Unordered List


Blogger Tips and TricksLatest Tips And TricksBlogger Tricks

Friday, 12 December 2014

Msimamo wa Iran kuhusu silaha za mauaji ya umati katika mkutano wa Vienna

Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ikiwa miongoni mwa wahanga wa silaha za mauaji ya umati, inaamini kuwa kumiliki silaha hizo hakudhamini usalama wa nchi yoyote ile. Hayo yameelezwa na Reza Najafi, mwakilishi wa Iran katika Wakala wa Kimataifa wa Nishati ya Atomiki (IAEA), kwenye mkutano wa kimataifa wa Vienna uliojadili taathira za kutumiwa silaha za nyuklia kwa binadamu. Amesisitiza kuwa, dhamana pekee ya kukabiliana na vitisho vya silaha hizo ni kutokomezwa kikamilifu chini ya udhibiti mkali wa kimataifa. Najafi ameongeza kuwa, tangu yalipojiri mashambulio ya Marekani dhidi ya watu wa Hiroshima na Nagasaki huko Japan, mwanadamu amekuwa akiishi kwa hofu na woga wa silaha za nyuklia. Amesema, suala la baadhi ya nchi kumiliki silaha hizo halikubaliki na kwamba linapaswa kulaaniwa, kwani ni kinyume na Mkataba wa Kuzuia Uzalishaji na Usambazaji wa silaha za Nyuklia (NPT).
Kuwepo maelfu ya vichwa vya mabomu ya nyuklia na kuzalisha silaha za kisasa za aina hiyo kunahesabiwa kuwa tishio kwa mwanadamu. Katika eneo la Mashariki ya Kati pia Israel ambayo ni utawala pekee kwenye eneo hilo unaomiliki silaha za nyuklia, inahatarisha amani ya eneo hilo kwa kuwa na mabomu kati ya 200 hadi 400 ya nyuklia.
Kwa kuzingatia wasiwasi huo, nchi nyingi zikiwemo zile za Jumuiya ya Nchi Zisiyofungamana na Siasa za Upande Wowote (NAM) zinasisitiza kutekelezwa kikamilifu na bila ubaguzi mkataba wa NPT.
 Jamhuri ya Kiislamu ya Iran pia sambamba na kukaribisha jitihada za pande zote za kutokomezwa silaha za atomiki duniani kote tangu huko nyuma ilipendekeza kutokomeza silaha hizo katika Mashariki ya Kati, na kuunga mkono suala hilo. Vilevile Iran imetoa pendekezo la kufanyika kongamano la kuangamizwa silaha za nyuklia Mashariki ya Kati lakini Marekani imezuia kufanyika kongamano hilo.
Katika hotuba yake kwenye mkutano wa Vienna, mwakilishi wa kudumu wa Iran katika wakala wa IAEA ameashiria matamshi ya Kiongozi Muadhamu katika ufunguzi wa mkutano wa 16 wa viongozi wa NAM mjini Tehran Oktoba 30 mwaka 2012, ambapo alisema kuwa Jamhuri ya Kiislamu inaamini kwamba matumizi ya silaha za nyuklia, kemikali na nyinginezo kama hizo ni dhambi kubwa isiyosameheka.
 Ripoti zilizotolewa zinasema, inakadiriwa kuwa katika muongo ujao, gharama za kuzalisha silaha zaidi za nyuklia na mitambo inayohusiana na silaha hizo itafikia dola trilioni moja. Mkutano wa kimataifa wa Vienna  uliojadili taathira za silaha za nyuklia kwa binadamu pengine ni fursa nzuri ya kukumbusha kwa mara nyingine wasiwasi wa walimwengu kuhusu silaha hizo, lakini hatupaswi kusahau kuwa, kufanikishwa dhana ya kuwa na dunia isiyo na silaha za nyuklia kunapaswa kuanzia katika nchi ambazo zinaamini kwamba kuwa na silaha hizo kunazisaidia kiusalama.
Kwa msingi huo nchi zinazomiliki silaha hizo zinapaswa kuchukua hatua za mwanzo kuhusu suala hilo, la sivyo jitihada au mikataba na makubaliano yanayofanyika kuhusu suala hilo hayatakuwa na natija yeyote. Kama sera za kijeshi na kiusalama za nchi zinazomiliki silaha za atomiki zitaendelea kutegemea mlingano wa nguvu wa silaha za nyuklia, itakuwa vigumu kuchukuliwa hatua za maana katika uwanja huo.
Ni kwa msingi huo ndiyo maana mwakilishi wa Iran katika wakala wa IAEA amezitaka nchi zinazomiliki silaha za nyuklia kutekeleza majukumu yao kwa mujibu wa mkataba wa N.P.T na kuacha kuzidisha silaha hizo, kuzalisha vizazi vipya au kupeleka silaha hizo katika nchi nyingine.

No comments:

Post a Comment