Matokeo ya Uchaguzi wa Serikali za
Mitaa uliofanyika juzi nchini Tanzania yanaonyesha kuimarika upinzani
nchini humo baada ya kupata viti vingi vya uenyekiti wa mitaa na vijiji,
pamoja na mamia ya wajumbe wa Serikali hizo.
Hayo yanaonyesha kuwa vyama hivyo
vimeanza kuimarika katika ngazi za chini, tofauti na ilivyokuwa mwaka
2009, katika uchaguzi ambao CCM kilipata ushindi wa kishindo wa asilimia
91.72, huku wapinzani wakigawana asilimia 8.28 zilizobaki.
Licha ya uchaguzi huo wa juzi kugubikwa
na kasoro nyingi, upinzani umeonekana kuchomoza huku katika baadhi ya
mikoa ukipata ushindi maradufu hasa katika maeneo ambayo una nguvu kubwa
wakati katika maeneo ambayo ulikuwa na viti vichache au kutokuwa navyo
kabisa, umeibuka na kuipokonya CCM baadhi ya mitaa na vijiji.
Vyama vinavyounda Umoja wa Katiba ya
Wananchi (Ukawa) yaani Chadema, CUF na NCCR-Mageuzi vimejizolea viti
vingi tofauti na awali, huku chama kipya cha ACT kikichomoza na kupata
ushindi katika maeneo kadhaa ya mikoa ya Kigoma na Katavi.
Mikoa ambayo upinzani umeonekana kuzoa
viti vingi ni Arusha, Kilimanjaro, Mbeya, Iringa, Kigoma, Mara, Kagera
na Dar es Salaam, hali ambayo wachunguzi wa mambo wameielezea kuwa siyo
dalili njema kwa CCM.
No comments:
Post a Comment