpiganaji wa makabila ya Kisuni wamesema, kwa msaada wa wanamgambo wa Kishia, vikosi vyao vimeukomboa mji wa Husaiba al-Sharqiya ulioko umbali wa kilomita 10 mashariki mwa Al Ramadi kutoka mikononi mwa magadi wa Daesh. Amir al-Fahdawi, kamanda wa vikosi vya makabila ya Iraq amesema, leo wameukomboa mji wa Husaiba al-Sharqiya, huku wakiandaa mikakati ya kuwarejesha nyuma zaidi wapiganaji wa kundi la kigaidi la Daesh. Kwa mujibu wa kamanda huyo, ndege za kivita za jeshi la Iraq zinaendelea kuzishambulia kwa makombora ngome za kundi la kigaidi la Daesh zilizoko kwenye ufukwe wa Mto Euphrates. Kushikiliwa mji wa Al Ramadi na kundi la kigaidi la Daesh kumetilia shaka athari za mashambulio ya anga dhidi ya ngome za kundi hilo yanayofanywa na muungano wa madola ya kigeni yanayoongozwa na Marekani. Wakati huo huo Muwaffaq al Rabei, mjumbe wa Kamisheni ya Usalama na Ulinzi katika bunge la Iraq amesisitiza kuwa mapambano dhidi ya kundi la kigaidi na kitakfiri la Daesh yataendelea. Al Rabei amesema mji mkuu wa Iraq, Baghdad uko salama na kwamba kundi la kigaidi la Daesh halina uwezo wa kutia mguu katika mji huo

Daesh waua raia 400 katika mji wa Palmyra, Syria

Kundi la kigaidi na kitakfiri la Daesh limewaua kwa halaiki raia 400 wa Syria, wengi wao wakiwa ni wanawake na watoto katika shambulio dhidi ya mji wa kale na wa kihistoria wa nchi hiyo wa Palmyra. Televisheni ya Syria imeripoti jinai hiyo iliyofanywa na magaidi hao wanaoungwa mkono na madola ya kigeni ikiwanukuu wakaazi wa mji huo wa kihistoria wenye magofu ya kale yaliyohifadhiwa vizuri ya tokea enzi za utawala wa Rumi yakiwemo mahekalu. Mauaji hayo ya halaiki yamefanywa na magaidi wa kundi la Daesh baada ya kuwatuhumu wakaazi wa mji wa Palmyra kuwa wanashirikiana na serikali na kukataa kutii amri za magaidi hao. Wakati huohuo wanaharakati wa upinzani wameeleza kupitia mitandao ya kijamii kuwa mamia ya miili ilikuwa imetapakaa barabarani katika mji huo baada ya kushikiliwa na kundi la kitakfiri la Daesh siku ya Jumatano iliyopita. Katika upande mwengine Mkurugenzi wa Mambo ya Kale wa serikali ya Syria Mamoun Abdulkarim amesema athari nyingi za kihistoria zilizokuwemo kwenye makumbusho ya mji wa Palmyra zimeondolewa, lakini imeshindikana kuzihamisha baadhi ya nyengine zenye uzito wa tani tatu hadi nne. Itakumbukwa kuwa kundi la kigaidi na kitakfiri la Daesh ni maarufu kwa ubomoaji wa maeneo ya turathi za kihistoria kwa madai kwamba athari hizo ni nembo na alama za shirk

Saudia yalazimika kutangaza hali ya hatari mpakani

Saudi Arabia leo imelazimika kutangaza hali ya hatari katika ukanda wa mpaka wake wa kusini na Yemen baada ya kuongezeka mashambulizi ya makombora ya wanamapambano wa Yemen dhidi ya Saudia.
Televisheni ya al Masirah imetangaza kuwa, jeshi la Yemen na wapiganaji wa kamati za wananchi wa nchi hiyo wameendelea kushambulia maeneo ya Saudia yanayopakana na mkoa wa Saada, kama ambavyo wameshambulia kwa makombora pia jengo la walinzi wa mpakani wa Saudia katika eneo la at Twiwaal huko Jizan.
Wakati huo huo wakazi wa mkoa wa al Jawf wa kaskazini mwa Yemen wameandamana kulalamikia uongo unaoenezwa na televisheni za al Jazeera na al Arabiya. Televisheni ya al Masirah imeripoti kuwa, wananchi wa Yemen leo wameandamana katika maeneo mbalimbali ya mkoa wa mpakani wa al Jawf kaskazini mwa Yemen wakikanusha na kulalamikia uongo unaonezwa na televisheni hizo za Qatar na Saudia kwamba eti wakazi wa mkoa huo wako tayari kupambana na Ansarullah. Waandamanaji wamesema kuwa, uongo kama huo hautatia doa mshikamano wa wananchi wote wa Yemen katika kukabiliana na jinai wanazofanyiwa na Saudia na waitifaki wake

Waislamu waandamana Saudia kulaani jinai za Daesh

Hali ya wasiwasi imezidi kutanda katika mkoa wa mashariki mwa Saudi Arabia siku mbili baada ya kutokea shambulio la bomu katika Msikiti wa Imam Ali AS huko al Qadeeh.
Leo wakazi wa mji wa al Qadeeh wamefanya maandamano makubwa wakilalamikia serikali ya Saudia kwa kushindwa kuwalinda.
Waandamanaji wamewaambia waandishi wa habari kuwa vikosi vya usalama vya Saudi Arabia vimewatelekeza wakazi wa mji huo na kutoa mwanya wa makundi ya kigaidi kama Daesh kufanya mashambulizi hadi misikitini.
Wakati huo huo Wizara ya Mambo ya Ndani ya Saudia imesema kuwa, aliyefanya shambulio la kigaidi la siku ya Ijumaa katika Msikiti wa Imam Ali AS huko al Qadeeh ni raia wa Saudia anayejulikana kwa jina la Salih bin Abdulrahman Salih al Ghisaami.
Wizara hiyo imeongeza kuwa, gaidi huyo alikuwa anasakwa na maafisa usalama wa Saudia kwa kuwa na mfungamano na kundi la kitakfiri la Daesh ambalo hadi sasa limeshaua maelfu ya watu katika maeneo mbalimbali ya ulimwengu wa Kiarabu.

Rais Rouhani: Hatutoruhusu 5+1 lidhibiti utajiri wetu

Rais Hassan Rouhani wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema kuwa, inabidi mji wa Khorramshahr (wa kusini magharibi mwa Iran) wenye utajiri wa mafuta ukombolewe kutoka katika mashinikizo ya kundi la 5+1 na Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa.
Rais Rouhani amesema hayo leo katika maadhimisho ya siku ya ukombozi wa mji wa Khorramshahr na kuongeza kuwa, ardhi ya kiuchumi ya Iran imetekwa na Baraza la Usalama na kundi la 5+1 na kusisitiza kuwa, kama ambavyo makamanda wa kijeshi wa Iran walifanikiwa kuukomboa mji wa Khorramshahr kutoka mikononi mwa wanajeshi vamizi wa Iraq, viongozi wa kisiasa nao wataikomboa Khorramshahr mpya kutoka kwenye mashinikizo ya madola ya kigeni.
Amesema, Iran ni taifa ambalo haliwezi kamwe kuusahau ukombozi wa Khorramshahr na kwamba litapambana vilivyo na mashinikizo yote ya kiuchumi, kibiashara na kielimu hadi litakajikomboa kikamilifu kwa miongozo ya busara ya Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu na kwa taufiki na uwezo wa Mwenyezi Mungu Mtukufu.

UN yalaani mauaji wa kiongozi wa upinzani Burundi

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-moon amelaani mauaji ya kiongozi wa upinzani nchini Burundi. Zedi Feruzi, kiongozi wa chama cha Umoja kwa ajili ya Amani na Maendeleo ya Burundi (UPD-Zigamibanga) aliuliwa kwa kupigwa risasi na watu wasiojulikana jana usiku wakati alipokuwa akielekea nyumbani kwake katika wilaya ya Ngagara iliyoko katika mji mkuu wa nchi hiyo Bujumbura. Taarifa iliyotolewa na Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa kupitia msemaji wake imeeleza kuwa jinai hiyo na ya shambulio la guruneti la siku ya Ijumaa katika soko kuu la jiji la Bujumbura lililoua watu wawili na kujeruhi wengine wengi yanatishia kuleta hali ya kutoaminiana na kuchochea machafuko nchini humo. Ban Ki-moon amewahimiza wadau mbalimbali nchini Burundi kufuatilia mazungumzo ya kisiasa yaliyoandaliwa na Umoja wa Mataifa na kuhusisha wawakilishi wa serikali, vyama vya upinzani na jumuiya za kidini.
Wakati huohuo wanaharakati wa upinzani nchini Burundi wamesimamisha mazungumzo na serikali kufuatia mauaji ya kiongozi wa chama cha upinzani cha UPD-Zigamibanga. Katika taarifa yao waliyoitoa mapema leo, wanaharakati hao wamelaani mauaji hayo waliyoeleza kuwa ni "kitendo kibaya sana" na kusema, wanasimamisha mpango wa kufanya mazungumzo na serikali. Aidha wamesema mauaji ya Zedi Feruzi yanaweza yakawa sehemu ya mpango wa kuwaondoa viongozi wanaoendesha kampeni dhidi ya Rais Pierre Nkurunziza wa nchi hiyo. Watu wapato 30 wameshauawa hadi sasa nchini Burundi katika matukio mbalimbali yakiwemo ya mashambulio na mapigano kati ya polisi na waandamanaji wanaopinga uamuzi wa Nkurunziza wa kugombea urais kwa muhula wa tatu

Friday, 15 May 2015

Mapinduzi ya kijeshi nchini Burundi

Baada ya masiku kadhaa ya machafuko ya umwagaji damu yaliyojiri katika mji mkuu wa Burundi, Bujumbura, Meja-Jenerali Godefroid Niyombare, afisa wa ngazi ya juu wa jeshi ametangaza kupitia redio moja ya binafsi kuwa mapinduzi ya kijeshi yamefanyika nchini humo. Jenerali Niyombare amesisitiza kuwa Rais Pierre Nkurunziza ameondolewa madarakani na baraza lake la mawaziri limevunjwa. Wakati huohuo Mkuu wa majeshi ya Burundi Jenerali Prime Niyongabo ametoa tamko jengine kupitia redio ya serikali na kuwatangazia wananchi kwamba mapinduzi hayo ya kijeshi yamezimwa. Jenerali Niyongabo amewahakikishia wananchi kuwa wanajeshi watiifu kwa Rais Nkurunziza wameidhibiti Ikulu ya Rais pamoja na uwanja wa ndege wa kimataifa wa Bujumbura. Mbali na utata huo, kuna habari za kutatanisha pia kuhusu mahali aliko Rais Pierre Nkurunziza mwenyewe. Jana Jumatano, kiongozi huyo alikuwa ameelekea Dar es Salaam, Tanzania kuhudhuria kikao cha dharura cha viongozi wa nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC); na kwa mujibu wa ripoti za mwisho ni kwamba angaliko mjini Dar es Salaam. Nayo serikali ya Uganda imekanusha habari za kuwasili nchini humo Rais wa Burundi kupitia bandari ya Entebe. Kutokea mapinduzi ya kijeshi nchini Burundi lilikuwa jambo la kutarajia kutokana na hali ya mgogoro inayoshuhudiwa hivi sasa nchini humo. Japokuwa tangazo la jeshi la kutopendelea upande wowote kati ya pande hasimu kwenye mgogoro wa nchi hiyo na kimya kilichoonyeshwa na makamanda wa jeshi katika muda wote wa mwezi mmoja sasa vilipunguza uwezekano wa kutokea mapinduzi hayo. Kutokea mapinduzi ya kijeshi kulizidi kuonekana kuwa ni jambo lililo mbali kutokana na hitilafu za mitazamo pia zilizojitokeza kati ya maafisa wa polisi na makamanda wa ngazi za juu wa jeshi. Pamoja na hayo kuondoka nchini Rais Nkurunziza na kuelekea Tanzania kwa safari rasmi kulitoa fursa kwa majenerali wa jeshi ya kuchukua hatua dhidi yake.Meja-Jenerali Niyombare, ambaye mwezi Februari alivuliwa wadhifa wake wa Mkuu wa Idara ya Intelijinsia na Usalama wa nchi, alishirikiana na baadhi ya maafisa waandamizi wa jeshi na polisi na kufanya mapinduzi ya kijeshi. Msimamo wa jenerali huyo wa kupinga uamuzi wa Rais Nkurunziza wa kugombea urais kwa muhula wa tatu ndio uliomponza na kumfanya avuliwe wadhifa aliokuwa nao. Tunaweza kusema kuwa uamuzi wa Nkurunziza wa kutaka aendelee kuwa rais wa Burundi baada ya kuweko madarakani kwa kipindi cha miaka kumi umeigawa nchi hiyo katika kambi mbili za wapinzani na waungaji mkono wa uamuzi wake huo. Mgawanyiko na mpasuko huo ndani ya jamii ya Burundi ulianzia katika vyama na makundi ya kisiasa na kudhihirika zaidi hivi sasa kwa jaribio la mapinduzi ya kijeshi ambalo limewagawa pia makamanda wa jeshi na vikosi vya usalama vya nchi hiyo. Msimamo wa Rais Pierre Nkurunziza wa kutaka aendelee kuwania urais kwa muhula wa tatu ulipingwa na kukosolewa na Umoja wa Afrika, Umoja wa Ulaya pamoja na nchi nyingi za Kiafrika. Pamoja na hayo kutokana na kuungwa mkono na viongozi wa chama chake tawala cha CNDD-FDD na bila kujali maandamano ya kumpinga ya wafuasi wa vyama vya upinzani yaliyoutikisa mji mkuu Bujumbura, alishikilia msimamo wake huo wa kugombea tena urais. Hata vifo vya watu wasiopungua 23 waliouawa katika machafuko na maandamano ya upinzani havikuiteteresha azma ya Nkurunziza ya kuwania tena urais wa Burundi. Kwa mujibu wa baadhi ya duru, mazungumzo yanayofanyika kati ya makamanda wa jeshi yanazidi kuupa nguvu uwezekano wa kuzimwa mapinduzi ya kijeshi yaliyotokea jana nchini humo.
Alaa kulli hal ung’ang’anizi wa Nkurunziza wa kutaka aendelee kubaki madarakani umemtumbukiza kiongozi huyo kwenye kapu la viongozi wa kizazi kilichopita barani Afrika waliosibiwa na ugonjwa wa uchu wa madaraka, ambao hatimaye waling’olewa madarakani kwa nguvu kutokana na mashinikizo ya maandamano ya wananchi au mapinduzi ya kijeshi. Lisilo na shaka ni kuwa kutokana na hali inayoshuhudiwa hivi sasa nchini Burundi, ya kutibuka na kuvurugika hali ya usalama hakuna uwezekano uchaguzi wa tarehe 26 ya mwezi ujao wa Juni kufanyika kama ulivyopangwa. La kusubiri ni kuona radiamali gani itatolewa na viongozi wa Umoja wa Afrika na wa Jumuiya ya Afrika Mashariki kuhusiana na matukio yanayoendelea kujiri nchini Burundi…/

Rwasa: Burundi inakaribia tena vita vya ndani

Agathon Rwasa Agathon Rwasa
Kiongozi wa chama cha upinzani cha FNL nchini Burundi amesema nchi hiyo ya Afrika Mashariki inakaribia kutumbukia tena kwenye vita vya ndani na ameitaka jamii ya kimataifa kuingilia kati ili suala hilo lisitokee. Akizungumza kwenye mahojiano maalumu na idhaa hii mapema leo, Agathon Rwasa amesema jeshi la Burundi linaonekana kugawanyika baada ya tangazo lililotolewa hapo jana na Jenerali Godefroid Niyombare, kwamba ameipindua serikali ya Rais Pierre Nkurunziza. Bw. Rwasa amesema iwapo mapinduzi ya kijeshi yanayoendelea yatakosa kufanikiwa na Rais Nkurunziza akarudi madarakani na kudhibiti hali ya mambo, kiongozi huyo atahitajika kutumia fursa hiyo kufungua milango ya mazungumzo badala ya kutumia mkono wa chuma dhidi ya mahasimu wake. Kiongozi wa chama cha FNL pia amesema iwapo mapinduzi yatafanikiwa, wafanyamapinduzi watapaswa kujumuisha Warundi wote katika mchakato wa kurudisha utawala wa sheria haraka iwezekanavyo

Mauaji ya kutatanisha mashariki mwa DRC

Habari kutoka mji wa Beni, mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo zinasema kuwa watu wasiopungua 20 wameuawa katika mazingira ya kutatanisha katika kipindi cha siku tatu zilizopita. Mashuhuda wameiambia idhaa hii kwamba maiti za watu 20 zilizokatwa vipande vipande zimetapakaa katika vichaka na misitu ya karibu na mji wa Beni na kwamba serikali imesisitiza kuwa waasi wa kutoka Uganda wa ADF-Nalu ndio waliotekeleza mauaji hayo. Hii ni katika hali ambayo, jeshi la DRC miezi miwili iliyopita lilitangaza kuwa limeharibu ngome nyingi za waasi hao katika maeneo mengi hususan katika mikoa ya Kivu Kusini na Kaskazini inayopatikana mashariki mwa nchi hiyo.
Eneo la mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo limekuwa likikumbwa na mauaji yanayotokana na hujuma za makundi ya waasi; na wafuatiliaji wengi wa mgogoro wa nchi hiyo wanasema waasi hupiga kambi mashariki mwa DRC kutokana na eneo hilo kuwa na rasilimali nyingi kama vile madini yenye thaman

Saudia yavunja mapatano ya usitishaji vita Yemen

Watu wasiopungua tisa wameuawa na wengine wengi kujeruhiwa baada ya ndege za kivita za Saudia kudondosha mabomu licha ya utawala huo wa Riyadh kutangaza usitishaji wa hujuma yake ya kijeshi ya wiki saba dhidi ya nchi hiyo masikini.
Duru zinaarifu kuwa Wayemen kadhaa wameuawa leo baada ya ndege ya helikopta aina ya Apache kushambulia eneo la al-Safiya katika mkoa wa Sa'ada kaskazini mashariki mwa nchi hiyo. Hali kadhalika mapema leo ndege za kivita za Saudia zimedondosha mabomu katika bandari ya Aden na mikoa ya Hajjah na Abyan. Saudia imekiuka tangazo lake la usitishaji vita kwa muda wa siku tano kuanzia Jumanne. Wakati huo huo Iran imesema meli yake inayopelekea misaada ya kibinadamu Yemen imefanya hivyo kwa ushirikiano na Umoja wa Mataifa. Naibu Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran anayeshughulikia masuala ya Kiafrika na Kiarabu Hossein Amir-Abdollahian amesisitiza kuwa meli hiyo ya misaada ya Iran itafika Yemen kama ilivyopangwa. Hivi karibuni Kamanda mwandamizi wa jeshi la Jamhuri ya Kiislamu ya Iran alitahadharisha kuwa, shambulizi lolote dhidi ya meli ya misaada ya kibinadamu ya Iran inayoelekea Yemen litawasha moto wa vita katika eneo zima la Mashariki ya Kati. Jenerali Masoud Jazayeri, amesema meli hiyo iliyopewa jina la 'Nejat' yaani 'uokovu' imebeba misaada ya kibinadamu kama vile chakula na dawa na wala haipaswi kuzuiwa au kushambuliwa kwa mujibu wa sheria za kimataifa

Assad: Wasyria ni imara katika kupambana na ugaidi

Rais Assad akizungumza na ujumbe wa Iran mjini Damascus, Mei 13 2015 Rais Assad akizungumza na ujumbe wa Iran mjini Damascus, Mei 13 2015
Rais Bashar al-Assad wa Syria amesema magaidi hawatafanikiwa katika njama zao za kuvuruga azma ya Wasyria katika mapambano yao dhdi ya ugaidi.
Assad ameyasema hayo Jumatano mjini Damascus katika mkutano na Alaeddin Boroujerdi, Mkuu wa Kamati ya Usalama wa Taifa na Sera za Kigeni katika Bunge la Iran, Majlisi ya Ushauri ya Kiislamu.
Katika kikao hicho, Assad na Boroujerdi walijadili na kuashiria uungaji mkono wanaopata magaidi kutoka baadhi ya nchi za Magharibi na waitifaki wao katika eneo na kusema magaidi ni vibaraka wa nchi zinazowaunga mkono. Rais wa Syria amesema magaidi na waungaji mkono wao wamekuwa wakifanya hadaa na kueneza propaganda ili kufidia kipigo wanachopata katika medani ya vita. Amesema kwa irada yao imara na msaada wa nchi rafiki kama Iran, Wasyria wanaangamiza ugaidi na machafuko katika nchi yao. Kwa upande wake Boroujerdi amewapongeza Wasyria, jeshi na uongozi wa nchi hiyo kwa kusimama imara na kuongeza kuwa, wakiendelea hivyo hatimaye watapata ushindi kamili dhidi ya magaidi. Aidha amesema Iran itaendelea kuiunga mkono Syria hadi pale mgogoro utakapomalizika nchini humo. Wakati huo huo duru za habari zinasema wapiganaji wa Harakati ya Hizbullah ya Lebanon wamepata mafanikio makubwa katika mapamabano na magaidi katika milima ya Qalamoun kaskazini mwa Damascus

Jeb Bush aambiwa: 'Kaka yako aliunda ISIS'

Jeb Bush Jeb Bush
Mwanafunzi wa chuo kikuu nchini Marekani amemlaumu vikali mgombea tarajiwa wa kiti cha urais kwa tiketi ya chama cha Republican Jeb Bush na kumfahamisha bayana kuwa kundi la kigaidi la ISIS (Daesh) liliundwa na kaka yake, rais wa zamani wa Marekani George W. Bush.
Tukio hilo limejiri katika mkutano wa kampeni katika jimbo la Nevada siku ya Jumamosi baada ya Jeb Bush kumaliza mkutano huo. Jeb Bush aliwahi kuwa Gavana wa Florida na anatazamiwa kutangaza azma yake ya kuwania urais katika uchaguzi ujao wa rais mwaka 2016.
Ivy Ziedrich, mwanaharakati wa kisiasa, alimbana vikali Jeb kuhusu hatua ya George W Bush kuvamia Iraq na hatimaye kuunda kundi la kigaidi la ISIS. Mwanaharakati huyo amemfahamisha Jeb Bush kuwa kaka yake alivamia Iraq na kuwaachia kwa makusudi wanamgambo wapate silaha za kisasa.
Jeb Bush alipinga kauli hiyo, hata hivyo alisema kuna baadhi ya makosa yaliyofanywa na rais wa wakati huo wa Marekani katika kutuma majeshi nchini Iraq.

Curfew' yatangazwa kaskazini mwa Nigeria

Jeshi la Nigeria limetangaza amri ya kutotoka nje (curfew) katika mji wa Maiduguri kaskazini mashariki mwa nchi hiyo siku moja baada ya wapiganaji wa Boko Haram kuvamia mji huo. Msemaji wa jeshi la Nigeria, Kanali Tanko Gusau, amesema hatua hiyo imechukuliwa ili kuwalinda raia na mali zao. Wakaazi wa Maiduguri watatakiwa kubakia majumbani mwao kuanzia saa 12 jioni hadi 12 asubuhi kila siku hadi hali itakapoimarika.
Hapo jana Jumatano, wapiganaji wa kundi la kigaidi la Boko Haram walivamia mji wa Maiduguri lakini jaribio lao la kuteka kambi ya kijeshi katika mji huo lilifeli baada ya kuzidiwa nguvu na wanajeshi wa serikali. Habari zinasema wanajeshi 3 waliuawa kwenye mapigano ya hapo jana huku Boko Haram likipoteza makumi ya wapiganaji wake. Pia vijana 6 wa kujitolea wanaolinda mji wa Maiduguri maarufu kama sungusungu wamepoteza maisha kwenye patashika hiyo

Tuesday, 12 May 2015

Wanajeshi wanane wa Mali wauawa Timbuktu

Wanajeshi wasiopungua wanane wa Mali wameuawa na wengine 10 kujeruhiwa katika shambulio lililofanywa na waasi wa nchi hiyo karibu na mji wa Timbuktu wa kaskazini mwa nchi hiyo.
Duru za kuaminika zimeripoti habari hiyo na kusema kuwa shambulio hilo lilifanywa jana na waasi wa Tuareg.
Afisa mmoja wa masuala ya misaada ya kibinadamu katika eneo hilo amesema kuwa, waasi wanaopigania kujitenga eneo la Azawad kwa kifupi CMA walipambana na wanajeshi wa serikali jana asubuhi ambapo wanajeshi wanane waliuawa na wengine 10 kujeruhiwa.
Kwa mujibu wa afisa huyo, magari mawili ya jeshi la Mali yamechomwa moto na waasi hao.
Jeshi la Mali limekataa kutoa maelezo rasmi kuhusu habari hiyo ingawa hata hivyo afisa mmoja wa kikosi cha dhiba cha jeshi la Mali kilichotumwa katika eneo hilo amethibitisha habari hiyo.

Meli ya Iran yaendelea na safari yake kuelekea Yemen

Meli ya misaada ya kibinadamu ya Iran kwa ajili ya wananchi wanaondelea kushambuliwa kinyama na Saudi Arabia huko Yemen inaendelea na safari yake baada ya kuondoka katika bandari ya Bandar Abbas, kusini mwa Iran.
Meli hiyo ya mizigo iliyopewa jina la Nejat yaani "wokovu" ina tani 2,500 za mahitaji ya lazima zaidi kikiwemo chakula, madawa na mahema.
Mbali na maafisa wa Hilal Nyekundu ya Iran, wanaharakati kadhaa wa kimataifa wamo ndani ya meli hiyo. Kati ya wanaharakati hao wako wafanyakazi wa kutoa misaada ya kibinaadamu, hudumza za afya na wanaharakati wa kutetea amani kutoka Marekani, Ufaransa na Ujerumani.
Waandishi wa habari na timu ya madaktari kutoka Iran ni miongoni mwa watu waliomo kwenye meli hiyo.
Meli hiyo itapitia Lango Bahari la Hormuz, Ghuba ya Oman, Bahari Arabu na yamkini ikatia nanga katika Ghuba ya Aden au kuelekea Bandari ya Hudaydah. Wakati huo huo Sayyid Amir Mohsen Zeyai, mkuu wa shirika la Hilal Nyekundu la Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amelilaumu vikali shirika la kimataifa la Msalaba Mwekundu kwa kudharau masaibu yanayoendelea kuwatesa wananchi wasio na hatia wa Yemen

Pakistan yatuma askari usalama nchini Bahrain

Viongozi wa Pakistan wametangaza kuwa wametuma askari maalumu wa masuala ya kiusalama nchini Bahrain baada ya kuombwa na viongozi wa ukoo wa kifalme wa Aal Khalifa ili kupambana na wimbi la mapinduzi la wananchi wa nchi hiyo. Shirika la habari la Reuters limezinukuu duru za Pakistan zikifichua jana kuwa, askari maalumu wa masuala ya kiusalama wa Pakistan wametumwa nchini Bahrain ili kushirikiana na mamluki kutoka nchi nyinginezo kwa ajili ya kuzima harakati za kimapinduzi za wananchi wa nchi hiyo. Hayo yameripotiwa katika hali ambayo wachambuzi wa masuala ya kisiasa wanaamini kuwa, si jambo rahisi kuweza kuzimwa harakati hizo za wananchi wa Bahrain hasa kutokana na kuwa, Saudia ambayo imetuma wanajeshi wake kukandamiza wananchi wa Bahrain, hivi sasa inafanya jinai pia katika nchi nyingine ya Kiarabu na Kiislamu ya Yemen. Vile vile utawala wa kifalme wa Bahrain unaendelea kumshikilia Sheikh Ali Salman, Katibu Mkuu wa chama cha Kiislamu cha al Wifaq cha nchi hiyo pamoja na Nabil Rajab, mwanaharati wa haki za binadamu wa Bahrain. Utawala wa ukoo wa Aal Khalifa huko Bahrain umeomba msaada kutoka kwa Marekani, Saudi Arabia na baadhi ya nchi kama vile Pakistan ili kuzima harakati za wananchi wa nchi hiyo wanaopigania haki zao na kuupinga utawala huo wa kiimla

Televisheni ya al Masirah yaonesha ndege ya Morocco

Mabaki ya ndege ya kijeshi ya Morocco iliyotunguliwa na wanamapambano wa kikabila wa Yemen Mabaki ya ndege ya kijeshi ya Morocco iliyotunguliwa na wanamapambano wa kikabila wa Yemen
Televisheni ya al Masirah ya nchini Yemen imerusha hewani mkanda wa video unaoonesha ndege yenye bendera ya Morocco iliyoangushwa na wanamapambano wa kikabila wa Yemen kaskazini mwa nchi hiyo. Katika mkanda huo wa video, anaonekana mwandishi wa televisheni hiyo akionesha baadhi ya mabaki ya ndege hivyo ambapo katika sehemu moja ya mabaki hayo ya ndege kunaonekana pia bawa la ndege lenye bendera ya Morocco. Wapiganaji wa kikabila wanaonekana wakishingiria na kukusanya mabaki ya ndege hiyo ya kijeshi ya Morocco aina ya F16 iliyokuwa inafanya mashambulizi dhidi ya wananchi wa Yemen. Huku hayo yakiripotiwa, Naibu Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran anayehusika na masuala ya Afrika na Kiarabu, Hussein Amir Abdollahiyan amesema kuwa kinachotarajiwa kutoka kwa Umoja wa Mataifa ni kuchukua hatua za maana za kukomesha uadui wa Saudi Arabia dhidi ya wananchi wa Yemen. Bw. Abdollahiyan alisisitiza hayo katika mazungumzo ya simu baina yake na mjumbe mpya wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa katika kadhia ya Yemen, Bw. Ismail Ould Cheikh

Jeshi la Iraq laua wanamgambo 73 wa kundi la Daesh

Uongozi wa operesheni za kijeshi za Dijla nchini Iraq umetangaza kuwa, vikosi vya nchi hiyo vimefanikiwa kukomboa kikamilifu kisima cha mafuta cha Ajil, mashariki mwa mji wa Tikrit baada ya kupambana vikali na wanamgambo wa kundi la kigaidi la Daesh na kuua wanamgambo 73.
Vyombo vya habari vya Iraq vimemnukuu Luteni Jenerali Abdul Amir al Zaydi akisema kuwa, mapigano makali yalizuka baina ya vikosi vya Iraq na wanamgambo wa Daesh na kupelekea wanamgambo 73 kuuawa wakiwemo wenye uraia wa kigeni.
Luteni Jenerali al Zaydi ameongeza kuwa, askari watatu wa vikosi vya ulinzi vya Iraq wameuawa na wengine 13 kujeruhiwa katika mapambano hayo.
Vikosi vya ulinzi vya Iraq vimefanikiwa pia kuangamiza magari 37 ya kivita ya kundi la kigaidi la Daesh.
Ameongeza kuwa, kisima hicho cha mafuta kilichovamiwa na wanamgambo wa Daesh kinadhibitiwa kikamilifu na vikosi vya ulinzi vya Iraq hivi sasa

Saudia yashirikiana kijasusi na utawala wa Kizayuni

Ndege ya Saudi Arabia ikiwa katika Uwanja wa Ndege wa Ben-Gurion huko Tel Aviv. Ndege ya Saudi Arabia ikiwa katika Uwanja wa Ndege wa Ben-Gurion huko Tel Aviv.
Duru za kuaminika zimefichua kuwa, Saudi Arabia na utawala wa Kizayuni wa Israel zimetiliana saini mkataba wa ushirikiano wa kijasusi katika suala la Yemen pamoja na kutumiwa ndege zisizo na rubani za Kizayuni katika anga ya Yemen. Mwandishi wa Radio Tehran amezinukuu duru za kuaminika zikifichua kuwa, Khalid bin Ali bin Abdullah al Hamidan, mkuu wa shirika la kijasusi la Saudi Arabia hivi karibuni alielekea katika ardhi za Palestina zinazokaliwa kwa mabavu na Wazayuni na kutia saini mkataba wa ushirikiano wa kijasusi kati ya Saudia na utawala wa Kizayuni wa Israel. Kabla ya hapo baadhi ya vyombo vya habari kama vile televisheni ya al Alam na gazeti la Kizayuni la Yediot Ahronot vilitangaza habari ya kutua ndege ya Saudi Arabia katika uwanja wa ndege wa Ben-Gurion huko Tel Aviv. Mashirika ya habari yalisema kuwa ndege hiyo ilikuwa ya mwana mmoja wa ukoo wa kifalme wa Aal Saud ingawa Saudia ilidai kuwa ndege hiyo ilikuwa na shirika la ndege la Ureno. Hii si mara ya kwanza kuripotiwa habari za ushirikiano baina ya utawala wa Kizayuni wa Israel na ukoo wa Aal Saud na habari za kuweko ushirikiano mpya baina ya pande hizo mbili dhidi ya wananchi wa Yemen zinatilia nguvu ushirikiano wa muda mrefu baina ya Saudia na utawala wa Kizayuni wa Israel.

Monday, 11 May 2015

Kikwete aitisha mkutano wa EAC kuijadili Burundi

Rais Jakaya Kikwete wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ameitisha mkutano wa wakuu wa nchi tano za Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) ili kujadili mgogoro unaoikabili Burundi. Rais Kikwete ameitisha mkutano huo wakati Burundi ikiripotiwa kuwa katika vurugu zinazotishia hali ya usalama, hasa kipindi hiki cha kuelekea uchaguzi mkuu wa mwezi ujao. Rais Kikwete ambaye ni Mwenyekiti wa Kiduru wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) amesema kuwa, kuna haja ya kufanyika mkutano huo kwa ajili ya kujadili mgogoro wa kisiasa unaoikabili Burundi. Rais Kikwete amesema kama ninavyomnukuu: “Tumekubaliana kuwa sisi ndani ya EAC yaani Tanzania, Kenya, Uganda, Rwanda na Burundi yenyewe tukutane Dar es Salaam, Jumatano ya keshokutwa, ili tujadiliane jinsi gani ya kuwasaidia ndugu zetu wa Burundi kuandaa uchaguzi wao kwa mafanikio, wakihakikisha kuwa nchi yao inabakia na umoja, utulivu, usalama na amani bila misukosuko isiyokuwa na sababu. Wakati huo huo, wimbi la wakimbizi wa Burundi wanaoingia Tanzania linazidi kuongezeka.

Wapinzani nchini Burundi waendelea kuandamana

Wapinzani nchini Burundi wamepuuza onyo la serikali la kupiga marufuku maandamano na badala yake wameendelea kuandamana wakipinga hatua ya Rais Pierre Nkurunziza ya kuogombea kwa muhula mwingine wakisisitiza kuwa, hatua hiyo inakinzana na Katiba na mkataba wa Arusha. Jana mamia ya wanawake waliandamana katika mji mkuu Bujumbura na kukusanyika katika Wizara ya Mambo ya Ndani ya nchi hiyo. Taarifa zaidi kutoka Burundi zinasema kuwa, mgogoro wa kisiasa unaoikabili nchi hiyo umezorotesha shughuli za kiuchumi. Jumuiya mbalimbali ukiwemo Umoja wa Afrika na Jumuiya ya Afrika Mashariki zimeendelea kutoa wito wa kudumishwa amani na utulivu nchini humo.
Takribani watu 15 wamepoteza maisha katika ghasia na maandamano nchini Burundi. Wapinzani wanasema Nkurunziza anakiuka mapatano ya Arusha yaliyomaliza vita vya ndani nchini humo, lakini wafuasi wa rais huyo wanasema katika muhula wake wa kwanza Nkurunziza alichaguliwa na Bunge na hivyo muhula huo hauwezi kuhesabiwa.

Zarif: Iran kupanua ushirikiano wake na Afrika Kusini

Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Iran amesema kuwa, Jamhuri ya Kiislamu iko tayari kustawisha zaidi ushirikiano wake na Afrika Kusini katika nyanja zote hususan uga wa kiuchumi. Dakta Muhammad Javad Zarif amesema hayo katika mazungumzo yake na Bi Maite Nkoana-Mashabane, Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Afrika Kusini ambaye yuko safarini hapa nchini na kuongeza kuwa, licha ya kuweko vikwazo, lakini Iran na Afrika Kusini zinaweza kuwa na ushirikiano katika masuala ya mafuta na kadhalika. Kwa upande wake Bi Maite Nkoana-Mashabane, amesema kuimarishwa ushirikiano wa Tehran na Pretoria ni jambo muhimu na kwamba, lengo la safari yake hapa nchini ni katika kuimarisha uhusiano huo. Aidha akizungumza kwenye kikao cha kamisheni ya pamoja ya uchumi ya Iran na Afrika Kusini Bi Nkoana-Mashabane alisema vikwazo ilivyowekewa Iran si vya kimantiki, vya upande mmoja na havina uhalali wa kisheria.

Afkham: Madai ya Ahmad Shaheed ni urongo mtupu

Msemaji wa Wizara ya Mashauri ya Kigeni ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema kuwa, madai ya Ahmad Shaheed, Ripota Maalumu wa Baraza la Haki za Binadamu la Umoja wa Mataifa anayeshughulikia Masuala ya Iran kwamba, hapa nchini kumekuwa kukitekelezwa unyongaji wa watu kwa siri na kunyongwa pia wafungwa wa kisiasa ni urongo mtupu. Marzieh Afkham amebainisha kwamba, madai hayo yanakinzana wazi na majukumu yake. Afkham amesema, Iran imebainisha mara chungu nzima kwamba, Ahmad Shaheed amekuwa akitegemea vyanzo vya uongo katika kuandaa ripoti zake ambazo zinapingana na uhalisia wa mambo. Msemaji wa Wizara ya Mashauri ya Kigeni ya Iran amebainisha kwamba, inasikitisha mno kwamba, utendaji kazi wa Ripota Maalumu wa Baraza la Haki za Binadamu la Umoja wa Mataifa anayeshughulikia Masuala ya Iran hauko katika mkondo sahihi na hautegemei ushahidi wa kweli. Amesema, madai hayo ya mara kwa mara dhidi ya Iran yana malengo ya kisiasa.

UNICEF: Hali ya kibinadamu Yemen ni mbaya

Mfuko wa Watoto wa Umoja wa Mataifa (UNICEF) umetahadharisha kuhusiana na hali mbaya ya kibinadamu inayoikabili Yemen kutokana na uvamizi na mashambulio ya kijeshi ya Saudi Arabia katika nchi hiyo na kusisitiza kwamba, hali ya kibianadamu nchini humo ni mbaya mno. Mohamed al-Asadi, msemaji wa Mfuko wa Watoto wa Umoja wa Mataifa (UNICEF) nchini Yemen amesema kuwa, hali ya kibinadamu nchini Yemen inazidi kuwa mbaya siku baada ya siku. Amesema, kutokana na mashambulio ya Saudia kusababisha hasara kubwa, hali ya kibinadamu ni mbaya na kwamba, wananchi wa nchi hiyo wanahitajia misaada zaidi. Tume ya kuchunguza hasara zitokanazo na mashambulizi hayo, imetangaza kuwa zaidi ya watu 2,000 wamekwishauawa na maelfu ya wengine kujeruhiwa. Hayo yanajiri katika hali ambayo, wanajeshi wa Yemen pamoja na wapiganaji wa harakati ya wananchi ya Ansarullah wamekaribisha kwa mikono miwili pendekezo la usitishwaji mapigano kwa muda ili kuruhusu misaada ya kibinadamu kuwafikia raia wa kawaida wanaokabiliwa na matatizo. Usitishaji vita huo wa siku tano utaanza kutekelezwa kesho

Asoma adhana katika majimbo yote 50 ya Marekani

Jameel Syed, Muislamu wa jimbo la Michigan nchini Marekani amekamilisha safari yake ya siku 35 ya kuzunguka na kusoma adhana katika majimbo yote 50 ya nchi hiyo. Syed ambaye kitaalmu ni afisa masoko na mwadhini katika msikiti ulioko kwenye kiunga cha Rochester katika jimbo la Michigan, alikamilisha ziara yake hiyo ya kidini siku ya Ijumaa kwa kuadhini katika msikiti huo. Jameel Syed, mwenye umri wa miaka 40 anasemekana kuwa ni mtu wa kwanza kusoma adhana katika majimbo yote 50 ya Marekani. Akizungumzia safari yake hiyo Syed amesema, ilikuwa ni safari kubwa na ya kustaajabisha ambayo ilimkutanisha na Waislamu wa rangi na asili tofauti, pamoja na wasiokuwa Waislamu katika vituo vya taksi, viwanja vya ndege na misikiti. Miongoni mwa maeneo alikosoma adhana Muislamu huyo ni katika ufukwe wa Hawai ambako alikutana na kuzungumza pia na wasiokuwa Waislamu. Jameel Syed alifanya ziara pia katika msikiti wa Chapel Hill huko Carolina Kaskazini walikokuwa wakisali wanachuo watatu Waislamu waliouliwa kwa kupigwa risasi na Mzungu mmoja mapema mwaka huu. Itakumbukwa kuwa mnamo tarehe 10 Februari, Craig Hicks aliwaua kwa kuwapiga risasi Deah Shaddy Barakat aliyekuwa na umri wa miaka 23, mke wake Yusor Mohammad Abu-Salha, miaka 21 pamoja na dada yake Razan Mohammad Abu-Salha aliyekuwa na umri wa miaka 19 karibu na Chuo Kikuu cha Carolina Kaskazini. Japokuwa polisi ilitangaza kuwa mauaji ya wanachuo hao Waislamu yalitokana na mzozo juu ya eneo la kuegesha magari, lakini wazazi wa marehemu hao wamesema watoto hao waliuliwa kwa sababu ya chuki za kidini. Jameel Syed alikutana na familia za vijana hao wa Kiislamu na kuwapa mkono wa pole kwa msiba huo uliowafika

Friday, 8 May 2015

AU yasema hali hairuhusu kufanyika uchaguzi Burundi

Umoja wa Afrika (AU) umeonya leo kuwa hali ya Burundi si mwafaka kwa ajili ya kufanyika uchaguzi na kusema kuwa haitoweza kutuma waangalizi wake nchini humo baada ya malalamiko ya machafuko yaliyosababisha vifo, yaliyochochewa na hatua ya Rais wa nchi hiyo Pierre Nkurunziza kuamua kugombea urais kwa kipindi kingine cha tatu. Mkuu wa Kamisheni ya AU Bi Nkosazana Dlamini Zuma amesema mazingira yaliyopo si mwafaka kwa ajili ya uchaguzi na kuongeza kama ninavyomnukuu:”Huwezi kwenda kwenye nchi ambayo unakutana na wakimbizi wanaoondoka, kisha useme, ‘tunakwenda kufanya uangalizi wa uchaguzi’”. Mkuu wa Kamisheni ya Umoja wa Afrika amebainisha kuwa kutokana na mambo yalivyo haoni hata kama uchaguzi utaweza kufanyika katika mazingira hayo. Kuhusiana na uamuzi wa Mahakama ya Katiba ya Burundi wa kumuidhinisha Rais Nkurunziza kugombea urais kwa muhula wa tatu, Bi Nkosazana Dlamini Zuma amesema, ukiondoa mahakama hiyo, tafsiri nyengine zote wanazopatiwa kuhusiana na katiba ya nchi hiyo zinaonyesha kuwa Rais Nkurunziza hafai kugombea kwa kipindi cha tatu. Wakati huohuo watu wasiopungua wanne wameuawa katika wimbi jipya la machafuko yaliyosababishwa na upinzani dhidi ya hatua ya Rais Pierre Nkurunziza ya kugombea urais kwa kipindi kingine cha tatu. Kwa mujibu wa Shirika la Msalaba Mwekundu maiti tatu zimeonekana leo kwenye barabara za mji mkuu Bujumbura. Mtu mwengine ameuawa kwa guruneti katika mapigano kati ya polisi, waandamanaji na wanamgambo wanaoiunga mkono serikali wajulikanao kama Imbonerakure. Katika tukio jengine lililotokea kwenye wilaya ya Nyakabiga jijini Bujumbura leo, waandamanaji wanaopinga Rais Nkurunziza kugombea tena urais wamemuua kwa kumvisha matairi ya moto shingoni mtu mmoja, wakisema ni mwanachama wa tawi la vijana la chama tawala ambaye aliwahi kuwashambulia wakati walipokuwa wakiandamana…/
Zaidi katika kategoria hii:

Mwanachama wa Al Shabab ajisalimisha Kenya

Serikali ya Kenya, imetangaza kuwa mwanachama mmoja wa kundi la kigaidi la ash-Shabab nchini Somalia amejisalimisha kwa jeshi la polisi huko mkoani Garissa, kaskazini mashariki mwa nchi hiyo. Kwa mujibu wa duru za usalama nchini humo, mwanachama huyo wa kundi hilo ambalo limekuwa likitekeleza jinai katika siku za hivi karibuni, amejisalimisha kwa polisi ya Kenya baada ya kujiengua kutoka kundi hilo. Kwa mujibu wa taarifa hiyo, gaidi huyo wa ash-Shabab ambaye bado hajatajwa jina lake, amechukua uamzi huo kulalamikia jinai ambazo zimekuwa zikitekelezwa na wanachama wa kundi hilo dhidi ya watu wasio na hatia katika maeneo tofauti ya ndani na nje ya Somalia. Inaelezwa kuwa kijana huyo mwenye umri wa miaka 22, ambaye hajatajwa kwa sababu za kiusalama, alijiunga na kundi hilo hapo mwaka 2011. Amesema kuwa, amejisalimisha kwa jeshi la serikali kupitia fremu ya msamaha uliotangazwa na serikali ya Nairobi kwa wanachama wa kundi hilo. Kwengineko viongozi wa serikali ya Nairobi wametangaza kuwa, makumi ya vijana waliokuwa wamejiunga na kundi hilo la kigaidi, wamerejea makwao kufuatia operesheni za askari wa kusimamia amani wa Umoja wa Afrika nchini Somalia AMISOM. Mwanzoni mwa mwaka huu, serikali ya Kenya ilitangaza msamaha kwa wote kwa ajili ya vijana waliojiunga na kundi la kigaidi la ash-Shabab.

Wanigeria waliokuwa Niger walazamika kurudi makwao

Maelfu ya raia wa Nigeria waliokimbia mashambulizi ya kundi la kigaidi na kitakfiri la Boko Haram, wamefukuzwa nchini Niger. Taarifa iliyotolewa leo na kiongozi mmoja wa Niger, imesema kuwa, zaidi ya watu elfu tatu miongoni mwa wavuvi na wakimbizi raia wa Nigeria ambao walikimbia nchi yao kutokana na mashambulio ya kundi hilo, tayari wameondoshwa nchini humo. Kwa upande wao raia hao wa Nigeria, wamenukuliwa wakisema kuwa, wamelazimika kurejea nchini mwao na kwamba mamia ya wakimbizi wengine wa nchi hiyo nao wanajiandaa kurudi makwao. Wameongeza kuwa, watu watatu kati yao walipoteza maisha kutokana na kutembea kwa muda mrefu usiopungua siku tatu katika safari hiyo ya kurejea kwao. Kufuatia taarifa hiyo, serikali ya Nigeria, imeahidi kupeleka malori kwa ajili ya kuwabebea wakimbizi hazo. Charles Otegbabe, mmoja wa maafisa wa serikali ya Nigeria amethibitisha habari hiyo na kusema kuwa, serikali imewapokea wakazi wa mji wa Gaidam, uliopo katika jimbo la Borno ambao awali walikimbilia nchini Niger ili kuokoa maisha yao kipindi kundi la Boko Haram liliposhadidisha jinai zake nchini humo. Kwa mujibu wa serikali ya Niger,  Jumatatu iliyopita, jeshi la nchi hiyo lilitekeleza operesheni katika eneo la ziwa Chad nchini humo na kuchukua hatua ya kuwahamisha raia kutoka sehemu moja kwenda nyengine . Hii ni katika hali ambayo Niger, imewapa hifadhi raia wapatao laki moja wa Nigeria waliokimbilia nchini humo kuokoa maisha yao kutokana na mashambulizi ya kundi la Boko Haram.

Daesh wagawa madawa ya kulevya kwa vijana wa Iraq

Duru za habari kutoka Iraq, zimeripoti kuwa, kundi la kigaidi na kitakfiri la Daesh limekuwa likigawa madawa ya kulevya kwa vijana wa nchi hiyo ili kuwafanya waweze kujiunga na kundi hilo katika kutekeleza jinai za kigaidi. Hayo yamethibitishwa na Farhan Muhammad, kiongozi mwandamizi wa Baraza la Mkoa wa al-Anbar na kuongeza kuwa, baada ya kundi hilo la kigaidi linalotenda jinai kwa jina la Uislamu, kuingiza idadi kubwa ya madawa ya kulevya ya aina mbalimbali vikiwemo vidonge kupitia mipaka ya Syria kuelekea al-Anbar, wanachama wa Daesh, wamekuwa wakigawa madawa hayo ya kulevya kwa vijana wa mkoa huo kitendo kinachotajwa kuwa ni njia mojawapo ya kuweza kuwafanya vijana wengi wajiunge nalo. Kwa mujibu wa afisa huyo wa serikali, kundi la Daesh, linatekeleza mpango wa kuwatia kasumba vijana, sanjari na kuwatumia katika kutekeleza jinai zake hapo baadaye. Amewataka viongozi wa kundi hilo linalojinadi kuwa na mafungamano na Uislamu kutekeleza jukumu lao la kidini, badala ya kwenda kinyume na misingi ya dini hiyo tukufu inayopiga marufuku vitendo vya aina hiyo. Hayo yanajiri katika hali ambayo, hivi karibuni kulienea habari kwamba, wanachama wa kundi la kigaidi na kitakfiri la Daesh wamekuwa wakitumia vidonge vya kulevya ili kuwafanya wasipitiwe na usingizi vitani. Mbali na hapo hivi karibuni pia kundi hilo liliifanyia matengenezo hoteli ya kimataifa ya Nainawa iliyopo katika mji wa Mosul nchini Iraq ambayo itatumiwa na makamanda wake katika starehe na anasa. Mambo hayo pamoja na mengineyo, ndiyo yaliyowafanya weledi wa mambo waamini kuwa, kundi hilo kinyume na madai yake, linakwenda kinyume na misingi ya Kiislamu na linatekeleza njama za Wamagharibi dhidi ya dini hiyo tukufu

Magaidi Syria waungana kupambana na kundi la Daesh

Makundi ya kigaidi kusini mwa Syria yameungana na kutekeleza mashambulizi makali dhidi ya wanachama wa kundi la kigaidi na kitakfiri la Daesh nchini humo. Habari kutoka kwa magaidi hayo, zimeeleza kuwa, kundi la kitakfiri la Jab’hatu Nusra na makundi mengine yanayopigana dhidi ya serikali halali ya Syria, yaliungana siku chache zilizopita na kutekeleza operesheni kali dhidi ya wanachama wa kundi la Daesh katika eneo la al-Qahtwaniyyah, katika viunga vya mji wa al-Qunaitra, kusini mwa Syria na kufanikiwa kudhibiti ngome muhimu ya wanachama wa kundi hilo. Katika mapigano hayo makali, makumi ya matakfiri wa kundi la Jab’hatu Nusra na Daesh, wameangamizwa huku wengine wengi wakijeruhiwa vibaya. Makundi hayo ya kitakfiri yaliyoungana katika operesheni za kuitwaa ngome hiyo muhimu ya kundi la kigaidi la Daesh, ni pamoja na makundi ya kigaidi ya Jayshul-Islami, Jayshul-Yarmuuk, Jayshul-Awwal na Ahrarush-Sham, yote ya Masalafi wa Kiwahabi ambayo yanapambana dhidi ya serikali ya nchi hiyo. Kwengineko jeshi la Syria kwa kushirikiana na wanamapambano wa Harakati ya Kiislamu ya Hizbullah, limefanikiwa kudhibiti kikamilifu maeneo ya Isal al-Ward lenye upana wa kilometa mraba 45 katika mipaka ya pamoja kati ya Syria na Lebanon, al-Qaranah, Wadi al-Dar na Wadi al-Sahrij, yaliyoko katika miinuko ya al-Qalamun nchini Syria. Katika operesheni za kudhibiti maeneo hayo, makundi ya magaidi wa kundi la Jab’hatu Nusra, wakiwamo Abu Mujahid na al-Aswad, makamanda wa ngazi za juu wa kundi hilo, wameangamizwa na jeshi la nchi hiyo na wanamapambano wa Hizbullah ya Lebanon

Monday, 4 May 2015

Uandikaji matini ya makubaliano waendelea vyema

Zarif Zarif
Waziri wa Mambo ya Nje wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema kuwa: Uandikaji wa matini ya makubaliano ya nyuklia kati ya Iran na kundi la 5+1 unaendelea vizuri, ijapokuwa bado kuna masuala mengi yaliyosalia. Muhammad Jawad Zarif amesema kuwa, mazungumzo ni magumu, lakini amesisitiza kwamba Iran na kundi la 5+1 zina nia ya kweli ya kutatua migogoro migumu ili kufungua kurasa mpya. Pande hizo mbili za mazungumzo ya nyuklia zilianza kazi ya kuandika matini ya makubaliano ya nyuklia Alkhamisi iliyopita huko New York Marekani.
Mazungumzo hayo yanafanyika kwa kuhudhuriwa na Sayyid Abbas Araqchi na Majid Takhte Ravanchi, Manaibu Mawaziri wa Mambo ya Nje wa Iran na Helga Schmid, Naibu Mtaribu wa Siasa za Nje wa Umoja wa Ulaya. Sayyid Abbas Araqchi, afisa mwandamizi katika timu ya mazungumzo ya nyuklia ya Iran pia amesema kuwa anataraji kwamba rasimu ya makubaliano kamili itakuwa tayari, ingawa kutakuwepo na masuala mengi yaliyosalia kwenye rasimu hiyo.

Hamas ipo tayari kushiriki uchaguzi Palestina

Wafuasi wa Hamas Wafuasi wa Hamas
Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina Hamas imetangaza kuwa ipo tayari kushiriki katika kinyang'anyiro cha uchaguzi wa bunge na urais wa Mamlaka ya Ndani ya Palestina. Hamas imetoa taarifa na kutangaza utaarifu wake kwa ajili ya kushiriki katika uchaguzi wa Palestina na kumtuhumu Mahmoud Abbas, Rais wa Mamlaka ya Ndani ya Palestina kuwa ndiye anayekwamisha utekelezaji wa mchakato wa kisheria wa uchaguzi. Taarifa ya Hamas imeongeza kuwa Mahmoud Abbas halipi uzito wa hali ya juu suala la kufanyika uchaguzi na anakwamisha kuainishwa tarehe ya kufanyika chaguzi hizo. Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina Hamas vile vile imeshutumu matamashi ya Mahmoud Abbas kwamba upo ulazima kwa Hamas kuwasilisha ombi la kimaandishi kwa ajili ya kufanyika uchaguzi huo na kuongeza kuwa matamshi hayo ni wazi yatazidisha mgawanyiko kati ya Wapalestina na kukwamisha kufikiwa makubaliano na mapatano ya kitaifa.

Czech yakosoa vikwazo dhidi ya Russia

Zeman Zeman
Rais Milos Zeman wa Czech amesema kuwa vikwazo vilivyowekwa kwa Russia kutokana na mgogoro wa Ukraine havina athari bali vinachochea hali ya mivutano. Rais wa Czech amesema kuwa vikwazo vya Magharibi dhidi ya Russia havina athari, bali vimekuwa tu vikizidisha hali ya mivutano na ametaka kuondolewa vikwazo hivyo haraka iwezekanavyo.
Madola ya Magharibi yameiwekea Russia vikwazo ka kuituhumu nchi hiyo kwamba inahusika katika mgogoro mkubwa wa hivi sasa katika nchi jirani ya Ukraine; mgogoro ulioibuka baada ya Kiev kuanzisha oparesheni za kijeshi dhidi ya vikosi waitaki wa Russia mashariki mwa Ukraine mwaka uliopita. Russia imekanusha tuhuma hizo za Magharibi dhidi yake

Wakala wa Daesh atiwa nguvuni Lebanon

Magaidi wa Daesh Magaidi wa Daesh
Mwanachama wa ngazi ya juu wa kundi la kigaidi na kitakfiri la Daesh ametiwa mbaroni nchini Lebanon huku akiwa na pasi bandia ya kusafiria. Ibrahim al Barakat alitiwa mbaroni mapema jana na anatuhumiwa kwa kuwa wakala wa kundi la kigaidi la Daesh. Hayo yameelezwa na afisa usalama wa Lebanon. Barakat alitiwa mbaroni wakati alipokuwa akijaribu kuelekea Uturuki kupitia kaskazini mwa Lebanon huku akitumia pasipoti bandia.
Mbali na kuvishambulia vikosi vya Lebanon mwaka jana, Ibrahim al Barakat aliye na umri wa miaka 40 anakabiliwa na tuhuma za kuwasajili vijana kutoka Tripoli, mji mkubwa zaidi huko kaskazini mwa Lebanon, kwa ajili ya kupigana na wanamgambo huko Syria na Iraq. Tarehe 11 mwezi Oktoba mwaka jana, wanajeshi 11 wa Lebanon waliuliwa baada ya mapigano kuzuka kufuatia kutiwa mbaroni raia mmoja wa Lebanon aliyekuwa akituhumiwa kuwasajili vijana kujiunga na makundi ya kigaidi huko Syria.

Watu waliovalia sare za jeshi waua makumi Nigeria

Watu waliokuwa na silaha wameuwa makumi ya raia, wengi wao wakiwa wanawake na watoto huko Nigeria katika mfululizo wa mashambulizi dhidi ya vijiji kadhaa katika jimbo la Plateau. Nanzing Bani kiongozi wa jamii katika eneo amesema kuwa mauaji hayo yalitokea jana wakati watu waliokuwa na silaha huku wakiwa wamevalia sera za kijeshi walifanya ufyatuaji risasi wa kiholela dhidi ya raia huko katika eneo la Kardarko na katika vijiji jirani jimboni Plateau. Kiongozi huyo wa kieneo amesema kwamba idadi ya waliouawa inaweza kufikia 100. Watu walioshuhudia na wenyeji wa eneo hilo wamesema kuwa wavamizi walichoma moto majengo na nyumba nyingi katika eneo hilo. Mashambulizi hayo ya watu wenye silaha yamepelekea makumi ya wakazi wa eneo hilo la katika jimbo la Plateau kuzihama nyumba zao.

Ubaguzi wa rangi, mgogoro wa kitaifa Marekani

Kufuatia kuongezeka ghasia zitokanazo na ubaguzi wa rangi Marekani, Spika wa Bunge la Baraza la Wawakilishi nchini humo amesema uhusiano baina ya Wamarekani wenye asili ya Afrika na maafisa wa polisi sasa umegeuka na kuwa mgogoro wa kitaifa. John Boehner katika mahojiano na Televisheni ya NBC amesisitiza kuwa maafisa wa usalama wa umma hawapaswi kujihusisha na vitendo vya utumiaji mabavu. Marekani hivi sasa imekumbwa na mgogoro wa kitaifa. Hiyo ni kauli ya kiongozi nambari tatu Marekani baada ya rais na makamu wake. Katika mgogoro huo, mamilioni ya Wamarekani weusi au wenye asili ya Afrika daima wananyanyaswa na kufanyiwa ukatili wa maafisa wa usalama na polisi wazungu. Katika kipindi cha mwaka moja uliopita, kumeshuhudia visa kadhaa vya polisi wazungu wakiwafyatulia risasi na kuwaua kiholela Wamarekani wenye asili ya Afrika. Katika vitendo hivyo vya unyama na ukatili, polisi huwalenga na kuwafyatulia risasi washukiwa ambao aghalabu huwa vijana na mabarobaro. Katika kitendo cha hivi karibuni cha ukatili huo wa polisi Freddie Gray, Mmarekani mweusi baada ya kutiwa nguvuni na polisi mzungu alipigwa na kuadhibiwa vikali ndani ya gari la polisi na kisha kukimbizwa hospitali kutokana na majeraha aliyoyapata. Akiwa hospitalini alifariki dunia. Kufuatia tukio hilo, mji wa Baltimore umeshuhudia machafuko makali zaidi ya mitaani ambapo wananchi wenye hasira wamejitekeza kwa moto kulalamikia ubaguzi na ukatili wa polisi ya Marekani. Machafuko hayo yametajwa kuwa mabaya zaidi katika miaka ya hivi karibuni. Ikumbukwe kuwa katika historia ya Marekani kumeshuhudiwa uasi na maandamano ya Wamarekani weusi wakilalamikia ubaguzi wa rangi nchini humo. Kilele cha malalamikio hayo kilikuwa katika miongo ya 1950 na 1960 ambapo mashinikizo yalipelekea kuidhinishwa sheria kadhaa ikiwemo sheria ya kuwapa Wamarekani weusi haki ya kupiga kura. Pamoja na hayo, hivi  sasa baada ya kupita zaidi ya miaka 50 tokea kuibuka mapambano ya haki za kijamii Marekani, Wamarekani wenye asili ya Afrika wangali wanakabiliwa na ubaguzi mkubwa na dhulma zisizo na kikomo. Hali imekuwa mbaya kiasi kwamba hivi sasa maafisa kadhaa wazungu katika kikosi cha polisi Marekani wamefyatuliwa risasi katika kile kinachotajwa kuwa ni ulipizaji kisasi. Weledi wa mambo wanasema hali kama hivyo itaitumbukiza Marekani katika mgogoro mkubwa sana wa kiusalama. Marekani ni moja za nchi zenye idadi kubwa zaidi ya silaha ndogo ndogo miongoni mwa raia. Inakadiriwa kuwa katika kila Wamarekani watatu, moja au wawili kati yao wana silaha. Idadi kubwa ya silaha hizo pia ziko mikononi mwa Wamarekani wenye asili ya Afrika na wasiokuwa wazungu. Kwa msingi huo inadokezwa kuwa iwapo maandamano hayatapelekea kumazilika vitendo vya ubaguzi wa rangi na ukatili wa maafisa wazungu katika vikosi vya usalama, basi natija itakuwa ni kuanza mapambano ya silaha mitaani. Jamii ya Marekani hivi sasa katika upande moja inakabiliwa na matatizo makubwa ya ubaguzi wa rangi na katika upande wa pili inakumbwa na mgogoro wa kiuchumi na kupungua kiwango cha maisha bora katika jamii na hayo yote yamepelekea kuongezeka mashinikizo ya kila aina. Ni kwa sababu hii ndio weledi wa mambo wanasema Marekani sasa iko katika dimbwa kubwa la mgogoro wa kijamii ambao unaweza kuwa hatua ya kwanza ya mapinduzi au hata vita vya kitabaka na kirangi. Hatua ya John Boehner, Spika wa Baraza la Wawakilishi ambaye ni kiongozi nambari tatu nchini Marekani kutumia ibara ya ‘mgogoro wa kitaifa’ katika kufafanua kuhusu machafuko ya ubaguzi wa rangi hivi sasa nchini humo ni kengele ya hatari kuhusu kuibuka umwagikaji damu nchini humo.

Friday, 1 May 2015

Garissa:Vyombo vya usalama vilizembea?

Waziri wa usalama wa ndani nchini Kenya Generali Joseph Nkaiserry amekiri kwamba vyanzo na duru za kijasusi zilitahadharisha lakini zilipuuzwa kabla ya shambulizi la Al Shabaab katika chuo kikuu cha Garrissa.
Karibu watu 150 walikufa wakati wa shambulio hilo.
Waziri Nkaissery ameongeza kusema shughuli za wokozi zilizofuata pia zilifanywa kiholela.
Baadhi ya Maafisa wakuu wa polisi wamesimamishwa kazi kufuatia shambulia hilo la Chuo Kikuu cha Garrissa

Maandamano mapya Baltimore Marekani

Kumetokea maandamano mapya nchini Marekani katika mji wa Baltimore kufuatia kifo cha kijana mweusi Freddie Gray aliyekufa kutokana na majeraha akiwa mikononi mwa polisi. Mamia ya watu wameandamana katika mitaa, wakionyesha ujasiri licha ya hali mbaya ya hewa iliyokuwepo
.
Matokeo ya mwanzo ya uchunguzi wa polisi wa jinsi kijana wa miaka ishirini na mitano mwenye asili ya weusi alivyouawa bado hayajawekwa hadharani.

Kiongozi wa waasi wa ADF atiwa mbaroni nchini TZ

Habari kutoka nchini Tanzania zinasema kuwa, kiongozi wa kundi la waasi wa ADF wa nchini Uganda ametiwa mbaroni nchini Tanzania. Vyombo vya habari yakiwemo magazeti ya nchini Uganda yamethibitisha kutiwa mbaroni mtu anayeaminiwa kuwa ni Jamil Mukulu, mkuu wa kundi la waasi wa ADF ambao wanatuhumiwa kufanya mauaji ya watu 300 tangu mwezi Oktoba hadi hivi sasa katika nchi jirani ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo. Habari zinasema kuwa Mukulu ametiwa mbaroni kwa ushirikiano wa polisi wa Tanzania na wenzao wa Uganda. Hata hivyo jeshi la Uganda limesema kuwa haliwezi kuthibitisha kuwa mtu aliyetiwa mbaroni ni Jamil Mukulu hadi atakapochukuliwa vipimo vya vinasaba, DNA. Kwa muda mrefu polisi ya Uganda ilikuwa imetoa amri ya kutiwa mbaroni kiongozi huyo wa waasi wa ADF mwenye umri wa miaka 51 kwa tuhuma za kufanya mauaji ya kigaidi na kuiomba Interpol iisaidie kutiwa mbaroni kiongozi huyo wa waasi. Kundi la ADF lilianzishwa mwaka 1995 mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo ili kupambana na siasa za Rais Yoweri Museveni wa Uganda

Ban asikitishwa na jinai za Saudia nchini Yemen

Ban Ki moon, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa amesema kuwa anasikitishwa na hatua ya Saudi Arabia ya kuendeleza mashambulizi nchini Yemen.
Ban alisema hayo jana na kuongeza kuwa, mashambulizi dhidi ya raia na miundombinu isiyo ya kijeshi zikiwemo hospitali na maeneo ya Umoja wa Mataifa nchini Yemen hayakubaliki kabisa na ni uvunjaji wa wazi wa haki za binadamu.
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa ametosheka tu na kusema anasikitishwa na jinai hizo za Saudi Arabia nchini Yemen katika hali ambayo mashambulizi dhidi ya nchi hiyo ya Kiarabu yameendelea kusababisha maafa kwa watu wasio na hatia.
Karibu watu 1,000 wameshauwa katika mashambulizi ya Saudia nchini Yemen wengi wao wakiwa ni wanawake na watoto wadogo.
Jana pia ndege za Saudi Arabia zilishambulia ofisi za televisheni ya al Masirah ambayo inahesabiwa kuwa marejeo makubwa ya habari zinazohusiana na mashambulizi ya Saudia nchini Yemen

Wamarekani waandamana kupinga manyanyaso

Mamia ya Wamarekani wenye hasira wamemiminika tena kwenye mitaa ya miji mbalimbali ya nchi hiyo kulalamikia mauaji ya Mmarekani mwenye asili ya Afrika, Freddie Gray aliyekufa kutokana na majeraha akiwa mikononi mwa polisi.
Mamia ya Wamarekani jana waliendelea kuandamana katika miji ya Baltimore, Maryland, Philadelphia, Pennsylvania pamoja na Cincinnati na Ohio.
Freddie Gray (25) alikufa tarehe 19 mwezi uliopita wa Aprili kutokana na majeraha makubwa, ikiwa ni wiki moja tu tangu alipotiwa mbaroni na polisi wa mji wa Baltimore. Maafisa sita wa polisi walioshiriki kumtia mbaroni Gray wamesimamishwa kazi.
Waandamanaji walibeba mabango yaliyoandikwa: "Komesha Ugaidi wa Polisi," "Sisi na watoto wetu si wahuni" n.k.
Miji mingi ya Marekani imeshuhudia maandamano katika kipindi cha wiki moja iliyopita na watu wengi wametiwa mbaroni na polisi kwa kushiriki kwenye maandamano hayo. Polisi wamewatia mbaroni zaidi ya watu 120 katika mji wa New York pekee.

UN yashindwa kudhibiti hali ya mambo nchini Libya

Mjumbe wa Umoja wa Mataifa amesema kuwa umoja huo umeshindwa kuyashawishi makundi hasimu nchini Libya kufanya mazungumzo baina yao. Mjumbe huo wa Umoja wa Mataifa nchini Libya ameyapa makundi ya Libya muda wa wiki moja yahakikishe kuwa yametangaza misimamo yao kuhusiana na muswada wa makubaliano ya amani yaliyopendekezwa na Umoja wa Mataifa. Bernardino Leon amesema kuwa, ana matumaini makubaliano hayo yataandaa mazingira mazuri ya kupatikana amani ya kudumu nchini Libya. Hata hivyo wanamgambo wa Fajr ambao wanaudhibiti mji mkuu Tripoli jana waliutaka Umoja wa Mataifa umuondoe mjumbe wake huyo nchini Libya. Aidha wanamgambo hao wamewataka wakazi wa Tripoli wajitokeze kwa wingi leo Ijumaa katika maandamano ya kupinga hatua ya Umoja wa Mataifa ya kuingilia mgogoro wa Libya. Kundi hilo pia limepinga waziwazi mwito wa Bernadino Leon, mwakilishi wa Umoja wa Mataifa nchini Libya wa kuyataka makundi hasimu yarejee kwenye meza ya mazungumzo ya amani. Mwezi Septemba mwaka 2014 Umoja wa Mataifa ulianza rasmi kupatanisha mgogoro wa Libya baina ya jeshi na wanamgambo wa nchi hiyo hata hivyo mapigano ya mara kwa mara yamekuwa yakikwamisha juhudi hizo za Umoja wa Mataifa.

Marekani yawapa magaidi wa Syria dola bilioni 3

Mkuu wa kundi linalojiita "Muungano wa Kitaifa wa Wapinzani wa Nje ya Syria" ameishukuru Marekani kwa kuyasaidia kifedha makundi ya waasi wa nchi hiyo na kuiomba iendelee kuwa pamoja na waasi hao kwa hali na mali.
Shirika la habari la Ufaransa limemnukuu Khaled Khoja akisema hayo jana wakati alipoona na John Kerry, Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani na kuongeza kuwa, anaishukuru mno Marekani kwa kutoa msaada wa dola bilioni 3 kwa waasi wa Syria ambao uliwezesha kuanzishwa vita dhidi ya serikali ya Damascus.
Khaled Khoja ameongeza kuwa, waasi wa Syria wanaiomba Marekani iwasaidie kuzuia mashambulizi ya serikali ya Damascus ya kukomboa maeneo yanayodhibitiwa na waasi.
Mkuu huyo wa wapinzani wa Syria walioko nje ya nchi hiyo aidha amefumbia macho jinai zinazoendelea kufanywa na makundi ya kigaidi na uungaji mkono wa kila hali wa Marekani kwa makundi hayo ya kigaidi na kudai kuwa Rais Bashar al Assad hana uhalali wa kuwa Rais wa nchi hiyo licha ya wananchi wa Syria kumchagua kwa kura nyingi

Mapigano mapya yaua watu 19 kaskazini mwa Mali

Watu wasiopungua 19 wameuawa katika mapigano yaliyozuka baina ya waasi wa Tuareg na wanajeshi wa serikali, kaskazini mwa Mali. Wizara ya Ulinzi ya Mali imetoa taarifa ikisema kuwa, wanajeshi 9 wameuawa baada ya waasi wa Tuareg wa CMA wanaopigania kujitenga eneo la Azawad kuushambulia mji wa Lere karibu na mpaka wa Mali na Mouritania siku ya Jumatano. Taarifa hiyo ya jana ya Wizara ya Ulinzi ya Mali imeongeza kuwa, wanajeshi wengine 6 wamejeruhiwa kwenye shambulio hilo na wengine sita kutekwa nyara. Wanajeshi wa Mali walifanikiwa kuua waasi 10 wa Tuareg na kuwajeruhiwa wengine 16 kwenye mapigano hayo. Vile vile walifanikiwa kuharibu magari ya waasi hao na kuteka silaha zao kadhaa. Wakati huo huo Waziri wa Ulinzi wa Mali Tieman Hubert Coulibaly amesema kuwa mji wa Mali bado umo mikononi wa serikali. Eneo la kaskazini mwa Mali limeshuhudia siku kadhaa za machafuko. Serikali ya Bamako inawalaumu waasi kwa kuchoche machafuko hayo ikisema kuwa waasi hao wamekusudia kuharibu kwa makusudi mwenendo wa mazungumzo ya amani nchini humo.