KAMISHNA Jenerali wa Magereza nchini (CGP), John Minja, amesema kuwa jeshi hilo kwa sasa limeanza kuingia ubia na baadhi ya kampuni za ndani na nje ya nchi ili kutekeleza miradi mikubwa.
CGP Minja, alitoa taarifa hiyo jana kwenye mkutano wa wadau wa Magereza waliokutana kwa siku mbili mjini hapa kwa ajili ya kutoa maoni ya kuiboresha rasimu ya Sera ya Taifa ya Magereza.
Alisema kuwa kwa sasa wanatekeleza miradi 23 kupitia shirika lao la Magereza, ambayo aliitaja kuwa ni ng’ombe wa maziwa KPF (Marogoro), mahindi Songwe (Mbeya), ushonaji Ukonga (Dar), uhunzi KPF (Moro), samani (Arusha), mbao Uyui (Tabora), sabuni Ruanda (Mbeya), na chumvi (Mtwara).
Aliitaja miradi mingine kuwa ni kilimo Mang’ola (Arusha), kilimo Ludewa (Iringa), kilimo na mifugo Isupilo (Mafinga), kilimo (Arusha), kilimo na mifugo (Kitengule), mitamba Mugumu (Mara), kilimo Kiberenge (Moro), na ng’ombe wa nyama Mbigiri (Moro).
Pia ipo ya kilimo Idete (Moro), viatu Karanga (Moshi), useremara Ukonga (Dar), kilimo Mollo (Sumbawanga), kilimo na mifugo Kitai na kilimo Mkwaya (Songea) na kilimo (Bagamoyo).
CGP Minja, alibainisha kuwa miradi ambayo shirika la Magereza limeingia kwenye ubia ni kilimo Bagamoyo ambako wameingia ubia na Kampuni ya Tarbim kutoka Uturuki kwa ajijli ya kilimo cha nafaka, matunda na usindikaji.
Vile vile shirika lao lipo kwenye mazungumzo ya ubia na baada ya kutiliana saini itatekelezwa miradi ya uchimbaji wa chokaa/lime na kiwanda cha saruji Wazo eneo la Gereza Wazo.
Katika eneo la Gereza Kihonda mkoani Morogoro, kutafanyika ujenzi wa kituo cha biashara (shopping mall), na mfuko wa mafao ya wastaafu (GEPF).
Aliongeza kuwa eneo la Gereza Karanga kutajengwa kituo kingine cha biashara, kazi itakayofanywa na GEPF wakati kwenye eneo la Gereza Isupilo mkoani Iringa, wameingia ubia na Kampuni ya bia (TBL) kulima shayiri.
Aidha, aliongeza kuwa eneo la Gereza Mollo- Sumbawanga, TBL pia watalima shayiri huku kampuni ya Lake Biochem Ltd ya hapa nchini ikiingia ubia wa kulima nafaka na miwa eneo la Gereza Kitengule.
Aliyataja maeneo mengine kuwa tayari yamepata leseni za uchimbaji madini ambayo ni Gereza Kalilankulunkulu wilayani Mpanda uchimbaji wa dhahabu, uchimbaji wa madini ya vito na dhahabu Gereza la Majimaji Songea.
Kwa mujibu wa CGP Minja, eneo lingine ni Gereza la Kitai huko Songea kutakapofanyika uchimbaji wa madini ya vito.
Aliongeza kuwa maeneo yenye leseni za uchimbaji wa madini ya ujenzi ya mawe, kokoto na mchanga na kifusi ni magereza ya Lilungu (Mtwara), Maweni (Tanga), Butimba (Mwanza), Msalato (Dodoma), Kambi Bahi (Dodoma), na Wazo (Dar).
Mkutano huo wa siku mbili ulifungwa jana na Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi, Mbarak Abdulwakil.
No comments:
Post a Comment