Khatibu wa muda wa Sala ya Ijumaa hapa mjini Tehran amesema leo
kuwa, ripoti iliyotolewa wiki hii na Baraza la Seneti nchini Marekani ni
ya kushtua. Ripoti hiyo imefichua jinsi Shirika la Ujasusi la Marekani
(CIA) lilivyowatesa kinyama washukiwa wa ugaidi katika jela la
Guantanamo miaka kadhaa iliyopita. Ayatullah Ahmad Khatami amesema
mateso hayo ya CIA dhidi ya washukiwa wa ugaidi ni unyama na ukiukaji
mkubwa wa haki za binadamu. Ayatullah Khatami amesema inasikitisha kuona
Marekani ikijigamba kuwa inatetea haki za binadamu duniani ilihali nchi
hiyo ndiyo mkiukaji nambari moja wa haki hizo. Khatibu wa Sala ya
Ijumaa hapa Tehran pia amelaani mauaji ya Waziri wa Palestina, Ziad Abu
Ein aliyeuawa shahidi siku ya Jumatano na jeshi la utawala wa Kizayuni
wa Israel. Ayatullah Ahmad Khatami amesema serikali ya Umoja wa Kitaifa
ya Palestina inapaswa kuchukua hatua kali dhidi ya Israel kufuatia jinai
hiyo. Amesema kwa mara nyingine tena Wazayuni wameonyesha udhalimu na
unyama wao hadharani na kusisitiza kuwa muqawama na mapambano ya
Wapalestina ndiyo njia pekee ya kumshinda adui mzayuni.
No comments:
Post a Comment