Zoezi la upigaji kura linaendelea nchini Burundi na tayari
kumeripotiwa kutokea mashambulizi katika vituo kadhaa vya kupigia kura.
Wapiga kura wanaripotiwa kuwa wachache katika uchaguzi huo wa bunge
na serikali za mitaa huku watu wengi wakionekana kuhofia kujitokeza
katika vituo vya kupigia kura. Uchaguzi huo unafanyika pamoja na kuwa
jamii ya kimataifa imeitaka serikali ya Burundi kuuahirisha na kupanga
wakati mwingine unaokubalika na pande zote husika na chaguzi nchini
humo.
Wapinzani Burundi wametangaza kususia uchaguzi kwa madai kuwa si huru
na wa haki. Burundi ilitumbukia katika mgogoro mkubwa wa kisiasa
kuanzia mwezi Aprili wakati Rais Pierre Nkurunziza alipotangaza uamuzi
wake wa kugombea kiti cha urais kwa muhula wa tatu. Zaidi ya watu 70
wamepoteza maisha katika machafuko ya kabla ya uchaguzi Burundi huku
wengine zaidi ya laki moja wakikimbia nchi
Shirika la Ubunifu la Mediterranean limeonya juu ya hatari ya
kurejea magaidi katika eneo la Balkan kutoka katika nchi za Iraq na
Syria. Mtandao wa Intaneti wa al Alam umelinukuu shirika hilo likisema
hayo huko Sarajevo, Mji Mkuu wa Bosnia na kuongeza kuwa, hivi sasa kuna
raia 115 wa Bosnia ndani ya kundi la kigaidi la Daesh katika nchi za
Iraq na Syria. Kwa mujibu wa ripoti ya taasisi hiyo, eneo la Balkan
linakabiliwa na hatari ya vitendo vya kigaidi kama vinavyoendelea hivi
sasa huko Iraq na Syria kutokana na kurejea nyumbani raia wa nchi za
eneo hilo waliopigana kwenye makundi ya kigaidi katika nchi hizo mbili
za Kiarabu. Kwa mujibu wa shirika hilo, hatari hiyo inazikabili nchi
zote za eneo la Balkan na hata Russia kutokana na baadhi ya raia wa nchi
za Serbia, Albania, Macedonia na Montenegro kuwa na uhusiano wa karibu
na makundi ya kigaidi kama vile Daesh. Takwimu za idara ya mahakama ya
Bosnia zinaonesha kuwa karibu watu 192 wenye umri wa miaka 25 na vijana
wenye umri wa kati ya miaka 15 hadi 17 wametembelea maeneo yenye
mapigano huko Iraq na Syria kuanzia mwaka 2012 hadi mwishoni mwa mwaka
jana. Shirika hilo limeitaka polisi ya Bosnia kuongeza nguvu za
kudhibiti mitandao ya Intaneti na ya kijamii kwani ndiyo njia kuu
inayotumiwa kuwashawishi vijana hao kujiunga na makundi ya kigaidi.