Rais Jakaya Kikwete juzi alipiga marufuku vyama vya siasa na
asasi za kiraia kufanya kampeni za kuhamasisha wananchi kuhusu Katiba
Inayopendekezwa, akisema kufanya hivyo ni kuvunja Sheria ya Kura ya
Maoni kwa kuwa muda wake haujafika. Akihutubia mkutano wake na watu
wanaojipambanua kama ‘wazee wa Mkoa wa Dodoma’, Rais aliwahadharisha
wananchi wasikubali kile alichokiita kudanganywa na watu wasioitakia
mema nchi yetu.
Wakati Rais Kikwete akitoa kauli hiyo, siku hiyo
hiyo Rais Ali Mohamed Shein wa Zanzibar aliwataka viongozi wa vyama vya
siasa kuacha kile alichokiita kutumia vibaya mchakato wa Katiba
Inayopendekezwa kwa lengo la kuwagawa wananchi na kutishia amani na
utulivu uliopo nchini. Alikuwa akizungumza na wananchi na viongozi wa
CCM katika maadhimisho ya miaka minne ya kuwapo madarakani tangu
aliposhinda urais mwaka 2000. Alisema kumeanza kujitokeza viashiria vya
kuanza kuvuruga amani na utulivu uliopo hivi sasa kwa kisingizio cha
mchakato wa Katiba Inayopendekezwa.
Sisi hatuna ugomvi hata kidogo na kauli hizo za
viongozi hao, kwani ni wajibu wao kukemea au kutahadharisha wananchi
pale wanapodhani kuna umuhimu wa kufanya hivyo. Lakini tumeshangazwa na
hatua ya viongozi hao kufanya mambo ambayo ni tofauti na kauli zao za
kukemea kampeni. Katika mikutano yao mjini Dodoma na Zanzibar juzi,
viongozi hao walipiga kampeni kwa kutaka wananchi waunge mkono Katiba
Inayopendekezwa. Rais Shein alisema Katiba Inayopendekezwa ni mkombozi
wa wananchi wa Zanzibar na kudai imejibu hoja za malalamiko na kero za
Muungano. Mjini Dodoma, Rais Kikwete aliisifia Katiba Inayopendekezwa,
akisema uzuri wake hauhitaji kuambiwa na mtu kutokana na kuandikwa
vizuri na kwa lugha rahisi, huku akiilinganisha na timu ya mpira
iliyokamilika katika kila idara.
Hapa tumezungumzia tu kauli za kampeni walizozitoa
juzi katika hafla tofauti mjini Dodoma na Zanzibar. Lakini mtu yeyote
mwenye kumbukumbu nzuri atakumbuka kwamba viongozi hao, mawaziri na
viongozi wa chama chao cha CCM wamekuwa wakitoa kauli nyingi za kuipigia
kampeni Katiba hiyo inayopendekezwa. Tumeshuhudia wakifanya hivyo kila
wanapopata fursa za kufanya ziara za kiserikali ama za kichama. Katika
ziara zake wiki iliyopita katika mikoa ya Mwanza na Tabora, Rais Kikwete
alifanya kampeni hizo na kuwataka wananchi wapige kura ya ‘ndiyo’ kwa
Katiba hiyo inayopendekezwa, wakati Rais Shein alifanya hivyo mjini
Zanzibar katika mikutano ya hadhara wiki mbili zilizopita, akiwa
ameandamana na viongozi wa CCM na mawaziri waandamizi wa Serikali ya
Mapinduzi ya Zanzibar (SMZ).
Tumelazimika kutoa mifano hiyo kuonyesha kuwa,
wakati vyama vya upinzani na asasi za kiraia zikipigwa marufuku
kuwaeleza wananchi kuhusu maudhui yaliyomo katika Katiba Inayopendekezwa
pamoja na Rasimu ya iliyokuwa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, Ikulu ya
Zanzibar na ya Serikali ya Muungano kwa muda mrefu zimekuwa
zikijihusisha katika vitendo vya kupigia kampeni Katiba Inayopendekezwa.
Rasilimali na fedha nyingi za umma zinatumiwa
katika kufanikisha mkakati huo, ambao pia unawahusisha baadhi ya
wahariri na vyombo vya habari kadhaa. Tukio la mwishoni mwa wiki, ambapo
wafuasi wa CCM walivuruga mdahalo wa Katiba na kumpiga Jaji Joseph
Warioba wakati akiwasilisha mada kwenye mdahalo huo ni ujumbe tosha kwa
kila mmoja wetu
No comments:
Post a Comment