Nchi wanachama wa Baraza la
Ushirikiano la Ghuba ya Uajemi (PGCC) ambazo mwaka 2011 ziliingilia kati
mgogoro wa Yemen na kuzuia mapinduzi ya wananchi wa nchi hiyo kupata
ushindi, kwa mara nyengine tena, hivi sasa zinafanya kila njia ili
kuzima tena wimbi la mabadiliko ya kisiasa lililoanza nchini humo tangu
mwezi Julai mwaka huu. Katika taarifa iliyotolewa mwishoni mwa kikao cha
35 cha Baraza la Ushirikiano la Ghuba ya Uajemi kilichofanyika siku ya
Jumanne katika mji mkuu wa Qatar, Doha nchi wanachama wa PGCC zimetaka
wapiganaji wa Kihouthi wa Kamati za Wananchi waondoke katika mji mkuu wa
Yemen, Sana’a na katika maeneo mengine yanayodhibitiwa na wapiganaji
hao.
Ali Abdullah Saleh, ambaye kuanzia mwaka
1978 hadi 1990 alikuwa Rais wa Yemen ya Kaskazini, na kuanzia mwaka
1990 hadi mwaka 2011 alikuwa Rais pia wa Yemen iliyoungana, kama
ilivyokuwa kwa watawala wa aghalabu ya nchi za Kiarabu za Mashariki ya
Kati na za kaskazini mwa Afrika, mwaka 2011 naye pia alikabiliwa na
wimbi kubwa la upinzani wa wananchi. Japokuwa Saleh alijaribu kuzima
wimbi hilo la upinzani ili aweze kuendelea kubakia madarakani, lakini
wananchi wa Yemen walishikilia msimamo wao kuhakikisha dikteta huyo
anang’atuka madarakani. Licha ya hatua alizochukua Ali Abdullah Saleh
mwenyewe, baadhi ya watawala wa nchi za Kiarabu za eneo, nao pia
walijaribu kufanya juu chini ili kumwokoa dikteta huyo na gharika ya
mapinduzi ya wananchi wa Yemen. Baadhi ya nchi wanachama wa PGCC na hasa
Saudi Arabia ilikuwa moja ya viranja wakuu wa kumlinda Saleh na
kuhakikisha anaendelea kushika hatamu za utawala, lakini nguvu na ukubwa
wa wimbi la upinzani wa wananchi dhidi ya dikteta huyo, ziliulazimisha
utawala wa kifalme wa Aal Saud ufikirie mbinu na hila nyengine kupitia
PGCC ili kupotosha mkondo wa mapinduzi ya wananchi wa Yemen. Kulingana
na mpango huo Ali Abdullah Saleh aling’atuka madarakani kwa sharti la
kutoshtakiwa na kufatiliwa kisheria kwa jinai alizotenda, na akakabidhi
madaraka kwa makamu wake Abd Rabbuh Mansur Hadi, kupitia uchaguzi wa
kimaonyesho uliofanyika nchini humo. Mbinu na hila ya mpango wa Baraza
la Ushirikiano la Ghuba ya Uajemi ulipotosha mkondo wa mapinduzi ya
wananchi wa Yemen na kuwatumbukiza wananchi hao kwenye lindi la hali ya
mchafukoge wa kisiasa iliyoendelea kwa muda wa miaka mitatu. Kushadidi
hali hiyo na udhaifu mkubwa wa kiutendaji ulioonyeshwa na serikali ya
mpito ya Abd Rabbuh Mansur Hadi, viliwafanya wananchi, wakiongozwa na
harakati ya Mahouthi ya Ansarullah waanzishe wimbi jipya la maandamano
dhidi ya serikali hiyo. Kushadidi na kuendelea wimbi hilo la maandamano
ya upinzani lililoanza mwezi Julai mwaka huu hatimaye kuliipigisha
magoti serikali ya Mansur Hadi, ambapo mnamo mwezi Septemba ilikubaliana
na matakwa ya wananchi likiwemo la kujiuzulu serikali na kuundwa
serikali mpya kwa maafikiano na harakati ya Ansarullah. Hata hivyo
maafikiano hayo hayakukubaliwa na baadhi ya nchi wanachama wa PGCC
hususan Saudi Arabia na Imarati. Kwa mtazamo wa Saudia, kuundwa serikali
itakayotoa nafasi kuu kwa Ansarullah na kuifanya harakati hiyo iwe na
sauti kubwa katika matukio ya Yemen ni tishio dhidi ya mipaka yake na
pia kunaitia hofu na wasiwasi Riyadh juu ya kujitokeza mlingano mpya wa
nguvu katika eneo. Wapinzani wa Ansarullah katika eneo wanaitakidi kuwa
kupata nguvu harakati hiyo ambayo waungaji mkono wake waliowengi ni
Mashia wa Zaidiyyah kutazipa nguvu zaidi harakati nyengine za kupinga
tawala za kifalme katika nchi nyengine za Kiarabu na kuongezeka satua na
ushawishi wa Iran nchini Yemen. Kwa sababu hiyo nchi wanachama wa PGCC
zimetoa wito katika kikao chao cha 35 wa kutaka makubaliano ya Septemba
yabatilishwe na wapiganaji wa Ansarullah waondoke katika mji mkuu wa
Yemen na katika maeneo mengine wanayoyadhibiti. Baadhi ya viongozi wa
harakati ya Ansarullah akiwemo Ali al Bukhaiti, mjumbe wa baraza la
kisiasa na Hussein al Azi, mkuu wa mahusiano ya nje katika ofisi ya
kisiasa ya harakati hiyo wamepinga azimio au taarifa yoyote ya kuingilia
masuala ya ndani ya Yemen na kusisitiza kwamba taarifa ya Baraza la
Ushirikiano la Ghuba ya Uajemi ni ya uingiliaji, ni tusi kwa wananchi wa
Yemen na ni njama ya kushadidisha hitilafu za kimatapo na kimadhehebu
katika nchi hiyo…/
No comments:
Post a Comment