Umoja wa Mataifa ulitangaza jana kuwa, mapambano dhidi ya makundi
ya wanamgambo waasi na yale yanayosababisha ghasia na machafuko
yatachukua muda mrefu huko mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya
Kongo. Hivi sasa, viongozi wa serikali ya Kongo pamoja na wale wa Umoja
wa Mataifa wanalinyooshea kidole cha lawama kundi la waasi wa ADF NALU
wa nchini Uganda kwa kusababisha ukosefu wa amani na utulivu nchini
Kongo. Hayo yanajiri katika hali ambayo, Martin Kobler, Mkuu wa
Operesheni za kikosi cha Umoja wa Mataifa nchini Kongo MONUSCO
hajatangaza kinagaubaga kama kundi la ADF NALU limehusika na machafuko
yanayoendelea mashariki mwa nchi hiyo. Imeelezwa kuwa, waathiriwa wa
mashambulio ya waasi yaliyoanza mwezi Oktoba hadi sasa katika mji wa
Beni ulioko katika jimbo la Kivu Kaskazini, mashariki mwa Kongo imefikia
watu 250. Waasi wa ADF wamejikita mashariki mwa Kongo tokea mwaka 1995.
Baadhi ya ripoti zinaeleza kuwa kundi hilo la waasi wa Uganda
lilihusika na mauaji ya watu wasiopungua 13 yaliyofanywa siku za
Jumamosi na Jumapili iliyopita huko mashariki mwa Kongo. Kabla ya hapo,
Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa lilipitisha azimio
lililopendekezwa na Ufaransa na Uingereza la kuitaka serikali ya Kongo
iwatimue waasi walioko mashariki mwa nchi hiyo. Kuhusiana na kadhia
hiyo, wanachama wa kudumu na wasio wa kudumu wa baraza hilo walitoa
taarifa ya kuunga mkono kuwepo hali ya utulivu na amani nchini humo, na
kusisitiza suala la kupokonywa silaha waasi hao. Hata hivyo, ADF NALU
sio kundi pekee la waasi linalosababisha ukosefu wa amani na utulivu
katika eneo la mashariki mwa Kongo, kwani licha ya waasi hao wa Uganda,
kundi jingine la waasi wa Kihutu la Democratic Forces for the Liberation
of Rwanda 'FDLR' la nchini Rwanda linalovuruga amani na utulivu nchini
Kongo. Makundi hayo yamekuwa yakiwatumia watoto kwenye medani za vita na
hata kuwadhalilisha kijinsia watoto na wanawake katika nchi hiyo.
Wahutu wa Rwanda walikimbilia nchini Kongo kwenye muongo wa 1990 na
kuunda kundi la waasi, na imeelezwa kuwa, idadi kubwa ya wanamgambo wa
kundi hilo ni watu waliohusika na mauaji ya kimbari ya mwaka 1994 nchini
Rwanda. Hii ni katika hali ambayo, wataalamu wengi wanaamini kwamba,
propaganda kubwa zinazofanywa na madola ya Magharibi kuwa zinashirikiana
na Kongo kwa lengo la kurejesha amani na utulivu nchini humo, ni
mchezo wa kisiasa tu na wala nchi hizo hazina azma thabiti ya kurejesha
amani katika eneo la mashariki mwa Kongo. Kwa hakika viongozi wa
Magharibi, wao wenyewe ndiyo wasababishaji wakuu wa machafuko na
mapigano barani Afrika na hasa nchini Kongo ili waweze kuendelea kubaki
kijeshi kwenye maeneo mbalimbali na kupora maliasili na utajiri wa nchi
hizo. Wadadisi wa mambo wanaeleza kuwa, mashirika ya kigeni yakiwa na
lengo la kupora maliasili na utajiri wa Kongo, yanataka machafuko na
mapigano yaendelee nchini humo. Nazo nchi za eneo la Maziwa Makuu ya
Afrika zinajaribu kulinda maslahi yao kwa kuendelea machafuko mashariki
mwa Kongo. Kabla ya hapo, Umoja wa Mataifa uliunda jopo la wataalamu la
kuchunguza mgogoro wa Kongo, na kutoa ripoti iliyokuwa ikizituhumu nchi
za Rwanda na Uganda kuwa zinawapatia silaha waasi, kuwachochea wanajeshi
wa serikali ya Kinshasa watoroke jeshini pamoja na kuwapatia waasi hao
msaada wa kiintelijinsia. Katika hali kama hiyo, hatua ya Umoja wa
Mataifa ya kutangaza kuendelea mapigano na mapambano dhidi ya makundi ya
waasi mashariki mwa Kongo, inaweza kuwa ni tahadhari na indhari ya
kukaririwa majanga ya kibinadamu katika eneo hilo.
No comments:
Post a Comment