Dar es Salaam. Wakati Serikali ya Marekani ikisema haitatoa
fedha za Changamoto za Milenia (MCC) hadi utekelezaji wa maazimio ya
Bunge kuhusu ufisadi katika akaunti ya Tegeta Escrow wa Sh306 bilioni
utakapofanyiwa kazi, Ikulu imesema, Rais Jakaya Kikwete hatatekeleza
agizo hilo kwa shinikizo la msaada huo.
MCC ni taasisi ya Serikali ya Marekani inayotoa
misaada kwa nchi zinazoendelea. Shughuli za MCC zinajengwa katika msingi
kwamba msaada utaleta ufanisi na matokeo makubwa zaidi pale tu
unapoimarisha utawala bora, uhuru wa kiuchumi na uwekezaji katika watu
ambao unakuza uchumi na kuondoa umaskini.
Taarifa hiyo ilisema Bodi ya Wakurugenzi ya
Shirika la MCC kupitia taarifa yake kwa umma iliyotolewa jana na Ubalozi
wa Marekani nchini ilisema, katika mkutano wa bodi hiyo uliokutana
Desemba 10 mwaka huu nchini Marekani, ulielezea hofu na masikitiko
kuhusu hali ya rushwa inavyoendelea Tanzania.
Fedha ambazo Tanzania ilipaswa kupata kupitia
mradi huo wa MCC awamu ya pili ni Dola 450 milioni ambazo ni sawa na
Sh765 bilioni.
“Japokuwa bodi ilipiga kura ya kuiruhusu Tanzania
iendelee na maandalizi kwa ajili ya mkataba wa pili kwa dhati kabisa,
inaihimiza serikali ya Tanzania kuchukua hatua thabiti na mahsusi za
kukabiliana na rushwa kama sharti la msingi kwa bodi hiyo kufanya uamuzi
wa mwisho wa kuidhinisha mkataba huo.
“Bodi ilieleza kutambua umuhimu wa kusubiri na
kuona utekelezaji kamilifu wa tamko lililotolewa na Ikulu ya Tanzania
hapo Desemba 9 mwaka huu kwamba itachukua hatua za haraka na kutoa
uamuzi dhahiri na thabiti kuhusu maazimio ya Bunge juu la suala la
IPTL,” ilieleza taarifa hiyo.
Katika tamko hilo kwa umma, Balozi wa Marekani
nchini, Mark Childress alisema “Kupigwa hatua katika mapambano dhidi ya
rushwa ni muhimu sana kwa mkataba mpya kati ya MCC na Tanzania na katika
kuboresha mazingira ya ufanyaji biashara Tanzania.”
Aliongeza: “Tunatoa wito kwa serikali kuchukua
hatua za haraka kuhusu suala hili hasa kutokana na uzito wake katika
masuala muhimu kadhaa ya maendeleo,” ilisema taarifa hiyo.
Hali kadhalika, Bodi iligusia makubaliano kadhaa
yaliyofanyika na Tanzania iliahidi kufanya mageuzi ya kisera, kimuundo
na kitaasisi ili kuongeza ufanisi na uwazi katika taasisi zake na katika
sekta ya nishati.
Balozi Childress aliendelea kusema, “Tunafurahi
kwamba mchakato wa majadiliano ya maandalizi ya mkataba wa pili
utaendelea kwa miezi kadhaa ijayo. Tunapenda kusisitiza kuwa ni lazima
ahadi hizi zitekelezwe kabla Marekani haijafanya uamuzi wa mwisho kuhusu
mkataba wowote mpya na Tanzania.”
Katika mkutano huo, Tanzania ilikuwa miongoni mwa
nchi 10 zilizojadiliwa na Bodi ya MCC iliyokutana kuangalia kama nchi
hizi zimekidhi vigezo vya kuendelea na mchakato wa kuandaa mikataba
mipya.
Iwapo mkataba huo utapitishwa, utakuwa wa pili wa
MCC kwa Tanzania kati ya mwaka 2008 na 2013 ambao ulitekeleza mkataba wa
uwekezaji wenye thamani ya Dola za milioni 698 sawa na Sh1.18 trilioni
ambao uliowezesha utekelezaji wa miradi ya maji, barabara na nishati ya
umeme nchini kote Tanzania
Chini ya mkataba huo, mtandao wa nyaya za umeme wenye zaidi ya
kilomita 3,000 ulijengwa, jumla ya kilomita 450 za barabara pia
zilijengwa, kadhalika mitambo mikubwa miwili ya usafishaji maji na njia
ya kurukia ndege katika kiwanja kimoja cha ndege ilijengwa.
Kauli ya Ikulu
Katibu Mkuu Kiongozi, Balozi Ombeni Sefue alisema
hilo ni jambo la kawaida kwani ili uweze kupata msaada huo ni lazima uwe
umetimiza masharti na vigezo ambavyo miongoni ni masuala ya utawala
bora na rushwa.
“Kabla ya kutia saini wanaangalia masuala ya
utawala bora na rushwa na kama walivyosema wanasubiri kuona utekelezaji
wake ni jambo la kawaida duniani kutokea.”
Kuhusu Rais Jakaya Kikwete kuchukua hatua za
haraka dhidi ya waliohusika na sakata hilo, Balozi Sefue alisema, “MCC
ipo au haipo Rais (Kikwete) anachukulia suala hili kwa umakini na
atachukua uamuzi kwa misingi ya ushahidi uliotolewa.”
EIL yakazia
Wakala wa Uchunguzi wa Mazingira (EIA) wameitaka
MCC kutokubali kuidhinisha mkabata huo na Tanzania wa dola 450 milioni
hadi Rais Kikwete atakapochukua hatua stahiki dhidi ya vitendo vya
rushwa viliyotawala kwenye sakata la ujangili na usafirishwaji wa pembe
za ndovu kwenda nje ya nchi hususani China.
Taasisi hiyo inayojihusisha na masuala ya
mazingira ilitoa wito huo jana kwa Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani,
John Kerry na Mwenyekiti ambaye pia ni Mkurugenzi wa MCC, Diana Hyde
kwamba wasitishe hatua hiyo kwa Tanzania.
Kutokana na hilo, EIA imeomba MCC ambayo imekuwa
ikifadhili miradi ya maendeleo nchini kusitisha hatua hiyo kwanza hadi
Rais Kikwete atakapolivalia njuga suala hilo.
Novemba mwaka huu, EIA ilitoa ripoti ya utafiti wa
ujangili uliyoanika madudu dhidi ya mauaji ya tembo na namna meno
yanavyotoroshwa nchini.
Mvutano bungeni
Katiba Bunge la 16/17 lililomalizika mjini Dodoma
mwishoni mwa mwezi uliopita, Mbunge wa Ubungo (Chadema), John Mnyika na
Waziri wa Fedha, Saada Mkuya walivutana kuhusu ufadhili huo wa MCC
uliokwama kutokana na ufisadi wa akaunti ya Tegeta Escrow.
Wakati wabunge wakiomba kiti cha Spika kiruhusu kujadiliwa
bungeni kwa ripoti ya Kamati ya Hesabu za Serikali (PAC) kuhusu ufisadi
wa akaunti ya Tegeta Escrow, Mnyika alisimama na kusema, “kama ripoti
hii haitajadiliwa basi fedha zinazotolewa na MCC tutazikosa.”
Baada ya kauli hiyo, Mkuya alisimama na kusema,
“Si kweli kwamba tutazikosa fedha hizo kwani taratibu zinaendelea vizuri
na mkataba utasainiwa Desemba mwaka huu na fedha hizo zitatoka
Desemba.”
Kafulila
Mbunge wa Kigoma Kusini (NCCR-Mageuzi), David
Kafulila akizungumzia uamuzi huo wa bodi ya MCC alisema, “taarifa hiyo
imekuja wakati mwafaka...imenivisha nguo baada ya kuwa nimevuliwa
bungeni na kuitwa mimi mwongo.”
Alisema, “Nilisema bungeni kwamba hasara
tunayoipata kutokana na ufisadi huo wa Escrow ni zaidi kwani misaada
tuliyokuwa tunaisubiri ya Sh900 bilioni kutoka Ulaya, Marekani Dola
milioni 700 na ukijumuisha Sh306 bilioni ni zaidi ya Sh2 trilioni.”
Kafulila alisema fedha hizo zilikuwa zitoke tangu
Septemba mwaka huu kama ambavyo Ghana imezipata lakini kutokana na
uzembe wa Serikali ya Tanzania, imepoteza kiasi hicho cha fedha.
“Waziri wa fedha (Saada Mkuya) na Profesa Muhongo
(Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo) walikana bungeni
kwamba ninasema uwongo sasa ukweli umejulikana nani ni mkweli na nani
ni mwongo,” alisema Kafulila jana