Unordered List


Blogger Tips and TricksLatest Tips And TricksBlogger Tricks

Friday, 19 December 2014

Muswada wa sheria ya usalama wapitishwa Kenya

Muswada wenye utata wa marekebisho ya sheria ya usalama umepitishwa bungeni nchini Kenya baada ya mijadala na malumbano ya mchana kutwa kati ya wabunge wa serikali na wale wa upinzani. Kikao maalumu cha bunge cha kujadili marekebisho ya sheria ya usalama kilivurugika mara kadhaa leo Alhamisi baada ya wabunge wa upinzani kuzusha rabsha ndani ya bunge na kutatiza kabisa shughuli za taasisi hiyo. Spika wa bunge la Kenya, Justin Muturi, alifanya juhudi kubwa za kuwatuliza wapinzani na hata kuahirisha kwa muda kikao hicho lakini kila wakati wabunge waliporudi ukumbini, fujo zilianza tena. Upinzani umelalamikia kupitishwa muswada huo ingawa kumekuweko na marekabisho kadhaa kwenye vipengee vilivyokuwa na utata.
Muungano wa upinzani wa CORD unapinga marekebisho ya sheria mpya ya usalama kwa madai kwamba mabadiliko hayo yatairudisha Kenya katika enzi za udikteta na utawala wa kipolisi. Mabadiliko hayo pia yamepingwa na makundi ya kiraia na yale ya kutetea haki za binadamu kwa madai kuwa yatatoa mwanya kwa vyombo vya usalama kukiuka haki za binadamu. Serikali imesema sheria hiyo ndiyo wenzo pekee unaweza kuisaidia kukabiliana na hali ya ukosefu wa usalama katika nchi hiyo ya Afrika Mashariki.
Katika hatua nyingine, bunge la Kenya limemuidhinisha Waziri mpya wa Mambo ya Ndani, Joseph Nkaissery, ambaye aliteuliwa na Rais Uhuru Kenyatta juma lililopita. Wabunge wa serikali na wale wa upinzani wamemuidhinisha Nkaissery ambaye sasa ataidhinishwa rasmi na Rais kabla ya kuapishwa. Nkaissery anachukua nafasi ya mtangulizi wake aliyefutwa kazi, Joseph Ole Lenku

No comments:

Post a Comment