Dar es Salaam. Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC), Zitto Kabwe ameanika chanzo cha kufunguliwa kwa Akaunti ya Tegeta Escrow kuwa ni mgogoro ulioibuka kati ya Tanesco na IPTL.
Akitoa ripoti ya uchunguzi wa akaunti ambayo Sh306
bilioni zilichotwa na IPTL, Zitto alisema ilianzishwa chini ya wanahisa
wawili; Kampuni ya Mechmar Malaysia Berhad iliyosajiliwa Malaysia
ambayo ilikuwa inamiliki hisa saba sawa na asilimia 70 katika IPTL na
Kampuni ya VIP Engineering and Marketing iliyosajiliwa nchini ikiwa na
hisa tatu sawa na asilimia 30 ya hisa zote.
Alisema mwaka 1995, Serikali kupitia Tanesco
iliingia Mkataba wa miaka 20 na IPTL kwa ajili ya kuzalisha na kuuziana
umeme wa megawati 100 japokuwa makubaliano ya awali (MoU) yalionyesha
kuwa mkataba ungekuwa wa miaka 15.
“Hata hivyo, Tanesco ilibaini kwamba gharama za
ujenzi wa mtambo wa kuzalisha umeme ambazo IPTL iliwasilisha kwake
zilikuwa kubwa tofauti na makubaliano ya kwenye mkataba,” alisema.
Alisema IPTL ilikuwa imefunga injini zenye msukumo wa kati (medium
speed) zenye gharama ndogo na uwezo mdogo badala ya injini za msukumo
mdogo (low speed) zenye nguvu kubwa na bei kubwa.
“Wakati huohuo, IPTL waliendelea kutoza kiasi
kikubwa cha fedha kinacholingana na gharama ya ufungaji wa mtambo wenye
msukumo mdogo (low speed). Katika utekelezaji wa Mkataba IPTL walitakiwa
kufunga jenereta tano zenye uwezo wa kuzalisha megawati 20 kila moja
lakini badala yake walifunga jenereta 10 zenye uwezo wa kuzalisha
megawati 10 kila moja, jambo ambalo lilikuwa ni kinyume na makubaliano
ya mkataba,” alisema.
Kutokana na IPTL kukiuka mkataba, alisema mwaka
1998 Tanesco ilifungua kesi katika Baraza la Kimataifa la Usuluhishi wa
Migogoro ya Uwekezaji (ICSID) kupinga ukiukwaji huo na hukumu
iliyotolewa na ICSID; IPTL iliagizwa kupunguza gharama za uwekezaji
kutoka Dola 163.531 milioni hadi 127.201 milioni kwa mwezi. Alisema
ujenzi wa mitambo ulikamilika mwaka 1997, uzalishaji na uuzaji wa umeme
ulianza mwaka 2002.
Alisema kuanzia mwaka 2002, gharama za uwekezaji
kutokana na uwepo wa mtambo wa kuzalisha umeme, zilianza kulipwa na
Tanesco kwa IPTL, huku gharama za uendeshaji zikiendelea kulipwa kwa
muda wote ambao mkataba unaendelea bila ya kujali kama mtambo unazalisha
umeme au hauzalishi.
“Gharama zilikoma kulipwa moja kwa moja kwa IPTL
mwaka 2007 baada ya Tanesco kubaini kuwa IPTL inakokotoa gharama hizo
kwa msingi wa Dola 38.16 milioni (ambayo ni sehemu ya mkopo wa Dola 105
milioni uliochukuliwa na wanahisa kutoka umoja wa benki za Malaysia,
ambao baadaye ulinunuliwa na Benki ya Standard Chartered ya Hong Kong,
badala ya mtaji wa uwekezaji wa Sh50,000 uliosajiliwa Brela.)
“Hali hii ilifanya tozo ya gharama za uendeshaji
kuwa kubwa. Endapo ungetumika mtaji wa uwekezaji wa Sh50,000 katika
kukokotoa gharama za uendeshaji, Tanesco ingekuwa inalipa tozo ndogo
kuliko ilivyo sasa,” alisema.
Alisema hiyo ndiyo ilikuwa sababu ya mwaka 2004,
Tanesco kufungua kesi ya pili kupinga kiasi kikubwa cha tozo ya gharama
za uendeshaji na kwamba uamuzi wa Baraza ilikuwa ni wanahisa waketi na
mteja wao (Tanesco) na kukubaliana kuhusu kanuni ya ukokotoaji wa tozo
hiyo.
“Mpaka sasa tunapowasilisha taarifa hii bungeni,
uamuzi wa ICSID-2 kwamba IPTL ikae na Tanesco kwa ajili ya kukokotoa
upya gharama za uendeshaji haujatekelezwa, hivyo Tanesco wanaendelea
kulipa Dola za Marekani 2.6 milioni (Sh4.5 bilioni kwa mwezi),” alisema.
Escrow kufunguliwa
Zitto alisema kwa mujibu wa taarifa ya CAG, imebainika kuwa
chanzo cha mgogoro kati ya Tanesco na IPTL ambacho ndicho
kilichosababisha kufunguliwa kwa Akaunti ya Tegeta Escrow ni taarifa
ziliyoifikia Bodi ya Wakurugenzi ya Tanesco.
Alisema katika taarifa hiyo, pamoja na mambo
mengine ilifahamishwa na mmoja wa wanahisa wa IPTL, Kampuni ya VIP
Engineering, kuwa kuna viashiria kuwa Tanesco wanailipa IPTL gharama
kubwa za uendeshaji.