Sunday, 14 June 2015
Misri yafungua tena kivuko cha mpakani cha Rafah
Serikali ya Misri leo imekifungua
tena kivuko cha Rafah kilichoko kwenye mpaka wa pamoja wa nchi hiyo na
Ukanda wa Gaza ili kuwaruhusu Wapalestina kuingia na kutoka katika eneo
hilo, ikiwa ni mara ya kwanza katika kipindi cha miezi mitatu, katika
kile kinachoonekana kama ishara ya kupungua mvutano uliokuwepo kati ya
Cairo na Harakati ya Muqawama wa Kiislamu ya Palestina HAMAS iliyoshika
hatamu za eneo la Gaza. Ukanda wa Gaza umewekewa mzingiro na utawala wa
Kizayuni wa Israel kwa zaidi ya mwaka wa saba sasa, na serikali ya Misri
imekuwa ikikifunga kivuko cha Rafah kwa muda mwingi tangu Rais Mohammad
Morsi aliyekuwa na uhusiano wa karibu na Hamas alipoondolewa madarakani
mwaka 2013. Wiki mbili zilizopita Cairo ilikifungua kituo cha Rafah kwa
muda wa siku tatu kuruhusu safari za upande mmoja tu kwa Wapalestina
waliokuwa wamekwama nje ya Ukanda wa Gaza kuweza kurejea makwao katika
eneo hilo. Lakini hatua ya leo ya kuruhusu kuingia na kutoka Gaza
kupitia kivuko cha Rafah inaonekana kama ishara ya kuboreka uhusiano wa
Misri na Hamas baada ya msuguano na mvutano mkali uliokuwepo kwa muda wa
miaka miwili. Serikali ya Cairo imeituhumu Hamas kuwa inayaunga mkono
makundi ya wanamgambo wenye silaha yanayopambana na serikali ya Misri
katika Rasi ya Sinai, tuhuma ambazo Hamas imezikadhibisha. Maafisa
katika mpaka wa Misri na Palestina inayokaliwa kwa mabavu wamesema
kivuko cha Rafah kitaendelea kuwa wazi kwa muda wa siku tatu, huku
baadhi ya duru za Palestina zikieleza kwamba muda huo unaweza kuongezwa;
hata hivyo hakuna kauli yoyote iliyotolewa na maafisa wa Misri
kuthibitisha suala hilo…
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment