Kwa ufupi
Nane; Anayetambua na kuthamini jitihada za wengine.
Kutambua jitihada za unaowaongoza na kuwapongeza ni jambo muhimu kwa
kiongozi yeyote hasa wa jumuiya ya shule.
Uongozi ni kuvuka mipaka ya mazoea na kuanzisha
michakato ya mabadiliko ya kimapinduzi inayowaelekeza watu kufikia
malengo kwa tija na ufanisi mkubwa.
Ni dhana na taaluma inayompa mhusika madaraka na
uwezo wa kuwawezesha wale wanaongozwa kuunganisha nguvu, stadi na vipaji
vyao na kuvitumia ili kufikia malengo yao.
Uongozi ni mchakato wa kuonyesha maana ya kile watu wanafanya kwa pamoja ili watu waelewe na kujituma zaidi kufikia malengo.
Wiki iliyopita tulichambua baadhi ya sifa sita za kiongozi bora. Leo tunaendelea.
Saba; Jasiri wa kufanya uamuzi sahihi, wenye tija
na kusimamia utekelezaji. Awe na utayari wa kutekeleza wajibu wake
pasipo kuyumbishwa wala kuogopa vitisho vya watu, hasa anapojua kwamba
anachofanya kipo sahihi kisheria na kimebeba maslahi ya umma mpana.
Hii inahusisha kuwa tayari kuhatarisha maisha yake
kwa ajili ya watu wake. Viongozi kama hawa kwa sasa ni wachache. Mtu
asiye na ujasiri wa kufanya amuzi sahihi huyu hafai kuwa kiongozi wa
kisiasa au wa kitaaluma.
Nane; Anayetambua na kuthamini jitihada za
wengine. Kutambua jitihada za unaowaongoza na kuwapongeza ni jambo
muhimu kwa kiongozi yeyote hasa wa jumuiya ya shule.
Walimu wanaofanya kazi kwa jitihada kubwa na
kujituma wanapaswa kutambuliwa, kuthaminiwa, kutiwa moyo na kupongezwa.
Vivyo hivyo, wanafunzi wenye jitihada kubwa na wanaojituma kusoma kwa
bidii wanapaswa kutambuliwa, kutiwa moyo na kupongezwa.
Kwa bahati mbaya shule zetu nyingi zinatambua
jitihada za wanafunzi, lakini zimewasahau walimu wenye jitihada kubwa na
wanaojituma kufikia malengo. Kiongozi makini anapaswa kufahamu hili na
kulitekeleza kikamilifu.
Tisa; Mwenye maarifa na anayependa kujifunza
zaidi. Kila siku maarifa mapya na teknolojia mpya inaibuka duniani.
Kiongozi bora ni yule anayechangamkia fursa ya kujifunza.
Anachangamkia kupata maarifa zaidi kwenye kazi
zake za uongozi, kwenye sera na mipango ya nchi, kwenye mikakati ya
kitaifa na masuala nyeti ya kitaifa yanayomhusu. Kuwa na maarifa kuna
faida kubwa katika jukumu la uongozi.
No comments:
Post a Comment