Haki hii huwa katika masuala ya kaziza fani mbali mbali, nafasi za uongozi na hata katika mambo ya michezo na burdani.
Lakini hapa Tanzania na hasa Zanzibar mara nyingi siasa huwa ndicho kipimo kikubwa cha mtu kupewa dhamana na kiwango cha elimu au upeo wake wa kulielewa suala analotakiwa kulishughulikia kwa uadilifu halizingatiwi.
Wakati mwengine elimu inayohitajika kwa kazi hiyo hupuuzwa kabisa kama vile haiwezi kusaidia kuleta ufanisi.
Hili tumeliona hata katika Bunge la Katiba liliomalizika Dodoma hivi karibuni ambapo kiwango cha elimu kwa wale wanaotaka nafasi za uongozi siku zijazo kuonekana hata na hao tunaowaita wasomi kuwa sio muhimu na badala yake imependekezwa uwezo wa kusoma na kuandika uatosha kwa mtu kuwa mbunge. Haya ni maajabu makubwa.
Katika miaka michache iliyopita, Zanzibar ilitia fora katika kudharau elimu. Matokeo yake kulikuwepo mahakimu katika zile zilizoitwa “mahakama za wananchi” na baadhi ya wazee walikuwa mahakimu walikuwa hawajui hata kuandika a, b wala c.
Wengine walikuwa hawajui hata tafauti ya kesi ya uhalifu na ya madai. Watu hawa walipewa dhamana ya kufanya maamuzi makubwa ya kisheria na kuwa na mamlaka ya kusukuma watu gerezani waliowaona wanayo hatia ya kosa walilokabaliana nayo.
Wakati mwingine mtu alitiwa hatiani kwa sababu tu kama angelikuwa hana kosa asingelishitakiwa na mtuhumiwa kuambiwa mbona ni yeye ndiye aliyeshitakiwa na watu wengine wanaendelea nje ya mahakama na kazi zao za kwaida.
Kama mshitakiwa alionyesha kuwa mnyonge alipewa adhabu maalum ya kifungo kwa kosa la “kudharau” mahakama na yule aliyejitetea kwa nguvu pia aliadhiiwa kwa kuonyesha “jeuri” kwa mahakimu.
Pakitokea mtu kuzikusanya kumbukumbu za mahakama hii, panaweza kuandikwa kitabu cha kuchekesha na kusikitisha au kutengeneza filamu ya sinema ya kuchekesha.
Hata mkuu mmoja wa Jeshi la Wananchi wa Tanzania (TPDF) ukanda wa Zanzibar alikuwa hajui kusoma na kuandika. Kiongozi huyu, Brigedia Bakari Wakati, aliwahi kuchaguliwa kuwa Mjumbe wa Baraza la Wawakilishi.
Siku aliyoapishwa kuwa mwakilishi ndio ikawa aibu kubwa kwa vile alilazimika kula kiapo kwa karani wa Baraza kusoma maandishi na yeye kufuatilia na baada ya hapo ndio akaweka dole gumba badala ya saini katika hati ya kiapo.
Wapo tuliodhania zama zile hazitajirudia Visiwani, lakini ndio kwanza inaonekana mwenendo ule ni mzuri na unafaa kuendelezwa kwa maelezo ya “Mapinduzi Daima”.
Hivi karibuni uliwasilishwa katika Baraza la Wawakilishi muswaada wa sheria wa kuanzisha serikali za mitaa na kujadiliwa nafasi ya wawakilishi wa serikali katika mitaa na vijiji wajulikanao kama masheha.
Wengi wa hawa masheha wamekuwa wakilaumiwa sana na jamii na hata na wageni waliofuatilia mwenendo wa masuala ya ksiasa Zanzibar kuwa ndio wachangiaji wakubwa wa siasa za chuki na uhasama ziliokuwepo Visiwani miaka ya nyuma na saa zimeanza kujirudia.
Watu hawa, wengi wakiwa maofisa wastaafu wa vikosi vya ulinzi, wamekuwa wakifanya kazi zaidi kama wakereketwa wa CCM, badala ya kuwa wawakilishi wa serikali wenye wajibu wa kuitumikii jamii kwa misingi ya haki na usawa kwa kufuata sheria.
Wakati wa kujadili sifa zinazohitajka kwa masheha Wawakilishi wengi wa CCM, kama walivyofanya katika Bunge la Katiba, hawakujali elimu na kudai umuhimu ni kwa mtu anayechaguliwa kushika nafasi hiyo kujua kusoma na kuandika.
Wapo Wawakilishi, tena bila ya kuona haya wala kuelewa ni vibaya, walidai ati Zanzibar ya leo haina wasomi wengi wa kidato cha nne wenye umri wa zaidi ya miaka 40 na kwa hivyo pakiwekwa kiwango hicho cha elimu patakosekana watu wanaofaa kuwa masheha.
Huu ni unafiki na uzandiki wa hali ya juu ambao hauna lengo jingine isipokuwa ajenda ya siri ya kutaka kuendelea kuwa na wazee ambao sio wasomi kushika nafasi za masheha na kuendelea kuwaburuza wananchi kwa utashi wa kisiasa.
Kwa kweli inasikitisha, lakini ukichunguza utaona hiki ni kielelezo kingine cha Zanzibar kutokuwa tayari mpaka sasa kufanya mabadiliko ya kuwa na utawala bora.
Kwa vyovyote vile ndoto ya utawala bora haiwezi kutimia na itabakia kuwa ndoto kama viongozi wa kijamii watakuwa ni watu ambao hawana kiwango kizuri cha elimu.
Ni vizuri kwa serikali kwenda na wakati na kuona umuhimu wa elimu iwe katika siasa, mambo ya utawala na hata michezo.
Kudharau au kuwekea vizingiti elimu ni sawa na kufunga milango ya nchi kujipati maendeleo. Lakini lililo baya zaidi ni kuendelea kuwa na masheha wenye elimu duni ni kutoa mwanya wa kuendeleza siasa za chuki na uhasama Visiwani.
Hapa ningependa kukumbusha baadhi ya vituko vya hawa masheha. Kwa mfano baadhi ya masheha kwa jinsi walivyokuwa wanapenda kuvuruga mambo na kutojali haki za raia wala sheria wamefika hadi kukataa kuwajua watoto waliowazaa, watu waliowaozesha binti zao na majirani zao wa miaka nenda miaka rudi.
Sababu ya kufanya hivi ni kuhakikisha kuwa hawaandikishwi kuwa wapiga kura kwa vile wanawaona ni wapinzani na hawatoipigia kura CCM.
Sheha wa Mtoni, mjini Unguja, bila ya aibu alikuwa na ujasiri wa kusema hamjui mtu anayeitwa Maalim Seif Sharrif Hamad, ambaye ni jirani yake na kwa hivyo Maalim Seif ambaye alikuwa ni mgombea urais kwa tiketi ya Chama cha Wananchi (CUF) hakustahili kuandikishwa kupiga kura.
Hivyo, kweli anapotokea sheha kama huyu tuelewe nini na la kushangaza hakufukuzwa kazi kwa vile alifanya kazi yake kwa umakini na uadilifu. Bila ya kutafuna maneno naona ni kutokana na mwenendo huu ndipo wanapotokea wahuni ambao nao pia wakiwa watu ambao hawajali sheria kufanya ujahili uliovuka mipaka wa kulipiza kisasi wa kuwamwagia tindikali baadhi ya masheha.
Kama Zanzibar inataka maendeleo ya kweli na watu wake kuishi kwa maelewano na kushirikiana ni muhimu kufanya mageuzi makubwa juu ya uteuzi wa masheha. Moja ya eneo ambalo halifai kupuuzwa ni kiwango cha elimu cha mtu anayetaka kuchaguliwa kuwa sheha.
Huu mwenendo wa kuangalia zaidi utashi wa kisiasa wa mtu kama kigezo muhimu kwa kuchaguliwa kuwa sheha hauna mustakbali mzuri na Zanzibar na uzoefu unaafaa kutumika kama umetoa mafunzo ya kutosha.
Unapodharau elimu ni sawa na kusema hutaki maenedeleo ya jamii wala nchi na kama kweli Zanzibar inataka kujipatia maendeleo ni lazima kufanya mabadliko katika uteuzi wa masheha.
Makosa yamefanyika siku za nyuma na ni vizuri kuyarekebisha na sio kuyanedeleza. Tuache utashi wa kisiasa na tuweke maslahi ya nchi mbele. Mambo ya siasa ni ya kupita na ipo siku yatakuwa sehemu ya hitoria ya Zanzibar, lakini visiwa vya Unguja na Pemba vitanedelea kuwepo na kitachobadilika ni watu wake kutokana na vizazi na vifo.
Tumeona hali inavyokuwa katika nchi nyingi zinazokataa mabadliko. Tutumie mambo yaliyotokea katika nchi hizo, zikiwemo za majirani zetu, kujifunza ili tujiepushe na balaa tunaloweza kuja kujijutia na kubaki kujilaumu na kulaumiana kwamba tulishindwa au kukataa kuisoma hali halisi ya nchi.
Mageuzi hayazuiliki, iwe kwa kutumia hadaa, sheria mbaya au mabavu. Kinachoweza kufanyika ni kukawilisha mageuzi kuwafikia. Tubadilike haraka kabla ya wakati haujaamua kutubadilisha.
No comments:
Post a Comment