- Vigogo presha inapanda, inashuka
- Mjadala kutikisa Bunge wiki hii
RIPOTI ya uchunguzi ya Mdhibiti na
Mkaguzi Mkuu wa Serikali (CAG), kuhusu kashfa ya kuchota fedha zaidi ya sh
bilioni 200, kwenye Akaunti ya Tegeta Escrow zilizohifadhiwa katika Benki Kuu
ya Tanzania (BoT), umeanika madudu mazito yaliyofanywa na vigogo wa Serikali,
Tanzania Daima limedokezwa.
Ingawa ripoti hiyo ambayo Tanzania
Daima limebahatika kuiona, imekwepa kutaja majina ya vigogo hao na taasisi
wanazotoka, lakini inaonyesha kuwa jumla ya fedha za Escrow ni sh bilioni 306
ambazo ni matokeo ya Shirika la Umeme nchini (Tanesco), kulipishwa tozo la
uwekezaji zaidi ya kiwango kinachotakiwa kulipwa.
CAG katika ripoti hiyo, anasema
Tanesco walipaswa kurejeshewa sh bilioni 321 zilizolipwa ziada kwa IPTL kati ya
mwaka 2002 – 2012.
“Hivyo fedha za Escrow ni fedha za
umma, yote ilipaswa kurudi Tanesco na shirika kuendelea kuwadai IPTL sh bilioni
15,” alisema CAG.
Madudu mengine yaliyoibuliwa katika
ripoti hiyo ni kwamba, kampuni ya PAP haikununua kihalali hisa 70% za kampuni
ya Mechmar katika IPTL kwani zilizuiwa na Mahakama, hivyo hawana hati halisi za
hisa na PAP ilifanya udanganyifu katika malipo ya kodi kwa kutoa nyaraka za
uwongo na kuikosesha Serikali Mapato ya sh bilioni 8.7.
Inaeleza kuwa, kosa hili linahusu
pia mamlaka ya TRA Ilala, ambao walihusika kufanya mauzo hayo.
Akaunti ya kampuni ya VIP
Engineering and Management (VIPEM), ilifunguliwa na mmoja wa wabia wa IPTL,
James Rugemalira, ambaye alikuwa akimiliki asilimia 30 ya IPTL huku kampuni ya
Mechmar Bhd ya Malaysia ikiwa na hisa asilimia 70.
Kutokana na kiasi hicho cha hisa,
Rugemalira amelipwa kiasi cha dola milioni 75 (Shilingi Bilioni 123),
zikionyesha kwamba alilipwa kiasi cha dola milioni 7.5 (Shilingi bilioni 12.4)
mwaka jana na kiasi kilichosalia alimaliziwa mwaka huu.
Kiasi hicho cha fedha kililipwa kwa
Rugemalira na kampuni ya PAP inayomilikiwa na Harbinder Singh, ambaye kwa sasa
ndiye mmiliki pekee wa IPTL baada ya kununua hisa za Mechmar na zile za VIP.
Kwa mujibu wa ripoti hiyo ambayo
Gazeti hili imeinasa, Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali kwa kushirikiana na
Gavana wa Banki Kuu (BoT), na Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha, walivunja sheria
kwa kuelekeza kuwa kodi ya ongezeko la thamani kwenye tozo la uwekezaji
isilipwe na kusababisha serikali kupoteza mapato ya sh bilioni 21.
“Waziri kwa kushirikiana na Katibu
Mkuu Wizara ya Nishati na Madini, hawakufanya utafiti wa kini kuhusu uhalali wa
umiliki wa kampuni ya IPTL. Katibu Mkuu alisaini kutoa fedha za Escrow bila
kuhakikisha fedha za Tanesco zinarudi, hivyo kusababisha upotevu wa zaidi ya sh
bilioni 321,” inasema sehemu ya ripoti hiyo.
Kwa upande wa Tanesco, Mkurugenzi wa
Shirika hilo na Bodi yake, hawakutimiza wajibu wao kwa kugeuza maamuzi yao (ama
kwa kushinikizwa na Wizara au kwa rushwa), na kulikosesha shirika hilo zaidi ya
sh bilioni 321.
Wakati Waziri Mkuu Mizengo Pinda
akikaririwa bungeni kwamba fedha hizo sio za umma, ripoti hiyo inaonyesha kuwa
ni za umma.
Mgogoro uliosababisha fedha kuwekwa
katika akaunti hiyo ya Tegeta ya BoT, ulitokana na Tanesco kugoma kulipa
gharama za uwekaji mitambo (Capacity Charge), kwa IPTL mwaka 2006 kwa vile
ilibainika IPTL ilikuwa ikitoza gharama kubwa kuliko iliyopaswa.
Akaunti hiyo ya Tegeta, ilianzishwa
kwa sababu ya kuhifadhi fedha zote zilizopaswa kulipwa na Tanesco hadi hapo
mgogoro baina ya pande hizo mbili umalizike.
Hata hivyo, Septemba mwaka jana,
serikali kupitia Wizara ya Nishati na Madini, iliagiza BoT kulipa fedha hizo
kwa kampuni ya PAP mara baada ya kuridhishwa na uamuzi wa Mahakama Kuu uliosema
kwamba mgogoro baina ya wamiliki wa IPTL na Tanesco umemalizika na hivyo Benki
Kuu haina sababu ya kuhifadhi fedha hizo tena.
Uamuzi huo wa kulipwa, ulizua
upinzani mkali bungeni ambapo wabunge wawili wa kambi ya upinzani; Mbunge wa
Kigoma Kusini (NCCR-Mageuzi), David Kafulila na Mbunge wa Kigoma Kaskazini
(CHADEMA), Zitto Kabwe, walidai kuwa zoezi hilo limejaa ufisadi na Bunge
liliazimia kwamba suala hili lifanyiwe uchunguzi wa kina na Ofisi ya Mdhibiti
na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), pamoja na ile ya Taasisi ya Kuzuia
na Kupambana na Rushwa (Takukuru).
No comments:
Post a Comment