Serikali ya Tanzani iliwahi kutoa mwongozo wa mawasiliano yote
ya wafanyakazi wa Serikali na idara zake hasa yaliyohusu baruapepe, simu
na vifaa vingine vya Serikali.
Hata hivyo, agizo hili siku zote limekuwa
likipuuzwa. Kwa mfano, ukisoma taarifa mbalimbali za baadhi ya taasisi
nyeti za Serikali zinazokwenda kwa umma, utashangaa kukuta kuna anuani
za baruapepe za Google au Yahoo.
Kama haitoshi, idara nyingine za Serikali pia
zinatumia mawasiliano ya Yahoo au mengine ambayo si ya Serikali ya
Tanzania. Nina wasiwasi huenda anuani hizi zinatumika hata katika
nyaraka nyeti kama mikataba.
Siku za karibuni, watendaji hawahawa wa Serikali
walitoa mpya kwa kutupatia Watanzania namba ya simu ya Rais Jakaya
Kikwete kwa lengo la kutaka kumjulia hali alipokuwa katika matibabu
nchini Marekani.
Namba iliyotolewa kwa ajili ya kutuma ujumbe wa
kumtakia heri Rais ilikuwa +1-646-309-2295. Hii ni namba ya Marekani si
namba ya Tanzania, kwa hiyo mtu akituma ujumbe wake unahifadhiwa kwenye
hifadhi fulani huko Marekani hata kama huku nyumbani nako pia
itahifadhiwa na kampuni husika.
Taarifa zinasema zaidi ya watu milioni 10 walituma
ujumbe mfupi kwenye namba hiyo kwa ajili kumpa pole Rais na salamu
nyingine alipokuwa hospitalini na hata baada ya kutoka.
Bila shaka wengine kwa mapenzi waliyonayo kwa Rais
wao walituma ujumbe zaidi ya mara moja tangu siku namba hiyo ilipowekwa
hadharani na wasaidizi wa Rais.
Kama watu milioni 10 au zaidi walituma ujumbe
kwenye namba ya Marekani, ina maana kuna kampuni moja huko Marekani hivi
sasa imehifadhi namba za Watanzania milioni 10 au zaidi, tena bila tabu
na bila makubaliano yoyote na watu husika, yaani watumiaji wa namba
hizo.
Hatuna budi kuelewa kuwa Idara ya Usalama wa Taifa
ya Marekani (NSA) na shirika lao la ujasusi (CIA) ni watuhumiwa wakuu
wa kudukua taarifa za mawasiliano ya watu ndani ya nchi yao wenyewe na
hata nje.
Najiuliza wataalamu wetu hawakuliona hili mpaka waache mamilioni ya namba za Watanzania zikusanywe?
Kwa nini watendaji wa Ikulu walitoa namba ya nje
tena Marekani ambayo ni mtuhumiwa wa udukuzi, wakati tuna kampuni ya
simu yenye alama ya utaifa wetu, yaani TTCL?
Bila shaka kampuni hii ingeweza kutoa namba za
simu na huduma nyingine za mawasiliano, kwa ajili ya shughuli hiyo na
namba zikahifadhiwa na wao wenyewe TTCL na si mataifa mengine au kampuni
nyingine ya nje.
Hata kama hatuitaki TTCL kuna kampuni za mawasiliano kama Tigo,
Airtel, Zantel, Vodacom, Smart Bol na huduma nyingi za mawasiliano
nchini ambazo zinaweza kutoa namba ya simu na kutumika popote duniani.
Mbona viongozi wengi wa nchi hii wanasafiri sehemu
mbalimbali duniani na huko wanatumia namba za simu za nyumbani kwa
ajili ya mawasiliano?
Sielewi nini kilitokea mpaka wahusika katika ofisi
ya Rais na vyombo vingine vya usalama walishindwa kung’amua mapema
udhaifu huu wa kimawasiliano?
Hili suala halikubaliki hasa likiwa limemhusisha
kiongozi mkuu wa nchi. Siyo siri kuna watu katika hili wamefanya uzembe
wa hali ya juu, hivyo nashauri hatua kali zichukuliwe ili iwe funzo kwa
wengine.
No comments:
Post a Comment