Waziri wa Mawasiliano, Sayansi na
Teknolojia wa Tanzania, Prof. Makame Mbarawa amesema kuwa, utovu wa
maadili kupitia intaneti katika nchi yake ni changamoto kubwa kwa
serikali ya Dar es Salaam. Akizungumza kwenye mahojiano maalum na Idhaa
hii, Waziri Mbarawa amesema katika kutatua tatizo hilo, serikali
imepitisha sheria ya kukabiliana na uhalifu wa mitandao ikiwa ni pamoja
na kuwabana wanaotumia mtandao kueneza mambo yanayokinzana na maadili
kama vile kupakuwa na kusambaza picha za uchi na filamu za ngono.
Kuhusiana na kutumiwa teknolojia katika kutatua matatizo ya kisiasa
nchini Tanzania na barani Afrika kwa ujumla, Prof. Makame Mbarawa
amesema teknolojia ina nafasi ya aina yake katika kupunguza matatizo
yanayojitokeza hususan nyakati za uchaguzi katika nchi za Kiafrika.
Amesema maandalizi ya chaguzi mbalimbali barani Afrika kuanzia usajili
wa wapigakura, upigaji kura, kuhesabiwa kura na kutangazwa matokeo
kunaweza kurahisishwa na kuboreshwa zaidi kupitia teknolojia za kisasa
na hivyo kuepusha ghasia na machafuko yanayoshuhudiwa katika nchi za
Kiafrika baada ya chaguzi hizo.
No comments:
Post a Comment