Ripoti imefichuka kuhusu mikutano kadhaa ya siri baina ya
wawakilishi wa Saudi Arabia na Israel kwa lengo la kujadili misimamo yao
kuhusu Iran.
Kwa mujibu wa tovuti ya Bloomberg, mikutano hiyo imefanyika mara tano
katika kipindi cha miezi 17 iliyopita ambapo maafisa hao wa Saudia na
utawala haramu wa Israel wamekutana nyakati mbali mbali huko India,
Italia na Jamhuri ya Czech.
Tovuti hiyo imenukulu jenerali mstaafu katika jeshi la Israel
aliyeshiriki katika moja ya vikao hivyo akisema, "Tuligundua kuwa
tunakabiliana na matatizo na changamoto za pamoja na pia baadhi ya
majibu ya pamoja." Aidha siku ya Alkhamisi maafisa mashuhuri wa zamani
wa Saudia na Israel walikutana katika taasisi za Council on Foreign
Relations huko Washington. Kikao hicho kilihudhuriwa na Anwar Majed
Eshki, mshauri wa zamani wa serikali ya Saudia, na Dore Gold balozi wa
zamani wa Israel aliye karibu na Waziri Mkuu wa Utawala wa Kizayuni
Benjamin Netanyahu. Israel na Saudia zote kwa pamoja zinapinga kile
zinachosema ni kuenea ushawishi wa Iran katika eneo. Aidha pande mbili
hizo zimetangaza wazi kupinga mapatano ya nyuklia baina ya Iran na
madola sita makubwa duniani. Hivi karibuni pia gazeti moja la Uingereza
lilisema Israel imetangaza kuwa tayari kuipa Saudia makombora katika
vita vyake dhidi ya watu wa Yemen
No comments:
Post a Comment