Serikali imewekeza katika siasa, imesahau wakulima
Hata hivyo, wakulima wamekwazwa na kodi nyingi wanazotozwa kwa kila
gunia inapotokea wakauza sehemu ya mahindi yao yaliyolundikana. Malipo
hayo ni kama kodi ya halmashauri, gharama za kuhifadhi mahindi ghalani,
ubebaji wakati wa kushusha mahindi kituoni, kuchekecha mahindi, kuondoa
uchafu na kupeleka kwenye mizani.
Kwa ufupi
Siyo siri kuwa, iwapo fedha inazotumia katika mambo ya kisiasa zingeelekezwa kwenye kilimo, wakulima wangejikomboa kiuchumi.
Zipo dalili nyingi zinazoonyesha kwamba kuna
uwezekano mkubwa nchi yetu ikakumbwa na janga kubwa la njaa mwakani.
Kinachoendelea hivi sasa ni wakulima katika mikoa inayolima mazao ya
chakula kwa wingi kukata tamaa kutokana na mazao yao kukosa soko, huku
wakulima hao wakijikuta katika ufukara wa kutisha kutokana na kuwekeza
fedha zao katika kilimo cha mazao hayo, lakini Serikali imeshindwa
kuwatafutia masoko.
Hapa hatuzungumzii mazao ya biashara kama korosho,
tumbaku, kahawa na pamba ambayo kwa muda mrefu sasa yamegeuka kuwa
laana kwa wakulima kutokana na viongozi wa vyama vya ushirika nchi nzima
kuvigeuza vyama hivyo kama mitaji binafsi ya kujitajirisha
wakishirikiana na baadhi ya viongozi serikalini.
Kwa miongo minne sasa wakulima hao hawana sauti
wala mtetezi. Serikali ingetarajiwa kuvikwamua vyama hivyo, ambavyo
vilianzishwa na wakulima wenyewe na kuwa nguzo yao kubwa kiuchumi. Hata
hivyo, hakuna asiyejua kwamba Serikali kwa kuogopa nguvu ya vyama hivyo,
iliingilia kati na kuvisambaratisha kwa kupandikiza uongozi uliowekwa
mfukoni na wanasiasa.
Hapa tunazungumzia wakulima wa mazao ya chakula,
hasa mahindi yanayolimwa kwa wingi katika mikoa ya Mbeya, Rukwa, Katavi,
Ruvuma, Iringa na Morogoro inayojulikana kama ‘Kapu la Chakula’. Hivi
sasa wakulima wa zao hilo wamekata tamaa kutokana na kukosa soko la zao
hilo, hivyo hawaoni tena sababu ya kuwekeza katika kilimo hicho kutokana
na hasara waliyoipata msimu uliopita, ambao walikopa fedha kuandaa
mashamba na kununua pembejeo na kufanikiwa kuvuna kiasi kikubwa cha
mahindi. Wakulima walihamasika kutokana na Rais Jakaya Kikwete kutangaza
bei mpya ya mahindi kutoka Sh350 hadi Sh500 alipokuwa katika ziara ya
mkoani Ruvuma mwaka uliopita.
Matokeo yake ni kwamba mahindi yanaozea katika
makazi ya watu, maghala ya vyama vya ushirika, Wakala wa Taifa wa
Hifadhi ya Chakula (NRFA) na wafanyabiashara binafsi. Wakulima wamebaki
wakiwa midomo wazi, wakisubiri kuona miujiza ya mahindi yao kupata soko
ili wajikwamue katika ufukara na umaskini uliopitiliza. Takwimu
zinaonyesha kwamba mikoa hiyo imezalisha tani milioni 16 za mahindi,
huku Mkoa wa Rukwa pekee ukizalisha tani milioni nne.
Hata hivyo, wakulima wamekwazwa na kodi nyingi
wanazotozwa kwa kila gunia inapotokea wakauza sehemu ya mahindi yao
yaliyolundikana. Malipo hayo ni kama kodi ya halmashauri, gharama za
kuhifadhi mahindi ghalani, ubebaji wakati wa kushusha mahindi kituoni,
kuchekecha mahindi, kuondoa uchafu na kupeleka kwenye mizani.
Kutokana na umuhimu wa sekta ya kilimo ambayo
inatoa ajira kwa zaidi ya asilimia 80 ya wananchi, tungetarajia Serikali
iwekeze nguvu na rasilimali zake kwenye kilimo. Mipango ya Kilimo
Kwanza na Matokeo Makubwa Sasa imeonekana kuwa ni nadharia zaidi kuliko
utekelezaji. Ni kutokana na hali hiyo tunaishauri Serikali iwekeze kwa
wakulima badala ya kuwekeza kwenye siasa. Siyo siri kuwa, iwapo fedha
inazotumia katika mambo ya kisiasa zingeelekezwa kwenye kilimo, wakulima
wangejikomboa kiuchumi.
Ni wakati wa Serikali sasa kufikiri nje ya
kisanduku kwa kuwatafutia wakulima masoko ya uhakika kwa mazao yao,
yakiwamo matunda kama nyanya, maembe, machungwa na nanasi yanayoozea
mashambani kwa kukosa viwanda vya kusindika. Kipaumbele kiwekwe kwa
wakulima na Serikali itambue kwamba wananchi hawawezi kupata shibe
kutokana na siasa.
No comments:
Post a Comment