Mashirika ya kigeni pamoja na nchi
wafadhili wa Tanzania zimemtaka Rais Jakaya Mrisho Kikwete wa nchi hiyo
kuwachukulia hatua maafisa waandamizi wa serikali waliotajwa kuhusika na
kashfa ya wizi ya Escrow.
Baadhi ya nchi zimetishia kusitisha
misaada yao kwa Tanzania hadi pale kadhia hiyo itakapotatuliwa na
wahusika kuwajibishwa. Marekani ambayo ni moja ya nchi wafadhili
imetahadharisha kuwa itazuia msaada wa dola milioni 700 ambazo ni sawa
na shilingi trilioni 1.1 za Tanzania kutokana na kashfa ya Tegeta
Escrow.
Marekani imesema, mkataba wa pili wa
miradi inayofadhiliwa na shirika la nchi hiyo la Changamoto za Milenia
(MCC) utategemea hatua zitakazochukuliwa na serikali ya Tanzania dhidi
ya wahusika wa kashfa hiyo.
Hayo yanajiri wakati Rais Jakaya Kikwete
akisubiriwa kutoa maamuzi ya mapendekezo yaliyofikiwa na Bunge
kuhusiana na sakata la wizi wa fedha zaidi ya Sh. bilioni 300 kutoka
akaunti ya Tegeta Escrow wiki ijayo.
Baadhi ya nchi za Ulaya pia zimemtaka
Rais Kikwete kuchukua hatua za haraka dhidi ya wahusika wa kashfa hiyo
ya ufisadi la sivyo misaada kwa Tanzania itasimamishwa.
No comments:
Post a Comment