Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza
la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein amezindua mashindano ya Shirikisho
la Vyuo Vikuu na Taasisi za Elimu ya Juu Zanzibar (ZAHILFE) na
kusisisitiza dhamira ya Serikali ya kuendeleza na kuimarisha michezo
katika skuli na vyuo nchini.

Aliongeza kuwa kama ilivyofanyika katika kipindi kilichopita na kipindi kijacho jitihada zitaendelea kufanyika kuwahamasisha watoto kupenda michezo na hatimae kuanzisha klabu za michezo mbali mbali maskulini.Katika mnasaba huo, Dk. Shein alitoa wito kwa wazazi kuwahamasisha na kuwashajiisha watoto kupenda michezo na kwa wale ambao wanashiriki michezo kuwaunga mkono kwa kuwa michezo ni muhimu katika makuzi ya mtoto kiafya na hata kumsaidia katika kumjenga katika masomo yake.
Aliwakumbusha wazazi kuwa michezo sio sababu zinazowafanya watoto kuwa watukutu na kwamba tabia hiyo kwa watoto husababishwa na mambo mengine katika jamii hivyo watoto wapewe fursa ya kushiriki michezo kadri inavyowezekana.
Dk. Shein aliitaka jamii kuiangalia michezo katika sura tofauti na huko nyuma ambapo zaidi ilikuwa burudani lakini sasa michezo imekuwa ni sehemu inayotoa ajira nyingi na zenye manufaa kwa vijana hivyo jamii haina budi kushirikiana na Serikali kuimarisha michezo nchini.
Aliongeza kuwa lengo la kuanzisha vuguvugu la michezo maskulini na vyuo lengo lake ni kuibua vipaji na kuviendeleza ili Zanzibar iweze kutoa wanamichezo bora watakaweza kushindana na kushinda hatimae kurejesha hadhi ya Zanzibar katika ramani ya michezo ulimwenguni.
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi aliipongeza Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali kwa kusimamia vyema utekelezaji wa Sera ya Michezo nchini ikiwemo kusimamia vyema maandalizi ya mashindano mbalimbali katika ngazi zote za elimu.
Uzinduzi wa Mashindano hayo ambayo yanajumuisha michezo mbali mbali ikiwemo riadha, netiboli na mpira wa miguu ulihudhuriwa na viongozi mbalimbali pamoja na wanamichezo kutoka vyuo mbalimbali Zanzibar.