Mkuu mpya wa Sera za Kigeni wa Umoja
wa Ulaya amesisitiza juu ya udharura wa kufanyika uchunguzi wa haraka
na huru kuhusiana na sababu ya kufa shahidi Ziad Abu Ein, Waziri Asiye
na Wizara Maalumu wa Palestina. Federica Mogherini amebainisha kwamba,
kuna haja ya kufanyika uchunguzi kuhusiana na sababu ya kifo cha waziri
huyo. Aidha Mkuu wa Sera za Kigeni wa Umoja wa Ulaya amesema kuna
udharura kwa jamii ya kimataifa kuingilia kati kuhusiana na kile
kinachojiri katika ardhi za Palestina zinazokaliwa kwa mabavu. Wakati
huo huo, Ban Ki-Moon Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa naye ameutaka
utawala wa Kizayuni wa Israel ufanye uchunguzi kuhusiana na sababu ya
kufa shahidi waziri huyo wa Palestina. Ikumbukwe kuwa, jana wanajeshi wa
utawala wa Kizayuni wa Israel walimuua shahidi Ziad Abu Ein, Waziri
Asiye na Wizara Maalumu wa Palestina, kwenye vurugu zilizotokea kati ya
askari wa Israel na wananchi wa Palestina katika kitongoji cha Turmus
Ayya. Taarifa zinasema kuwa, wanajeshi wa Israel walianza kuwafyatulia
gesi ya kutoa machozi Wapalestina waliokuwa wakipanda mizaituni
kulalamikia ujenzi wa ukuta wa kidhalimu wa Israel katika eneo la Turmus
Ayya lililoko kaskazini mwa Ramallah. Ziad Abu Ein ambaye alikuwemo
kwenye maandamano ya Wapalestina ya kupinga ujenzi wa ukuta huo alipigwa
na kitu kizito kichwani na kupoteza fahamu, na juhudi za kuokoa maisha
yake zilishindikana kutokana na kuzidiwa na gesi.
No comments:
Post a Comment