Waziri wa serikali ya umoja wa kitaifa ya Palestina aliyeuawa
shahidi kwa kupigwa hapo jana na mwanajeshi wa utawala haramu wa Israel
amezikwa leo. Maelfu ya Wapalestina wakiongozwa na Rais Mahmoud Abbas
wamehudhuria maziko ya Ziad Abu Ein huku waombolezaji wakimtaka Abbas
achukue hatua kali dhidi ya utawala ghasibu wa Israel. Hapo jana
madaktari walioupasua mwili wa Abu Ein kwa ajili ya kuchunguza chanzo
cha kifo chake walisema kiongozi huyo alipoteza maisha baada ya kupata
majeraha shingoni pamoja na kuvuta gesi yenye sumu. Utawala wa Kizayuni
wa Israel umekataa kutambua ripoti ya madaktari licha ya kuwepo
mwakilishi wake kwenye shughuli za upasuaji wa mwili wa Waziri Ziad.
Utawala huo bandia umetoa taarifa ya upotoshaji na kusema Ziad Abu Ein
alifariki dunia kutokana na mshituko wa moyo. Picha za video
zinazoonyesha jinsi mwanajeshi mzayuni alivyomkaba koo waziri huyo wa
Palestina zimesambaa katika mitandao ya kijamii na hivyo kuamsha hasira
za ulimwengu kuhusiana na jinai hiyo ya Israel. Umoja wa Ulaya, Umoja wa
Mataifa pamoja na nchi mbalimbali za dunia zikiwemo Iran na Russia
zimelaani mauaji ya Waziri huyo na kutaka hatua kali zichukuliwe dhidi
ya wale waliohusika na unyama huo.
No comments:
Post a Comment