Mashirika ya Kimataifa ya Kutoa
Misaada ya Kibinadamu yanatafuta dola milioni 810 kwa ajili ya
kuwasaidia wakimbizi wa Sudan Kusini ifikapo mwakani. Mkuu wa Shirika la
Kuwahudumia Wakimbizi la Umoja wa Mataifa UNHCR ametahadharisha kwamba,
iwapo mapigano hayatasimamishwa nchini Sudan Kusini na kufikiwa
makubaliano ya amani, kuna uwezekano mkubwa wa kuongezeka idadi ya
wakimbizi wa nchi hiyo kwenye kambi za wakimbizi zilizoko nchi jirani na
kufikia idadi ya wakimbizi laki nane na elfu ishirini na moja. Mkuu wa
Shirika la Kuwahudumia Wakimbizi la Umoja wa Mataifa UNHCR amezitaka
nchi jirani na Sudan Kusini kushirikiana na shirika hilo la kimataifa
kwa lengo la kuhifadhiwa usalama na maisha ya wakimbizi walioko kambini.
Taarifa zinasema kuwa, wakimbizi wasiopungua elfu tisini na saba
wanakabiliwa na hali mbaya kwenye kambi za Umoja wa Mataifa zilizoko
nchini Sudan Kusini 'UNMISS'. Wakati huohuo, Amina Mohamed Waziri wa
Mambo ya Nchi za Nje na Biashara ya Kimataifa wa Kenya amewataka
wafadhili wa kimataifa kutoa misaada yao ya kifedha kwa ajili ya kuzuia
kujitokeza mgogoro wa kibinadamu nchini humo. Waziri Amina Mohamed
amesisitizia udharura wa kukomeshwa mapigano na kurejeshwa amani na
utulivu nchini Sudan Kusini.
No comments:
Post a Comment